Friday, November 18, 2016

MGAMBO IRINGA WATAKIWA KUWA WAZALENDO


Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mshauri wa Mgambo Mkoa wa Iringa ametakiwa kusimamia zoezi la medani la komaza 2016 ili kuchochea kuwaandaa vizuri vijana kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Agizo hilo lilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua zoezi la medani komaza 2016 lililofanyika Manispaa ya Iringa.

Masenza alisema “askari hufanya mambo mengi hususani misako na doria, kupambana na majambazi, kuzuia dawa za kulevya na wahamiaji haramu na kuilinda nchi”. Aliongeza “juhudi hizo zinathibitisha kwamba jeshi la mgambo linaumuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa letu, hivyo zoezi la medani komaza 2016 liwe kichocheo kikubwa cha kuwaandaa vijana wetu kuwa askari wazuri, wazalendo, waadilifu, watenda haki, jasiri na wenye dhamira ya uaskari”.

Aliwataka wanamgambo hao kuhakikisha mafunzo watakayopewa yanatekelezwa kwa vitendo. Aliongeza kuwa askari wanaoandaliwa wawe mfano wa kuigwa katika jamii inayowazunguka. Alisema kuwa wanamgambo wengine wakipata mafunzo, huonesha ubabe kwa jamii bila sababu ya msingi. “Sisi tusifanye hivyo, mafunzo haya yatupe nidhamu ya kuwaheshimu wananchi wanaotuzunguka na kuwasaidia” alisisitiza Masenza.

Mkuu wa mkoa alipongeza juhudi za mshauri wa mgambo mkoa wa Iringa za kuwaandaa vijana wanaoshiriki mafunzo ya mgambo kuwa wakakamavu kiaskari ambao wako tayari kuilinda nchi yao na kupambana na uhalifu wa aina yoyote katika mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment