Sunday, November 19, 2017

WANAIRINGA WATAKIWA KUFANYA MAZOEZI YA VIOUNGO KUKABILIANA NA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA



Na. Dennis Gondwe, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Wananchi mkoani Iringa wametakiwa kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayosababishwa na mfumo wa maisha usiozingatia lishe bora.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akizindua kampeni tambuzi ya kifua kikuu na magonjwa yasiyoambuliza katika uwanja wa kumbukumbu ya Samora mjini Iringa jana.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza
Mheshimiwa Masenza alisema kuwa magonjwa yasiyoambukiza ni magonjwa ambayo hayawezi kuambukizwa kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine na mara nyingi hutokana na mfumo wa maisha usiozingatia afya. 

Alisema magonjwa hayo hutokana na kutokufanya mazoezi, kuwa na uzito wa juu na kula vyakula visivyozingatia lishe bora. Alivitaja vyanzo vingine vya magonjwa hayo kuwa ni uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri.

Kwa bahati mbaya, magonjwa haya hayana dalili katika hatua za mwanzoni lakini dalili huanza kuonekana pale madhara sugu yanapoanza kuonekana. Magonjwa haya ni kisukari, shinikizo la damu na saratani” alisema mheshimiwa Masenza. Alisema kuwa mazoezi ni jambo la msingi katika kuhakikisha jamii inaepuka magonjwa hayo.

Mkuu wa mkoa wa Iringa aliwomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika bustani ya Manispaa kupima afya ili ugonjwa ukigundulika tiba ianze mara moja. Aliwakumbusha wananchi kuwa huduma hiyo ni muitikio wa nia ya Rais Dr. John Magufuli ya kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na afya njema ili waweze kuchapa kazi na kuivusha Tanzania kwenda nchi ya uchumi wa kati.

Akiongelea maandalizi ya kampeni tambuzi za kifua kikuu na magonjwa yasiyoambukiza, mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza mkoa wa Iringa, Dr Tatu Mbotoni alisema kuwa timu ya madaktari na madaktari bingwa imejipanga vizuri. Alisema kuwa huduma hiyo itatolewa kwa kasi na viwango ili kuwawezesha wananchi wa Iringa kutumia muda mfupi katika kupata huduma hiyo.

Aidha, alizitaja huduma zitakazotolewa katika bustani ya Manispaa kuwa ni upimaji wa ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, VVU na upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwa wanawake.

Shirika lisilo la kiserikali la Save the Children kwa kuunga juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya njema limefadhili zoezi la upimaji afya katika mkoa wa Iringa.
=30=

No comments:

Post a Comment