Na. Dennis Gondwe, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Wananchi mkoani Iringa
wametakiwa kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya
kuambukiza yanayosababishwa na mfumo wa maisha usiozingatia lishe bora.
Kauli hiyo ilitolewa na
mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akizindua kampeni
tambuzi ya kifua kikuu na magonjwa yasiyoambuliza katika uwanja wa kumbukumbu
ya Samora mjini Iringa jana.
Mheshimiwa Masenza
alisema kuwa magonjwa yasiyoambukiza ni
magonjwa ambayo hayawezi kuambukizwa kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine na
mara nyingi hutokana na mfumo wa maisha usiozingatia afya. Alisema magonjwa
hayo hutokana na kutokufanya mazoezi, kuwa na uzito wa juu na kula vyakula
visivyozingatia lishe bora.
Alivitaja vyanzo vingine vya magonjwa hayo kuwa ni
uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri.
“Kwa bahati mbaya,
magonjwa haya hayana dalili katika hatua za mwanzoni lakini dalili huanza
kuonekana pale madhara sugu yanapoanza kuonekana. Magonjwa haya ni kisukari,
shinikizo la damu na saratani” alisema mheshimiwa Masenza.
Alisema kuwa
mazoezi ni jambo la msingi katika kuhakikisha jamii inaepuka magonjwa hayo.
Mkuu
wa mkoa wa Iringa aliwomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika bustani ya Manispaa
kupima afya ili ugonjwa ukigundulika tiba ianze mara moja. Aliwakumbusha
wananchi kuwa huduma hiyo ni muitikio wa nia ya Rais Dr. John Magufuli ya
kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na afya njema ili waweze kuchapa kazi na
kuivusha Tanzania kwenda nchi ya uchumi wa kati.
Akiongelea
maandalizi ya kampeni tambuzi za kifua kikuu na magonjwa yasiyoambukiza,
mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza mkoa wa Iringa, Dr Tatu Mbotoni alisema kuwa
timu ya madaktari na madaktari bingwa imejipanga vizuri. Alisema kuwa huduma
hiyo itatolewa kwa kasi na viwango ili kuwawezesha wananchi wa Iringa kutumia
muda mfupi katika kupata huduma hiyo.
Aidha,
alizitaja huduma zitakazotolewa katika bustani ya Manispaa kuwa ni upimaji wa
ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, VVU na upimaji wa saratani ya shingo ya
kizazi na matiti kwa wanawake.
Shirika lisilo la kiserikali
la Save
the Children kwa kuunga juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wake wanakuwa
na afya njema limefadhili zoezi la upimaji afya katika mkoa wa Iringa.
=30=
No comments:
Post a Comment