Sunday, November 19, 2017

IRINGA KUIBUA WAGONJWA WA TB NA KUWATIBU



Na Mwandishi Maalum Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Mkoa wa Iringa imejizatiti kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu ili waanze matibabu mapema na kuzuia ugonjwa huo kuambukiza wengine.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa alizindua kampeni tambuzi za kifua kikuu na magonjwa yasiyoambukiza katika uwanja wa kumbukumbu ya Samora mjini Iringa jana.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa mhe Amina Masenza

Katibu Tawala Mkoa, Bibi Wamoja Ayubu

Mheshimiwa Masenza alisema “njia kuu ya kuzuia kuenea kwa kifua kikuu ni mgonjwa kugunduliwa mapema pale anapoanza kuonyesha dalili za awali na kuwekwa katika matibabu bila kuchelewa. Mgonjwa mmoja anaweza kuwaambukiza watu wasiopungua 20 kwa mwaka. Bila ya kuweka juhudi za kuwapata wagonjwa mapema na kuwatibu, kifua kikuu kitaendelea kuenea na kuwamaliza watu wengi nchini”. 

Alisema kuwa kwa kipindi cha Januari 2016-Juni 2017, mkoa wa Iringa umeweza kugundua wagonjwa wapatao 455. Alisema kuwa kwa lengo la Manispaa ya Iringa ni kupima na kugundua watu 528 kwa kila watu 100,000. Alisema kuwa hali hiyo, inadhihirisha uhiotaji wa kupima na kugundua watu wengi zaidi.

Mkuu wa mkoa alisema kuwa ni rahisi kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu. Alizitaja dalili za kifua kikuu kuwa ni kukohoa kwa wiki mbili au zaidi na homa za mara kwa mara hasa nyakati za jioni. Dalili nyingine ni kutokwa na jasho lisilo la kawaida wakati wa usiku hata kama kuna baridi. Kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu na kupungua uzito ni miongoni mwa dalili hizo. 

Nawashukuru sana wenzetu wa shirika la Save the Children kwa kuunga juhudi za Serikali za kuwatambua na kuwapima wale watakaobainika kuwa na dalili za kifua kikuu katika jamii yetu” alisema mheshimiwa Masenza.

Alishauri kuwa mtu anapoona mojawapo ya dalili hizi kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na tiba. “Serikali bado inaendelea kutoa dawa za kifua kikuu bila ya malipo yoyote. Dawa zinapatikana katika vituo vyote vya umma na vile vya binafsi” alisisitiza mheshimiwa Masenza.
=30=

No comments:

Post a Comment