Friday, July 19, 2013

RC ATAKA JAMII ISHIRIKISHWE KATIKA UTUNZAJI WA BARABARA




Serikali mkoani Iringa imetaka jamii ishirikishwe ipasavyo juu ya dhana ya utunzani wa barabara ili kuhakikisha barabara zinadumu na kupitika muda wote. 

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Iringa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.

Dkt. Christine amesema “katika kuhakikisha tunakuwa na barabara zinazopitika muda wote, nimeona mapungufu ya ushiriki wa jamii juu ya utunzaji wa barabara hizo. Wananchi wamekuwa wakifanya shughuli ndani ya hifadhi ya barabara na kuacha uchafu kwenye barabara na uchafu huo kuziba mifereji na kuharibu barabara”. Aidha, amewataka wajumbe wa kikao hicho kutoa elimu kwa wananchi ili washiriki kikamilifu katika utunzaji wa barabara hizo ili ziweze kudumu na kuwahudumia kwa muda mrefu. Amesema kuwa uchafu unaharibu mazingira, unaziba mifereji ya barabara na kusababisha mafuriko kwenye makazi ya wananchi.

Mkuu wa mkoa wa Iringa ametoa rai kwa viongozi na wananchi kushirikiana na miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ya Iringa –Dodoma na Iringa-Mafinga. Amesema kuwa ushirikiano huo na elimu kwa wananchi utasaidia kukomesha hujuma za wizi hasa wa mafuta na ementi ili miradi hiyo iweze kuwa ya manufaa kwa mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla na kukamilika kwa muda muafaka.

Aidha, amewataka wajumbe hao kuendela kushirikiana katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya Sheria mpya ya hifadhi ya barabara ambayo ni mita 30 kil upande kutoka katikati ya barabara. Amesema “wananchi waendelee kuelimishwa juu ya umuhimu wake kwani wanapojenga na kubomolewa nyumba zao haipendezi. Inawagharimu na kuwaumiza sana” alisisitiza Mkuu wa mkoa wa Iringa.
=30=

Thursday, June 6, 2013

DKT. ISHENGOMA AKEMEA KILIMO KANDO YA RUAHA




Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amekemea tabia ya ulimaji kandokando ya mto Ruaha ili kukulinda na kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji.

Kauli hiyo ameitoka katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa Hamza Ginga ambaye ni diwani wa Kata ya Kwakilosa katika kijiji cha Kiwere Wilayani Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa tatizo la ulimaji kandokando ya mto Ruaha na mito mingine ni chanzo cha uharibifu wa mazingira. Amesema kuwa maeneo ya kando kando ya mito katika wilaya zote mkoani Iringa yamevamiwa na watu ambao wamekuwa wakilima hadi kwenye kingo za mito.amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria zinazozuia ulimaji huo, bado utekelezaji wake ni hafifu. Aidha, katika kudhibiti uharibifu huo amezitaka Halmashauri kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu hao. 

Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri na vijiji kuhakikisha ulimaji kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji unaachwa mara moja. Amesema kuwa watu wanaolima kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji na maeneo mengine yaliyokatazwa kisheria wachukuliwe hatua za kisheria. Amesema kuwa tabia ya ulimaji wa vinyungu umechangia sana kupunguza maji katika mito kutokana na kupungua kwa akiba ya maji katika maeneo oevu. Amewataka wananchi kuzingatia sheria ya maji ambayo mtu haruhusiwi kulima karibu na kingo za mito katika umbali wa mita 100 kutoka kwenye kingo ya mto. 

Dkt. Christine amewaagiza wananchi kuhakikisha kuwa miti iliyopandwa inatunzwa na kuzuia moto kichaa kuchoma miti hiyo. Aidha, ameutaka uongozi wa wilaya kusimamia kwa umakini na kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kujihusisha na uchomaji moto miti. Amewataka wananchi kuwajibika kuzuia misitu isiungue moto na kuhakikisha kuwa hakuna moto kichaa mahali popote.

Akiongelea vyanzo vya maji, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema “vyanzo vya maji ni urithi wa taifa kila mtanzania ana haki ya kufaidika na rasilimali hii. Hivyo kila mtanzania ana wajibika kutunza vyanzo vya maji”. Amewataka wale wote waliovamia vyanzo vya maji na kukata miti na kulima katika maeneo hayo  waondoke mara moja na Serikali za vijiji ziwachukulie hatua wavamizi hao. 

Siku ya mazingura duniani katika mkoa wa Iringa ilitanguliwa na shughuli mbalimbali zikiwemo kutoa mafunzo maalumu kuhusu vyanzo vya maji na elimu juu ya mpango wa usimamizi shirikishi wa misitu, kutoa elimu juu ya madhara ya uharibifu wa mazingira, kufanya kampeni za kuzuia ulimaji kandokando ya vyanzo vya majina kutengeneza barabara za moto kuzuia misitu ya asili na ya kupandwa kuungua.
=30=

UJANGILI KUWAMALIZA TEMBO NCHINI




Ujangili na uharibifu wa mazingira vinachangia sana kupunguza idadi ya tembo duniani na hasa Tanzania kutokana na tembo wengi kuuliwa na kusababisha kuathiri utalii na baadhi ya spishi za wanyamapori kuwa hatarini kupotea.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu katika mkutano wa wadau wa mtandao wa kuboresha ulinzi wa maeneo ya hifadhi kusini mwa Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo Wilaya ya Iringa.

Nyalandu amesema kuwa tafiti zinaonesha kuwa ujangili na uharibifu wa mazingira kwa pamoja vimechangia kupungua kwa idadi ya tembo dunia. Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1930 kulikuwepo na tembo milioni 50 na sasa wamepungua na kubaki tembo 402,067 tu. Amesema kuwa ujangili huo unahatarisha kupotea kwa tembo na baadhi ya spishi za wanyamapori zinazotegemea wcolojia waliopo tembo. Amesema kuwa ugangili huo unaathiri utalii pia. 

Naibu waziri wa maliasili amesema kuwa hali hiyo inaashiria kutokuwepo kwa amani na usalama katika hifadhi na uchumi wa nchi. Amesema athari ya kiuchumi ni kubwa kwa sababu ujangili unaathiri uchumi kwa sababu idadi ya watalii wanaotembelea inapungua na hatimae kupunguza pato la taifa. Amesema kuwa ujangili unaathiri sana uchumi wan chi kwa sababu asilimia 17 ya pato la taifa linategemea utalii.

 Akiongelea mbinu za kukabiliana na mtandao wa ujangili unaotumia silaha za kisasa, amesema vi vema kuongeza uwezo wa kukabiliana na njama zinazotishia kupotea kwa tembo katika sura ya dunia. Aidha, ameutaka mkutano huo kujadili kwa kina kutoka na ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya ulinzi wa rasilimali za wanyamapori hasa tembo. 

Akielezea malengo ya mkutano huo, mratibu wa mradi wa kuboresha mtandao wa maeneo ya hifadhi kusini mwa Tanzania (SPANEST) ambao pia ni waandaaji wa mkutano huo, Godwell Ole Meing’ataki ameyataja malengo kuwa ni kutoa fursa kwa wadau na viongozi wa ngazi mbalimbali katika mikoa ya nyanda za juu kusini kubadilishana uzoefu, mbinu na mikakati ya kuboresha shughuli za uhifadhi katika mikoa ya nyanda za juu kusini. Lengo jingine amelitaja kuwa ni Kuweka mikakati ya kukabiliana na wimbi la ujangili wa tembo kwa kushirikisha wadau mbalimbali kwa kutambua kuwa hakuna mamlaka moja au mdau ambaye anaweza kukabiliana na janga hili bila ya ushirikiano wa wadau wengine pamoja na Kujadili kwa undani juu ya wimbi la ujangili wa tembo katika maeneo ya hifadhi na mapori ya wanyamapori katika maeneo ya nyanda za juu kusini na nchi kwa ujumla.

=30=



Friday, May 24, 2013

RAIS KIKWETE AWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA IRINGA-DODOMA




Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa barabara ya Iringa –Dodoma itakapokamilika itasaidia kuinua uchumi wa mkoa wa Iringa na maeneo ya jirani na kuwataka wananchi kuhakikisha kuwa wanaitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Kauli hiyo ameitoa leo mchana katika hotuba yake muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi katika uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma Km 260 kwa kiwango cha lami katika eneo la Migoli.
 Rais Dkt. Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha wageni


Dkt. Kikwete amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kuinua uchumi wa mikoa ya Iringa na Dododma na maeneo ya jirani kutokana na kuwa itafungia milango ya kibiashara kwa kurahisisha usafiri kwa abilia na usafirishaji wa mizigo. Akiongelea jukumu la wananchi katika kunufaika vizuri na ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, Rais Kikwete amewataka wananchi hao kijipanga katika kuongeza uzalishaji mali na kutumia vizuri fursa zilizopo ili kunufaika kiuchumi. 

Rais Kikwete amesema pamoja na minong’ono iliyopo kwa Serikali yake inatumia fedha nyingi sana klatika ujenzi wa barabara badala ya kupeleka fedha hizo katika maeneo mengine, amesema kuwa “kama taifa tumechelewa sana kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara”. Amesema kuwa huo ni uamuzi wa makusudi wa kuwekeza kwa kasi katika miundombinu ya barabara ili kuweza kufungua fursa nyingine nyingi. Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuunganisha kwa lami mtandao wa barabara zote nchini.  

Rais Dkt. Kikwete amekemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi kuiba mafuta na vifaa mbalimbali katika miradi ya ujenzi wa barabara. Amesema kuwa wizi huo umekuwa ukirudisha nyuma muda wa utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa barabara nchini. Amewataka wananchi kuwa walinzi dhidi ya wizi wa vifaa hivyo vya ujenzi na mafuta ili kuharakisha ujenzi ujenzi na ukamilishaji wa miradi hiyo.

Akimkaribisha Rais Kikwete kuhutubia, Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli amepongeza mahusiano mazuri yanayofanywa na Rais Kikwete kwa wadau mbalimbali wa maendeleo jambo linalowezesha ujenzi wa mirandi mingi ya barabara nchini.
Dkt Magufuli ameseam kuwa mradi uliowekwa jiwe la msingi Iringa-Migori- Fufu Escarpment Km 189 unagharimu zaidi ya Tshs. Bilioni 164. 
Rais Dkt. Jakaya Kikwete akipokea maelekezo ya mradi 

Akiongelea umakini katika kusimamia miradi ya ujenzi, Waziri wa Ujenzi amesema “Mkandarasi atakayezembea tutamfukuza” na msimamizi mshauri atakayeshindwa kuongoza atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
=30=

Sunday, May 19, 2013



Na Tulizo Kilaga

Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza mikutano ya mchakato wa kupokea maoni kutoka kwa watu na makundi mbalimbali kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA).

Mkutano wa kwanza umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii kampasi ya Bustani kwa kuanza kupokea maoni kutoka kwa viongozi waliowahi kuwa mawaziri,makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka hiyo.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki wakati akifungua mkutano huo alisema Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 inaitaka Wizara kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori kazi ambayo itakamilika Novemba mwaka huu.

Mhe. Waziri alisema kuwa Wizara kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji imeamua kuanza na viongozi waliowahi kuitumikia Wizara ili waweze kutoa maoni juu ya Sheria na Muundo wa Mamlaka ya Wanyamapori pamoja na Sheria ya Idara ya wanyamapori itakayobaki katika Wizara.

“Nyalaka hizi zimetengenezwa na watu wa ndani ya Wizara wenye uzoefu wa muda mrefu na hivyo tumeona ni vizuri tuwashirikishe ninyi viongozi mliowahi kuitumikia Wizara ili muweze kutoa michango yenu itakayotuwezesha kupata kitu bora kitakachopelekwa katika Baraza la Mawaziri na kisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ili Bunge la Novemba tuweze kuiwakilisha ikiwa ina baraka na maoni kutoka kwa kamati ya Bunge ili ipitishwe kama Sheria ya Mamlaka ya Wanyamapori,” alisema Mhe. Waziri.

Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Wanyamapori kutasaidia katika kurahisisha usimamizi wa rasilimali watu, kujitegemea kimaamuzi, na kuwa na uwezo wakujiendesha yenyewe bila kutegemea fedha kutoka hadhina.

Miongoni mwa mawaziri waliohudhuria mchakato huo ni Mhe. George Kahama, Mhe. Getruda Mongella, Mhe. Ezekiel Maige, Mhe. Dkt. Juma Ngasongwa, Mhe. Zabehi Mhita na Mhe. Arcado Ntegazwa.

Makatibu wakuu waliofika ni Mhe. Philimon Luhanjo, Mhe. Marten Rumbanga, Mhe. Rose Lugembe, Mhe. Balozi Dkt. Ladislaus Komba, Mhe. Alhaj Muhidin Ndolanga, Mhe. Salehe Pamba na waliowahi kuwa wakurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.