Tuesday, March 17, 2015

UTUNZAJI MAZINGIRA NI MUHIMU KUENDELEZA RASILIMALI MAJI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Tabia ya utunzaji wa mazingira imeelezwa kuwa ni muhimu katika kuendeleza rasilimali maji mkoani Iringa.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bw. Adam Swai katika hotuba yake ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji katika mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika Kata ya Ruaha, Manispaa ya Iringa. 
Bw. Swai amesema “utunzaji wa mazingira ni kitu muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa rasilimali maji. Sote tunafahamu kuwa rasilimali maji ni muhimu kwa maisha na maendeleo ya binadamu zikiwepo shughuli za kiuchumi. Bila maji hakuna maendeleo na bila maendeleo hakuna maji,”. 

Akiongelea kusuasua kwa ujenzi wa miradi ya maji, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu ujenzi wa miradi ya maji. Aidha, amewataka kuwapatia kazi makandarasi na wataalamu washauri wenye uwezo na sifa za kufanya kazi zenye ubora. Amewataka kujiridhisha na uwezo wa makandarasi kabla ya kuwapatika kazi juu ya ubora wa utendaji kazi wao ili miradi ikamilike kwa wakati.

Akiongelea juhudi za kuongeza upatikanaji huduma ya maji mijini na vijijini, ameshauri kutumia teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua. Ameongeza utumiaji wa teknolojia ya nguvu ya jua na nguvu ya upepo katika kusukuma maji katika ngazi ya kaya na taasisi kutokana na urahisi wa teknolojia hizo.

Akiongelea hali ya upatikanaji huduma ya maji mkoani Iringa, Mhandisi wa Maji Mkoa wa Iringa, Mhandisi Shaban Jellan amesema kuwa hadi kufikia Disemba, 2014, idadi ya watu waliokuwa wakipata huduma ya maji ndani ya umbali usiozidi mita 400 toka kwenye makazi yao ni 651,917 sawa na 69.3% ya wakazi wote wa Mkoa wa Iringa.

Akiongelea huduma ya maji vijijini, amesema kuwa wakazi wa vijijini wanaopata huduma ya maji ni 452,524 sawa na 66.1% ya wakazi wote waishio vijijini. Ameitaja idadi ya wanaopata huduma ya maji kwa kila Halmashauri kuwa ni 90% sawa na wananchi 14,213 katika Halmashauri ya Manispaa (vijijini-peri-urban), 69% sawa na wananchi 175,282 katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ni 60.8% sawa na wananchi 93,722 na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi 64.8 sawa na wananchi 172,258 wanaopata huduma ya maji. 

Maadhimisho ya wiki ya maji mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo maji na maendeleo endelevu.
=30=

Saturday, March 14, 2015

WIKI YA MAJI TAREHE 16-22 MACHI, 2015

WIKI IJAYO KUANZIA TAREHE 16-22 MACHI NI WIKI YA MAJI.
JIANDAE KUSOMA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA KATIKA SEKTA YA MAJI NCHINI KATIKA MTANDAO WAKO UUPENDAO

Saturday, February 28, 2015

DC MBONI AAPISHWA RASMI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa IRINGA
Ushirikishaji wananchi na makundi mengine katika jamii ni njia rahisi ya kuleta tija katika utekelezaji wa Ilani ya CCM na miradi ya maendeleo mkoani Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza muda mfupi baada ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Mufindi, Mboni Mhita katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa. 
Mhe. Mboni Mhita (kulia) walio kaa na Mhe. Amina Masenza (kushoto). Waliosimama ni Maafisa waandamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa
 Masenza amesema kuwa katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na miradi yote ya maendeleo katika Wilaya na Mkoa dhana ya ushirikishaji wananchi na wadau wengine ni muhimu sana katika kuleta tija ya kazi. Amesema wananchi na makundi mengine yanaposhirikishwa uelewa wa pamoja unakuwepo na kufanya utekelezaji wake kuwa ni jukumu la jamii nzima. Amesema kuwa mara nyingi mtafaruku na wananchi unatokea pale ambapo ushirikishwaji unakuwa mdogo au hakuna kabisa.
Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya kusoma kwa umakini nakala ya wajibu wa Mkuu wa Wilaya na kuuelewa kwa sababu ndiyo muongozo katika utendaji kazi wa Mkuu wa Wilaya. Amesema kuwa hakuna jambo lisilowezekana na kumtaka kutumia vizuri vyombo vya usalama na wataalamu waliopo katika Wilaya ya Mufindi. Aidha, amemtaka kufanya kazi bega kwa bega na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mufindi ili kazi yake iwe nyepesi. Amesema kuwa Kamati hiyo inawajibu wa kumshauri na kumsaidia katika kutekeleza majukumu katika Wilaya ya Mufindi.
 Mkuu wa Mkoa amesema kuwa wananchi wote wanamatumaini na Wakuu wa Wilaya katika kutatua matatizo yao. “Wewe ni lulu, wananchi wote wataangaika sehemu zote watakazokwenda lakini wakifika kwako watasema hapa tumefika na hapa ndiyo mwisho. Unamwambia mwananchi nenda mahakamani hataki, nenda polisi hataki nenda kwa Mkurugenzi hataki anajua wewe ndiye utaweza kumsimamia na wewe peke yako ndiye unaweza.” Alisisitiza Masenza.
Amesema kuwa wananchi wengi wanamatumaini sana na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwa sababu wanamajibu ya papo kwa papo kwa matatizo ya wananchi kwa vile vyombo walivyonavyo vinawafanya kuwa na majibu.
Akitoa shukrani zake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mboni Mhita amemshukuru Mhe. Rais kwa imani aliyonayo kwake na kumteua katika nafasi hiyo. Aidha, ameomba ushirikiano na ushauri kadri inavyowezekana ili kazi yake iwe rahisi. Amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kumpatia nasaha na vitendea kazi. “Mbali na vitabu ambavyo umenipa vya Ilani pamoja na Katiba, maneno yako yamekuwa na uzito sana naomba nikuahidi kwamba nitayazingatia na pindi nitakapoona kwamba nimekwama au nahitaji ushauri basi sitasita kuja kwako kuomba ushauri.” Alisisitiza Mboni.
Tukio hilo la kuapishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi limeshuhudiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, familia ya Mboni, watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Mufindi, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
=30=

DC MBONI AAPISHWA RASMI

MKOA WA IRINGA WAPIGA HATUA UJENZI WA MAABARA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Uongozi wa Mkoa wa Iringa umepongezwa kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya elimu kwa kuongeza kiwango cha ufaulu.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya Mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Mhe. Pinda amesema “napongeza uongozi wa Mkoa na Wilaya zote kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya elimu.” Amesema Mkoa umefanya vizuri katika elimu ya msingi na sekondari kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi. Amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Mkoa kuhusu sekta ya elimu, ufaulu wa mtihani wa darasa la saba mwaka 2014 ulikuwa asilimia 68.5 na ufaulu wa kidato cha nne ulikuwa asilimia 65.2.
Akiongelea ufaulu wa kidato cha sita mwaka 2013, Waziri Mkuu amesema kuwa Mkoa ulifanya vizuri na katika matokeo ya kidato hicho, asilimia 99 ya watahiniwa wote walifaulu. Amesema katika matokeo hayo, shule ya sekondari Igowole ambayo ni shule ya Kata Wilayani Mufindi iliongoza kitaifa. Aidha, shule ya sekondari Kawawa pia katika Wilaya ya Mufindi ilikuwa katika 10 bora kitaifa. Kutokana na mafanikio hayo mazuri, ameutaka uongozi wa Mkoa kutokurudi nyuma.
Akiongelea agizo la Mhe. Rais la ujenzi wa Maabara za Sayansi, Mhe. Pinda amewatia moyo viongozi wa Mkoa wa Iringa ili waendelee na jitihada ya kukamilisha agizo hilo la Mhe. Rais katika kipindi kilichoongezwa hadi kufikia mwezi Juni, 2015. Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kufuatilia ujenzi wa Maabara hizo za Sayansi nchini. Amesema “wito wangu ni kwa Wakuu wa Mikoa nchini kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ujenzi wa Maabara hizo za Sayansi ili Wilaya ziweze kufikia malengo yao kabla ya mwezi Juni 2015.”
Wakati huohuo, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kujenga Maabara mpya na za kisasa zinazoendana na mazingira ya sasa. Amekosoa hatua ya baadhi ya Halmashauri kukarabati Maabara za zamani zenye majengo yaliyochakaa na kuwakumbusha kuwa lengo la serikali ni kujenga Maabara mpya za kisasa zitakazodumu.  
Mkoa wa Iringa umefikia asilimia 34 ya ujenzi wa Maabara ambayo ni sawa na Maabara 108 kati ya mahitaji ya Maabara 318. Maabara 210 zipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji.
=30=

IRINGA YAONGEZA PATO LA MWANANCHI HADI TSHS. 1,660,532

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umepiga hatua katika kuongeza pato la mwananchi kufikia shilingi 1,660,532 mwaka 2013.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku sita Mkoani Iringa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Mheshimiwa Pinda amesema kuwa pato la mwananchi wa Mkoa wa Iringa linakua vizuri, mwaka 2006 pato la mwananchi mmoja mmoja lililuwa shilingi 589,607 na limeongezeka hadi kufikia shilingi 1,660,532 mwaka 2013. “Nawapongeza wana Iringa kwa kuwa juhudi na uchapakazi ambao umeufanya Mkoa kufikia hatua hiyo na kuwa wa pili baada ya Dar es Salaam.” Alisema Mheshimiwa Pinda. Amesema kuwa pato hilo ni sawa na shilingi 138,377 kwa mwezi au shilingi 4,612 kwa siku.
Amesema kuwa viashiria vya kukua kwa uchumu ni pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa zenye umeme, elimu bora, afya bora na vifaa vya mawasiliano. Amesema kulingana na taarifa ya shirika la fedha Duniani, Tanzania imetoka miongoni mwa nchi 10 masikini Duniani na kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa.
Waziri Pinda ameutaka Mkoa wa Iringa wenye fursa kubwa ya ardhi nzuri kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara na hali ya hewa nzuri kutumia vizuri fursa hiyo. Amesema kuwa kuna fursa nyingine za kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji katika ukanda wa chini. Ameyasema hayo wakati Mkoa wa Iringa ukiwa na zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wanaotegemea kilimo. Mheshimiwa Pinda amesema kuwa uzalishaji wa mazao ni mzuri na kuhakikisha kipo chakula cha nafaka ziada ya tani 1,032,613. Katika mwaka ulioishia 2013/2014, mavuno yalifikia tani 1,379,602 za mazao ya chakula na tani 77,622 za mazao ya biashara.
=30=



Wednesday, June 25, 2014

PICHA ZA MWENGE IRINGA DC

IRINGA DC

PICHA ZA MWENGE KILOLO

KILOLO

IRINGA DC YAKOPESHA VIJANA MIL 34



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya wilaya ya Iringa imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 34 kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya vijana vinavyojihusisha na ujasiliamali ili kuongeza mtaji na kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba katika risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyosomwa na Afisa Utumishi Mkuu wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Iringa iliyosomwa katika eneo la Isimani tarafani wilayani Iringa.
Dkt. Warioba amesema “katika kipindi cha mwaka 2013/2014 halmashauri ya wilaya imetoa mikopo yenye jumla ya shilingi 34,500,000 kwa vikundi 18 vya ujasiliamali vya vijana”. Amesema kuwa halmashauri hiyo ina vikundi 177 vya vijana vyenye jumla ya wanachama 1,358 kati yao wanaume 825 na wanawake 531.
Akiongelea mikopo kwa vikundi vya wanawake, mkuu wa wilaya ya Iringa amesema “katika kipindi cha mwaka 2013/2014 halmashauri imetoa mikopo yenye jumla ya shilingi 74,950,000 kwa vikundi 50 vya ujasiliamali vya wanawake.
Kuhusu ujumbe wa Mwenge wa Uhuru, mkuu wa wilaya amesema kuwa ujumbe uliobebwa mwaka huu 2014 “katiba ni sheria kuu ya nchi” chini ya kauli mbiu isemayo ‘jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya’.
Amesema kuwa katika kutekeleza ujumbe huo wananchi na viongozi wa serikali, vyama vya siasa na madhehebu ya dini wameshiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata katiba mpya kwa kupiga kura ya maoni kupitia mabaraza ya katiba yaliyoundwa katika halmashauri ya wilaya ya Iringa. Amesema kuwa wananchi wote walishiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata katiba mpya. Amesema kuwa pamoja na wananchi kushiriki kupitia makundi mbalimbali serikali imeendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura ya maoni ili kupata katiba mpya.
=30=