Thursday, December 30, 2010

...Bibi Mpaka awapongeza walimu wa shule ya Msingi Ikonda

Walimu wa shule ya msingi Ikonda wamepongezwa kwa kuwafundisha na kufaulu mtihani wa darasa la saba mapacha walioungana kwa moyo wa huruma, upendo na kujituma.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi Gertrude Mpaka jana katika hafla fupi ya kuwapongeza na kuwapa zawadi mapacha walioungana Maria Mwakikuti na Consolata Mwakikuti baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba iliyofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Consolata iliyopo katika kijiji cha Ikonda wilayani Makete.
 Mkuu wa Wilaya ya Makete, Bibi. Zainabu Kwikwega, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,
Bibi Gertrude Mpaka na Dr. Allesandro Nava

Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa amesema “nawapongeza sana walimu wa shule ya msingi Ikonda kwa kuwafundisha watoto hawa kwa moyo wa huruma, upendo na kujituma hadi kuhakikisha wanafaulu vizuri mtihani wao wa darasa la saba”. Kufaulu vizuri kwa mapacha hawa ni mchanganyiko wa juhudi za ufundishaji makini wa walimu na jitihada zao wenyewe za kujisomea kwa bidii. Ameongeza kuwa kufaulu vizuri pia kumetokana na ushirikiano wa wanafunzi wenzao kwa kuwaonesha upendo na kuwachangamsha na hatimae kujiona ni sehemu ya jamii inayowazunguka.

Bibi Mpaka ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi wa wanafunzi waliofauli ya Mkoa wa Iringa amesema kuwa “nimekuja hapa kuwapongeza kwa kufaulu vizuri katika mtihani wenu wa darasa la saba na kuwapa zawadi”. Aidha alitoa wito kwa jamii kuwasaidia mapacha hao ili wasione kama jamii imewapa kisogo. Amewataka Maria na Consolata kusoma kwa bidii zaidi na kuongeza maarifa ili kulitumikia taifa katika kuliletea maendeleo.

 Bibi Gertrude Mpaka, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa akikabidhi
zawadi za vitabu vya sekondari kwa Consolata na Maria

Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Iringa, Mwl. Leonard Msigwa akiwa katika picha ya pamoja na
Consolata na Maria mara baada ya kukabidhi zawadi za Mkoa

Mapacha hao kwa pamoja wanamatarajio ya kusomea sayansi ya kompyuta. Aidha walisema kuwa wanaridhika sana na jamii jinsi inavyowachukulia na kutoa wito kwa viongozi wengine kuwa wanakwenda kuwatembelea.

Mkuu wa Hospitali ya Consolata- Ikonda walipozaliwa mapacha hao na muangalizi wao Padre Dr. Allesandro Nava amesema kuwa “sikushangaa kwa kufaulu kwao sababu ni wajanja sana”.

Mapacha hao walioungana walizaliwa Disemba 1997 na wamefaulu mtihani wa darasa la saba kwa alama 151 kila mmoja lakini katika masomo tofauti tofauti na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imewapangia kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya wasichana ya Jangwani iliyopo Dar es Salaam.



Cheers

Monday, December 27, 2010

WATOTO YATIMA WANAHITAJI UPENDO NA HURUMA …!
Jamii imekumbushwa kuwa watoto yatima wanahitaji upendo, huruma na kutimiziwa mahitaji yao ya msingi kama watoto wengine.

Kauli hiyo imetolewa na Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa viti maalumu (CCM) kupitia mkoa wa Iringa jana katika chakula maalumu alichokiandaa kwa ajili ya watoto yatima wa kituo cha Daily Bread Life Ministries kilichopo Mkimbizi nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.

Mhe. Ritta Kabati, Mbunge viti Maalumu (CCM) akiwa na mtoto yatima
ambaye jina lake halikufahamika mara moja katika chakula cha mchana
alichowaandalia watoto yatima wa kituo cha Daily Bread Life Ministries cha
Mkimbizi, Manispaa ya Iringa

Mheshimiwa Kabati amesema kuwa jamii lazima ikumbuke kuwa watoto yatima na wenye mahitaji maalumu ni wanajamii kama walivyo watoto wengine na wanahitaji upendo, huruma na kutimiziwa mahitaji yao ya msingi ya kila siku kama chakula, malazi, mavazi, matibabu na elimu. Jamii haiwezi kujivua jukumu hili lenye pande mbili; upande wa kiroho kama tendo la huruma na mapendo na upande wa kimwili kama kuhakikisha unatunzwa na kuuwezesha kutimiza majikumu yake ya kibinadamu.

Mheshimiwa Kabati ameelezea madhumuni ya kuandaa chakula hicho cha mchana kwa watoto yatima kuwa ni kukaa na kufurahi pamoja na watoto hao akiamini ni jambo jema hasa katika majira haya ya sikukuu. Amesema ‘kukaa na kufurahi pamoja ni jambo jema, na sisi ndiyo baba zenu na mama zenu”.

Watoto wa kituo cha makao ya watoto yatima wakijichana vilivyo

Mheshimiwa Kabati pamoja na mengine ametoa zawadi mbalimbali za Noeli kwa watoto yatima kama mablanketi, nguo, masweta, sabuni, dawa za meno, miswaki, biskuti pia aliahidi kukinunulia seti ya Luninga kituo hicho ili watoto waweze kujifunza na kufuatilia mambo yanavyokwenda ndani na nje ya nchi.

Nae Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Gervas Ndaki alisema kuwa suala la elimu kwa watoto yatima ni suala la msingi sana hivyo jamii inalazimika kuliangalia kwa jicho la karibu. Aidha aliahidi kuwalipia ada watoto wawili (2) waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza hadi watakapomaliza kidato cha nne (4).

Mhe. Ritta Kabati akikabidhi zawadi ya ndoo ya sabuni miongoni mwa zawadi nyingine

Mhe. Ritta Kabati akiwa amembeba mtoto mchanga aliyeokotwa muda jalalani muda mfupi baada ya kuzaliwa
Katika risala ya kituo hicho iliyosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa kituo, Swiga James amesema kuwa kituo chake kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo michango ya shule, gharama za matibabu kuwa kubwa kwa watoto na ubovu wa miundombinu hususani barabara kufikia kituo hicho. Aidha, alishauri iandaliwe sheria kali ya kuwadhibiti wazazi wanaokwepa majukumu yao kwa watoto.

Kituo cha Daily Bread Life Ministries kilianzishwa mwaka 2002 na kilianza rasmi kupokea watoto Aprili 2004 kutoka ustawi wa jamii na kina watoto 36, wakike 20 na wakiume 16.




 Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Clement Mshana
akiongea na Maafisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Umma walipotembelea 
kituo cha makao ya watoto yatima cha NURU, nje kidogo ya Jiji la Mbeya


 Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Clement Mshana
akikabidhi zawadi mbalimbali kutoka kwa Maafisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa
Umma katika kituo cha makao ya watoto yatima cha NURU, nje kidogo ya Jiji la Mbeya

 Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Clement Mshana
akikabidhi zawadi mbalimbali kutoka kwa Maafisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa
Umma katika kituo cha makao ya watoto yatima cha NURU, nje kidogo ya Jiji la Mbeya

 Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Clement Mshana
akikabidhi zawadi mbalimbali kutoka kwa Maafisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa
Umma katika kituo cha makao ya watoto yatima cha NURU, nje kidogo ya Jiji la Mbeya

 Neema Mbuja, Afisa Habari wa Shirika la Maendeleo la Taifa
akiwa na mtoto yatima Neema NURU


 Maafisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Umma wakiwa katika
picha na watoto yatima wa kituo cha NURU



 Maafisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Umma wakiwa katika
picha na watoto yatima wa kituo cha NURU



 Maafisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Umma wakiwa katika
picha na watoto yatima wa kituo cha NURU
 Kituo cha Kamao ya watoto yatima cha NURU
kilichopo nje kidogo ya Jiji la Mbeya

Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Clement Mshana
akifafanua jambo katika kituo cha makao ya watoto yatima cha NURU

Monday, December 20, 2010

Zamaradi Kawawa, Afisa Habari Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, 
 Mhe. Dr. Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo)
na Clement Mshana, (Mkurugenzi wa Habari Maelezo) wakibadilishana mawazo
baada ya picha ya pamoja na Maafisa Habari wa Serikali katika Hoteli ya Mbeya Forest Hill
MADIWANI WAWEZESHWA KIMAFUNZO

Serikali imeamua kuwawezesha Waheshimiwa Madiwani na watendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa mamlaka za serikali za mitaa kwa kubadili mtindo wa utendaji kazi kwa mamlaka za serikali za mitaa imeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa mafunzo ya awali kwa Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Gertrude K. Mpaka.

Mpaka amesema Serikali imedhamilia kubadili mtindo wa utendaji kazi wa mamlaka za Serikali za Mitaa, chini ya Waheshimiwa Madiwani ili madhumuni ya kuanzishwa mamlaka za Serikali za Mitaa na sera ya ugatuaji madaraka kwenda katika mamlaka za Serikali za Mitaa iweze kutimizwa kwa vitendo kwa kuwawezesha Waheshimiwa Madiwani na watendaji kutoa huduma ipasavyo kwa wakazi wa mamlaka za serikali za mitaa.

Amefahamisha kuwa mada zitakazofundishwa katika mafunzo hayo zitajikita katika sheria ambayo ndiyo msingi wa kuongoza utekelezaji wa shughuli za Halmashauri. Ameyataja maeneo mengine kuwa ni kanuni za maadili ya Waheshimiwa Madiwani na kanuni za kudumu za Halmashauri. Ameongeza maeneo mengine kuwa ni mahusiano ya utendaji kati ya Serikali kuu na Serikali za Mitaa na sheria zinazoongoza mahusiano hayo, sheria ya fedha za Serikali za Mitaa na kazi na wajibu wa diwani kwa Halmashauri yake na kwa wananchi anaowawakilisha.

Gertrude Mpaka ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa akisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa wahusika amesema kuwa mafunzo hayo yanawahusu Waheshimiwa Madiwani wote hata kama walikuwepo katika baraza la kipindi kilichopita na kusisitiza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wote kupata uelewa wa wajibu kama wawakilishi wa wananchi ndani ya ya chombo cha wananchi.

Nae mtoa mada Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa katika Sekretarieti ya mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika mahojiano maalumu amesema kuwa baada ya mafunzo hayo mabadiliko ya kifikra yataonekana dhahiri katika utendaji wa Waheshimiwa Madiwani na kuongeza mahusino baina yao na watendaji katika Halmashari yao na wananchi wanaowawakilisha.

Mafunzo hayo maalumu ya Waheshimiwa Madiwani yameandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuendeshwa na kuratibiwa na Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa.


Sunday, December 19, 2010

...MADIWANI UNGANISHENI NGUVU KUWALETEA WANANCHI MAENDELEO

Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wamekumbushwa kuwa wanalo jukumu la msingi la kuunganisha nguvu na kuwaletea maendelea wananchi wao kupitia Ilani ya chama kilichopo madarakani na kuacha siasa za chuki na kupakana matope.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu wakati wa kufungua mafunzo ya awali kwa Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mufindi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Kalalu amesema kuwa jukumu lililo mbele yao ni ni kuitekeleza Ilani ya uchaguzi ya chama kilichopo madarakani ili kuweza kuunganisha nguvu katika kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua. Aidha amesisitiza kuwa kipindi cha kampeni na ushindani wa vyama vya siasa kimemalizika baada ya uchaguzi mkuu, na kuwataka kuacha siasa za kupakana matope, chuki na fitina.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Mufindi amewakumbusha Waheshimiwa Madiwani kuzingatia kuwa baada ya miaka mitano ya kuwawakilisha wananchi katika Kata zao watawajibishwa kutokana na kazi moja ya jinsi gani alisshiriki kuwaongoza wananchi wake katika kujiletea maendeleo.

Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo amesema kuwa yatasaidia kuondoa migogoro inayotokana na muingiliano wa majukumu katika mipaka ya kiutendaji baina yao na Halmashauri wanayoiongoza. Ameongeza pia kuwa mafunzo hayo yataondoa migogoro baina ya wananchi wanaowakilishwa na Halmashauri husika.

Mafunzo hayo ya Waheshimiwa Madiwani yameandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kusimamiwa na kuendeshwa na wataalamu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa. 

Friday, December 10, 2010

…UMITASHUMTA NI VIWANGO TU

Wanamichezo na watendaji wametakiwa kuendesha mashindano na kambi ya mkoa wa Iringa kwa viwango vilivyo bora ili mkoa uweze kujivunia hazina ya vipaji iliyopo kwa wananfunzi wa shule za msingi.

Bartholomew Mwellange Mwella, Afisa Tarafa ya Makambako,
akipiga mpira kuashiria ufunguzi rasmi wa UMITASHUMTA Mkoa wa Iringa

Rai hiyo imetolewa na Bartholomew Mwellange Mwella, Afisa Tarafa ya Makambako, kwa niaba ya Katibu Tawala Wilaya ya Njombe, Evergrey Keiya wakati akifungua rasmi mashindano ya michezo ya shule za msingi ngazi ya mkoa wa Iringa uliofanyika katika Mji mdogo wa Makambako.

Mwella amesisitiza kuepuka kasoro zote zilizojitokeza hapo awali na kupelekea mashindano hayo kufutwa mwaka 2001. Aidha alisisitiza kutokuwa na uvumilivu kwa mtendaji yeyote atakayetaka kuharibu mashindano hayo kwa namna moja au nyingine.

Amesisitiza kuwa wakati wa kuchagua timu ya mkoa lazima walimu na wachezaji watakaochaguliwa wawakilishe uhalisia wa mkoa na pasiwepo na masuala ya upendeleo kwa kuangalia udugu, mahusiano mazuri na mtu Fulani, wala Halmashauri anayotoka.

Aidha amewataka washiriki kutumia vizuri fursa waliyoipata kushiriki katika michezo hii kwa kuonesha vipaji vyao na kuuwakilisha vema mkoa katika mashindano ya kitaifa. Afisa Tarafa huyo amesisitiza kucheza kwa amani na utulivu wa hali ya juu mbali na halmashauri wanazotoka kwa kuzingatia wao ni watoto wa mkoa mmoja na ni ndugu.

Akiongeleza sababu za kufutwa kwa mashindano ya UMITASHUMTA mwaka 2001 Mwella amesema kuwepo kwa mapungufu mengi ndiyo sababu ya msingi ya kufutwa kwake. Ameyataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na malezi hafifu hasa kwa wanafunzi wa kike, mapungufu ya idadi ya siku za masomo, tatizo la chakula kwa wanafunzi, watumishi kutopewa stahili zao wanazostahili, udhibiti wa nidhamu kwa wanafunzi na vyombo duni vya usafiri kwa wanafunzi hao.

Nae Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Euzebio Mtavangu ameutaja umuhimu wa mashindano hayo kuwa ni kusaidia kuibua vipaji vya wachezaji katika timu za wilaya, Mkoa na Taifa, kuimarisha afya za washiriki, kusaidia kujenga uzalendo wa kulipenda Taifa. Aidha amezitaja faida nyingine kuwa ni sehemu ya muendelezo wa vipaji vya darasani na hivyo kuwafanya wanafunzi wazingatie masomo wakati wote, kusaidia kuimarisha udugu na urafiki miongoni mwa wanamichezo.

Afisa Michezo wa Mkoa wa Iringa, Keneth Komba amesema kuwa lengo la mashindano hayo ya UMITASHUMTA ni kuwajengea umoja wanafunzi wa shule za msingi na kuwafanya wajue kuwa wao ni wamoja. Ameongeza kuwa Mkoa wa Iringa umepata heshima kubwa kuwa miongoni mwa mikoa 10 iliyoteuliwa katika kushiriki katika mashindano hayo. Mikoa hiyo ni Morogoro, Kilimanjaro, Pwani, Singida, Dodoma, Arusha, Tanga, Mbeya, Dar Es Salaam na Iringa yenyewe.

Mashindano ya UMITASHUMTA yatafanyika mjini Kibaha, Mkoani Pwani kuanzia tarehe 13 Disemba, 2010 na yatahusisha michezo ya mpira wa miguu, pete na riadha.           

IRINGA YAONGEZA KIWANGO CHA UFAULU DARASA LA SABA

Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka 2010 kutoka asilimia 59.65 ya mwaka 2009 hadi 63.01 mwaka 2010 imefahamishwa.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude K Mpaka katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2010 kilichofanyika katika kituo cha vijana cha Nazareth Njombe.

Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwl Salum Maduhu (kushoto),
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka (katikati) na
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Bibi.  Sara Dumda (kulia)

Mpaka amesema “nachukua nafasi hii kuwapongeza Maafisa Elimu wa Wilaya, Waratibu wa Elimu Kata Walimu Wakuu na walimu kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya na kufanya Mkoa wa Iringa kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 59.65 ya mwaka 2009 hadi asilimia 63.01 mwaka 2010”.

Amezitaja takwimu za watahiniwa wa kuhitimu elimu ya Msingi mwaka 2010 kuwa ni watahiniwa 44,275. Kati yao 20,991 ni wavulana na 23,284 ni wasichana. Aidha jumla ya waliofaulu ni mtihani mwaka 2010 ni 27,899 wavulana wakiwa 13,709 na wasichana ni 14,190, ambao ufaulu huo ni sawa na asilimia 63.01 ya watahiniwa wote.

Katibu Tawala Mkoa ametaja changamoto inayoukabili Mkoa katika Sekta ya elimu kuwa ni wanafunzi wanaosajiliwa kufanya mtihani kutofanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro. Amesema kuwa utoro unachukua karibu asilimia 75.19 ya watahiniwa wote. Idadi ya wanafunzi walioshindwa kufanya mtihani mwaka huu ni 566, ikilinganishwa na 816 walioshindwa kufanya mtihani huo mwaka 2009 na kuagiza litafutiwe ufumbuzi wa kina.

Akiainisha sababu za wasiofanya mtihani Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Salum Maduhu amezitaja kuwa ni utoro wanafunzi (496), vifo (18), ugonjwa (38), mamba (13), sababu nyingine (1).

Kwa upande wa mahudhurio siku ya mitihani yamepanda kutoka 98.43% ya mwaka 2009 hadi 98.74% mwaka 2010. Aidha kiwango cha kumaliza elimu ya msingi kimeshuka kutoka 80.39 (2009) hadi 76.80% (2010) ambayo ni sawa na upungufu wa 3.59%.

Kwa upande wa ufaulu na nafasi kimkoa kwa kila Halmashauri 2010 ni Iringa Manispaa 77.33% (1), Mufindi H/M 71.67% (2), Njombe Mji 71.29% (3), Njombe H/M 66.47% (4), Makete H/M 62.88% (5), Ludewa H/M 58.83% (6), Iringa H/M 42.56% (7) na Kilolo H/M 39.71% (8).

Aidha Afisa elimu Mkoa amezitaja shule 10 zilizofanya vizuri kuwa
ni St.
Benedict (Mji Njombe), Southern Highland (Mufindi), Brooke Bon (Nufindi), Livingstone (Njombe Mji), Ukombozi (Iringa Manispaa), Lupalama A (Iringa H/M), Lihogasa (Njombe Mji), Star (Iringa Manispaa), Lugarawa (Ludewa) na St. Dominic Savio (Iringa Manispaa).

Maduhu pia amewataja wahitimu wawili ambao ni mapacha walioungana kimwili, kutoka shule ya msingi Ikonda, Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Wanafunzi hawa wamefaulu na kwa mchanganuo wa alamaufuatao:

JINA
MASOMO
Kis
Eng
M/Jamii
Hisb.
Say
Jumla
Consolatha Mwakikuti
32
34
29
27
29
151
Maria Mwakikuti
32
36
25
27
31
151


Mkoa wa Iringa umekamata nafasi ya tatu kitaifa kwa miaka mine mfululizo tangu mwaka 2007 hati 2010 na unajumla ya shule 853 za msingi.