Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa mkoa wa Iringa,
Amina Masenza amezitaka Halmashauri kuhimiza matumizi ya mashine za
kieletroniki za kodi (EFDs) kwa lengo la kuongeza mapato ya serikali.
Masenza amesema hayo
alipokuwa akichangia katika taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mkoa wa Iringa kwa
mwaka 2015/2016 iliyowasilishwa na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya
Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga
katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika
ukumbi wa Siasa ni Kilimo, Manispaa ya Iringa.
Masenza amesema “umefika wakati kwa kila halmashauri kuhimiza
na kuhamasisha matumizi ya mashine za kieletroniki za kodi katika kuongeza
mapato ya serikali. Mapato ya serikali yanakwamishwa na wafanyabiashara wasio
na nia njema ya kulipa kodi halali ya serikali kwa kukwepa kutumia mashine
hizi’’. Amesema halmashauri zina wajibu wa kuwahamasisha wafanyabiashara
kutumia mashine hizo katika biashara zao.
Amesema kuwa atashangaa
kusikia halmashauri inatetea wafanyabiashara kutotumia mashine hizo. Amesema
kwa kuwa serikali inatumia kile kinachokusanywa kujiendesha ni jukumu la jamii
nzima kuhimiza matumizi ya mashine hizo.
Katibu Tawala Mkoa wa
Iringa, Wamoja Ayubu amesema pamoja na kuwa jukumu la kukusanya kodi ni muhimu
sana kwa mustakabali wa serikali, kulipa kodi kwa hiari ni kitendo cha
kizalendo. Ameitaka jamii kujivunia kulipa kodi kwa hiari hasa wafanyabiashara.
Amesema kuwa halmashauri nyingi zinashindwa kujiendesha kutokana na mianya
iliyopo katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Akiongelea umuhimu wa
matumizi ya mashine hizo, Ayubu amesema kuwa mashine hizo zinauwezo mkubwa wa
kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi ya mali ya biashara bila kufutika kwa
muda usiopungua miaka mitano na kuondokana na usumbufu wa kuchapisha vitabu vya
risiti kwa kipindi chote hicho.
=30=
No comments:
Post a Comment