Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Jamii imetakiwa kuwekeza
katika michezo kwa wanafunzi ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira
kwa vijana.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya
ya Kilolo, Selemani Mzee wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMISSETA ngazi ya
Kanda ya nyanda za juu kusini yanayofanyika katika Manispaa ya Iringa.
“Wakati taifa kwa sasa likikabiliwa na changamoto ya ukosefu
wa ajira kwa vijana, ni vema tukaelekeza nguvu katika kuimarisha sekta ya
michezo hapa nchini. Ni imani yangu kuwa endapo michezo itaimarishwa, vijana
wengi watapata ajira kuanzia kwenye vilabu vya michezo, vyama vya michezo,
mawakala wa wachezi na timu za taifa” alisema Masenza. Vijana wenye
weledi wa michezo watakaochukuliwa na timu zilizopo ndani na nje ya nchi na
kulipwa vizuri watakuwa na uwezo wa kuwekeza hapa nchini na kuweza kutoa ajira
kwa vijana wengine ambao sio wanamichezo. Amesema kuwa wote ni mashahidi kuwa
watu wanaoongoza kulipwa fedha nyingi ni wachezaji wenye uweledi.
Amesema kuwa mataifa ya
Scandinavia yameweza kupunguza gharama za matibabu katika hospitali mbalimbali
kwa wananchi wake kutokana na kuwekeza katika sekta ya michezo. Kutokana na
hali hiyo ametaka jamii kushirikiana zaidi katika kukuza sekta ya michezo
nchini. “Kwa kufanya hivyo tutaweza
kuimarisha afya za wananchi wa mikoa yetu na taifa kwa ujumla na fedha nyingi
tunazoelekeza katika sekta ya afya zitawekezwa katika miradi mingine ya
maendeleo. Napenda nitoe wito kwa wananchi wa Kanda ya nyanda za juu kusini na
taifa kwa ujumla tujenge tabia ya kuipenda michezo ili tuweze kuimarisha afya
zetu” alisisitiza Mazenza.
Akiwasilisha taarifa ya
UMISSETA Kanya, Mwenyekiti wa UMISSETA Kanda ya nyanda za juu kusini, Mwalimu Asheli
Komba amesema kuwa mashindano hayo yanakabiliwa na changamoto za uhaba wa vifaa
vya kichezo na viwanja vya michezo. Nyingine ni uhaba wa wataalam wa michezo na
baadhi ya shule binafsi kutochangia michezo na kuona shule hizo si sehemu ya
mashindano. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni ufinyu wa bajeti zinazotengwa
serikalini kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za michezo.
Mwalimu Komba amependekeza
halmashauri ziendelee kutenga fedha kadri fursa inavyopatikana ili kuendeleza
wataalam wa michezo waliopo katika halmashauri hizo. Aidha, ameshauri kuwa
mikoa na halmashauri ziendelee kuhamasisha wadau wa ndani na nje ya mikoa ili
waweze kuchangia shughuli za michezo.
Mashindani ya UMISSETA
kitaifa yatafanyika mkoani Mwanza kuanzia tarehe 8-20 Juni, 2015 na Kanda ya nyanda
za juu kusini itawakilishwa na wanamichezo mahili 136 wakati michezo
itakayoshindaniwa ni mpira wa miguu, kikapu, wavu, riadha, netiboli, meza na
bao. Michezo mingine ni tamthilia na ngoma. Kaulimbiu ya mashindano hayo mwaka
huu ni michezo ni amani, upendo na mshikamano tujitokeze kuchagua viongozi
bora.
=30=
No comments:
Post a Comment