Sunday, November 26, 2017

MATUKIO KATIKA PICHA MAHAFARI YA CHUO CHA VETA IRINGA

MATUKIO KATIKA PICHA MAHAFARI YA CHUO CHA VETA IRINGA

MATUKIO KATIKA PICHA UZINDUZI WA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MKOANI IRINGA

VETA IRINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAFUNZO STADI KULINGANA NA UHITAJI WA SOKO LA AJIRA

VETA IRINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAFUNZO STADI KULINGANA NA UHITAJI WA SOKO LA AJIRA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imetakiwa kuendelea kusimamia na kuratibu mafunzo studi nchini ili mafunzo yanayotolewa yawe na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi- Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe katika mahafali ya 21 ya chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma Iringa yaliyofanyika katika viunga vya chuo cha VETA mjini Iringa.

Mkuu wa Mkoa alisema “kimsingi mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi bado ina kazi kubwa ya kusimamia, kuratibu, kugharamia, kutoa na kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kufikia dhamira kuu ambayo ni kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira”. Aidha, aliitaka mamlaka kuendelea kuboresha fani nyingine zinazohitaji maboresha makubwa kama karakana ya magari.

Akiongelea hitaji la wahitimu la kuunganishwa na fursa zinazohusu vijana ili kuwawezesha kuendana na mbadiliko ya teknolojia na soko la ajira, alisema kuwa sualaa hilo ni changamoto. “Suala hili ni changamoto kwa mamlaka, wazazi na hata wahitimu pia. Ninapenda kutumia mahafali haya kuwashauri wazazi kushiriki kikamilifu kuwasaidia ninyi katika hali ya mmoja mmoja, lakini nikishauri zaidi kwamba ninyi wahitimu kuunda na kusajili vikundi vyenye utaratibu mzuri wa usimamizi na uzalishaji wenye faida ambavyo vitaweza kuwapa fursa ya kupata mitaji kupitia taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na mifuko ya vijana inayosimamiwa na halmashauri zetu” alisema mkuu wa Mkoa.

Akiongelea ombi la serikali kugharamia mafunzo ya vitendo, mkuu wa Mkoa alisema kuwa suala hilo linahitaji majadilianao na mamlaka husika. Aidha, aliwakumbusha wazazi kuwa wanawajibu wa kuwasaidia watoto wao kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Katika risala ya wahitimu wa chuo hicho iliyosomwa na Geofrey Simon ilieleza kuwa changamoto ni kutokuwa na walimu wa kutosha kukidhi mahitaji na uwiano sahihi katika kufundisha baadhi ya masomo. Alisema kuwa jambo hilo hupelekea walimu waliopo kuwa na mzigo mkubwa wa kufundisha idadi kuwa ya wanafunzi katika masomo ya hisabati, kiingereza, ujasiriamali na michoro ya maumbo. Changamoto nyingine ni chuo kukosa gari la kusafirishia wanafunzi waendapo kutembea maeneo ya mafunzo na michezo.

Simon aliongeza kuwa karakana nyingi za chuo zina vifaa na mitambo ya kufundishia iliyopitwa na wakati na kufanya mafunzo kutokidhi ubora wa soko la ajira. “Serikali kutokuwadhamini wanachuo fedha ya kufanya mafunzo ya vitendo, hivyo wazazi wengi kushindwa kumudu gharama husika imekuwa ni changamoto kubwa” alisema Simon.

Katika taarifa ya mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma iringa, Raphael Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kimefanikiwa katika kugharamia mafunzo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa. Alisema kuwa mamlaka imekuwa ikigharamia chakula na malazi kwa wanafunzi wanaokaa bweni.

Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kinakabiliwa na changamoto ya kuwa na vifaa vya muda mrefu visivyoendana na teknolojia ya sasa. Alisema kuwa chuo chake kina mkakati wa kuboresha karakana za mafunzo kwa kununua vifaa vipya vya mafunzo vya kufundishia. Aidha, mamlaka imeendelea kuboresha bajeti ya mafunzo mwaka hadi mwaka.

Chuo cha mafunzo ya ufundi stadi cha Iringa kilianzishwa mwaka 1987 chini ya idara ya mafunzo na majaribio ya ufundi (NVTD) iliyokuwa chini ya wizara ya kazi. Fani za kwanza kutolewa zilikuwa ni uashi, bomba, useremala na umeme.  
=30=

JAMII YATAKIWA KUAMKA KUTETEA USAWA WA KIJINSIA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Wanawake na watoto wameendelea kuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka kutokana na mwamko mdogo wa jamii kuhusu usawa wa kijinsia.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, uliofanyika ngazi ya mkoa katika halmashauri ya wilaya ya Kilolo na kusomwa kwa niaba yake na mganga mkuu wa mkoa Dr Robert Salim.

Mkuu wa Mkoa alisema “katika mkoa wetu wa Iringa, vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikifanyika katika maeneo mbalimbali, wanawake na watoto wamekuwa ndiyo wahanga wakubwa. Kwa mfano, wanawake wameendelea kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka kati yao na wanaume, kukosekana kwa usawa kunakichangiwa na mfumo dume uliopo katika jamii, wanawake kunyanyaswa, kubaguliwa, kupigwa, kutelekezwa na watoto, kutokushirikishwa katika maamuzi hata yale yanayohusu maisha yao”. 

Aliongeza kuwa watoto pia wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi katika jamii.

Mkuu wa mkoa alisema kuwa kumekuwa na matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa, mimba za utotoni, kupigwa na kuterekezwa. ”Idadi ya watoto waliofanyiwa ukatili wa aina tofauti kwa kipindi cha kuanzia Julai 2016- hadi Oktoba, 2017 imefikia watoto 606. Watoto 306 wameripotiwa kufanyiwa ukatili wa kingono na watoto 300 ukatili mwingine kama kupigwa na kadharika. Inashangaza kuona kwamba idadi kubwa ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimekuwa vikifanywa majumbani, shuleni au njiani, ukatili huu umekuwa ukifanywa na watu au ndugu wa karibu wa familia husika” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili, wanawake 904 wamefanyiwa ukatili. Ukatili huo umewaathiri kiafya, kijamii, kisaikolojia na kiuchumi. Ukatili wa kijinsia umekuwa ukichangia kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa mengine yatokanayo na ngono.
 =30=

TANZANIA MSTARI WA MBELE KUPINGA UBAGUZI KWA WATOTO NA WANAWAKE



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuheshimu haki na utu wa mwanamke kwa kutekeleza mkataba wa umoja wa mataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya watoto na wanawake.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika maelezo yake wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliyofanyika ngazi ya mkoa katika halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na kusomwa na Afisa maendeleo ya jamii katika Ofisi ya mkuu wa mkoa, Saida Mgeni.

Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa nchi ya Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuheshimu haki na utu wa mwanamke kwa kutekeleza mkataba wa umoja wa mataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto ambao Tanzania imeusaini na kuuridhia. 

Serikali kwa kushirikiana na wanasiasa, viongozi wa dini, mashirika ya hiyari na watu binafsi wamekuwa wakitumia kampeni hii kuhamasisha jamii kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Alisema kuwa maadhimisho haya yalenge kutafakari mafanikio na changamoto zinazoikabili jamii na kuandaa mkakati wa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari 2016-septemba, 2017, wanawake 904 wamefanyiwa ukatili wa aina moja au nyingine. Aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia unachangia maongezeko ya maambukizi ya virusi vya ukimwi. 

Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye kiwngo kikubwa cha mambukizi ya vvu. Watu wenye umri wa miaka 15-49 ambao ni asilimia 9.1 na maambukizi ya wanawake ni asilimia 10.2 ikilinganishwa na asilimia 6.9 ya wanaume. Kitaifa ni asilimia 5.1 ambapo wanawake ni asilimia 6.3 na wanaume asilimia 3.5” alisisitiza Katibu Tawala Mkoa.

Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ilizinduliwa ngazi ya Mkoa, katika Kijiji cha Lyasa, Kata ya Image Wilaya ya Kilolo chini ya kaulimbiu ya isemayo ‘funguka! Ukatili dhidi ya wanawake na watoto haumuachi mtu salama chukua hatua’.     
=30=

Thursday, November 23, 2017

WAKULIMA IRINGA WATAKIWA KUTUMIA VIZURI MVUA ZA MWANZO KUPANDIA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Wakulima mkoani Iringa washauriwa kuzitumia vizuri mvua zilizoanza kunyesha kupanda kwa kutumia mbegu bora na kuzingatia mistari.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akiongea katika kipindi cha moja kwa moja cha Sunrise power kinachorushwa na kituo cha redio Nuru cha mjini Iringa jana.

Mheshimiwa Masenza alisema kuwa mvua zilizoanza kunyesha zitumike vizuri kwa kupandia. Aliwataka wakulima kuchagua mbegu bora zilizoidhinishwa na wataalam ili waweze kupata mazao bora. Aidha, alishauri kufuata ushauri wa wataalam wa akilimo ili kupata tija kupitia kilimo.

Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa iliyo mstari wa mbele katika kilimo cha mazao ya chakula katika mikoa ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania.
=30=

VYAMA VYA SIASA VYAASWA KUFANYA KAMPENI KISTAARABU



Na. Dennis Gondwe, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Vyama vya siasa mkoani Iringa vimetakiwa kufanya kampeni za kistaarabu na kuachana na vitendo vya vurugu kwa sababu serikalai ipo macho muda wote.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akiongea katika kipindi cha Sunrise power kinachorushwa na kituo cha redio Nuru cha mjini Iringa jana.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza (picha na maktaba)
Mheshimiwa Masenza ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Iringa alivitaka vyama vya siasa kuendesha kampeni za kistaarabu katika maeneo utakapofanyika uchaguzi mdogo wa madiwani. 

Napenda mkubuke kuwa baada ya uchaguzi maisha yanaendelea kama kawaida. Kila chama lazima kipige kampeni kwa uhuru na ustaarabu bila kusababisha viashiria vya vurugu” alisema mheshimiwa Masenza. 

Aliongeza kuwa mtu yeyote atakayefanya vurugu afahamu kuwa serikali ipo macho itamshughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi.

Uchaguzi mdogo wa madiwani unatarajiwa kufanyika tarehe 26/11/2017 katika Kata za Kitwiru na Kimala katika halmashauri za Manispaa na Kilolo mtawalia katika mkoa wa Iringa.
=30=