Thursday, December 21, 2017

UBIA SEKTA YA UMMA NA BINAFSI WAONGEZA UFANISI SAGCOT


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mafanikio ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi yamebadilisha fikra na kuongeza ufanisi kwa watendaji wa sekta ya umma katika mikoa ya Iringa na Njombe katika utekelezaji masuala ya ubia.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya mafanikio ya SAGCOT kwa Mkoa wa Iringa wakati wa ziara ya Katibu mkuu Ofisi ya waziri mkuu anayehusika na sera na mipango mkoani Iringa jana.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu akisoma taarifa ya Mafanikio ya SAGCOT kwa Mkoa wa Iringa

Ayubu alisema “moja ya mafanikio ya ubia uliyopo ni kubadilika kwa fikra na kuongezeka kwa ufanisi kwa watendaji wa sekta ya umma katika utekelezaji wa masuala yanayohusu ubia na sekta binafsi”. 

Alisema kuwa Mkoa uliweza kufuatilia changamoto mbalimbali na kufanikisha upatikanaji wa umeme kwenye kiwanda cha kusindika nyanya kiitwacho Darch Industries Ltd. Aliongeza kuwa upatikanaji wa barabara kutoka kiwanda hicho cha kusindika nyanya hadi barabara kuu ya Iringa-Mbeya uliwezeshwa. “Upatikanaji wa maeneo kwenye vijiji vinavyozalisha zao la nyanya kwa ajili ya kujenga vituo vya kukusanyia nyanya. Vituo vinane vimejengwa na wabia wa kiwanada cha kusindika nyanya” alisema Ayubu.

Katibu Tawala Mkoa alizitaja juhudi zilizofanywa na Mkoa kuwa ni pamoja na kutatua mgogoro wa matumzi ya maji kati ya muwekezaji (Silverlands) na wananchi ambapo hati ya makubaliano ya matumizi ya maji ilisainiwa na pande zote mbili. Pia, Mkoa umefanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika kiwanda cha kusindika chai cha Unilever.

Kongani ya Ihemi (Iringa na Njombe) inajumuisha wilaya za Iringa, Kilolo, Mufindi, Njombe na Wanging’ombe ilianza utekelezaji chini ya mpango wa SAGCOT mwaka 2015 ikiwa ya kwanza kati ya kongani sita za SAGCOT.

=30=

Saturday, December 16, 2017

SERIKALI YATHAMINI MCHANGO WA WADAU WA MAENDELEO IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na wadau wa maendeleo katika kuongezea mahali ambapo serikali inaishia katika kuwahudumia wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa mganga mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr Atupele Mwandiga alipokuwa akifunga kikao cha kuutambulisha mradi wa ‘USAID Tulonge Afya’ kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hills mjini Iringa jana.
 
Dr Atu Mwandiga

Dr Mwandiga alisema kuwa wadau wa maedeleo wamekuwa msaada mkubwa katika kuchangia juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake. 

Wadau wa maendeleo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa sana katika kuwaletea maendeleo na kuboresha afya za wananchi wetu. Uwepo wenu katika Mkoa huu umeongeza kasi ya serikali ya Mkoa na Halmashauri zake ya kuwafikia wananchi katika jitihada zao mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maisha, hasa kujikwamua kiuchumi na kuimarisha afya zao” alisema Dr Mwandiga.

Dr Mwandiga aliwapongeza waandaaji wa mradi huo kwa kuchagua kutumia mbinu za mabadiliko ya tabia kwa wanajamii (SBCC). Alisema kuwa mbinu hiyo imekuwa ikitoa matokeo chanya inapotumika vizuri.

Dr Mwandiga aliwaagiza waganga wakuu wa Wilaya kusimamia vizuri na kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo kupitia mbinu za mabadiliko ya tabia kwa wanajamii.
=30= 

SERIKALI ZA MITAA IRINGA ZIWATUMIE MAAFISA HABARI KUHABARISHA UTEKELEZAJI MIRADI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mamlaka za serikali za mitaa na wadau wa maendeleo wametakiwa kuwatumia maafisa habari wa serikali katika kuhabarisha utekelezaji wa miradi ili wananchi waweze kunufaika na huduma zao.

Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa mganga mkuu wa mkoa wa Iringa, Dr Atupele Mwandiga alipokuwa akifunga kikao cha kuutambulisha mradi wa USAID Tulonge Afya kwa wadau wa Mkoa wa Iringa katika hoteli ya Gentle Hills mjini Iringa jana.
 
Dr Atupele Mwandiga
Dr Mwandiga alisema kuwa mafanikio ya miradi inayotekelezwa kwa wananchi yanategemea na utoaji na upatikanaji wa taarifa za huduma zinazotolewa. 

Vivyo, hivyo mafanikio ya mradi huu wa ‘USAID Tulonge Afya’ pamoja na mambo mengine utategemea sana upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa za huduma na mafanikio. Na hili ni jukumu la maafisa habari wa serikali. Bahati nzuri kwa Mkoa wetu wa Iringa, serikali imeajiri maafisa habari katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri zote. Ni matumaini yangu kuwa wataalamu hawa watatumika vizuri katika kufikia malengo ya mradi huu” alisema Dr Mwandiga. 

Aidha, aliwataka kuwatumia pia maafisa maendeleo ya jamii walio katika kata zote za Mkoa wa Iringa katika kutekeleza mradi huo.
=30=

MATUKIO KATIKA PICHA UTAMBULISHO WA MRADI WA USAID TULONGE AFYA MJINI IRINGA






WADAU WA VVU/UKIMWI IRINGA WATAKIWA KUJITATHMINI



Na Ofisi ya mkuu wa Mkoa
Wadau wa mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na Ukimwi wametakiwa kujitathmini katika utekelezaji wa mkakati wa kupambana na VVU baada ya mbinu za awali kuonesha kushindwa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao cha kuutambulisha mradi wa USAID Tulonge Afya kilichofanyika katika hoteli ya Gentle Hills iliyopo mjini Iringa.
 
RAS Wamoja Ayubu
Ayubu alisema matokeo ya utafiti wa VVU na UKIMWI (2016/2017) yameonesha kuwa maambukizi ya VVU mkoani Iringa yameongezeka kutoka asilimia 9.1 hadi 11.3. “Maambukizi ya VVU mkoani Iringa yameongezeka kutoka asilimia 9.1 ya awali (2011/12) kufikia asilimia 11.3 (2016/17). Hii ni ishara wazi kuwa maambukizi mapya yameongezeka kwa asilimia 2.2” alisema Ayubu.

Aidha, aliwataka wadau wa mapambano dhidi ya VVU kujitathmini ili kuona maeneo ambayo hawakufanya vizuri. 

Tunatakiwa tujitathmini kuona ni wapi ambapo hatujafanya vizuri katika utekelezaji wa program zetu za mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU” alisema Ayubu.

Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa wadau wa maendeleo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika kuwaletea maendeleo na kuboresha afya za wananchi mkoani Iringa. 

Uwepo wenu katika Mkoa huu umeongeza kasi ya serikali ya Mkoa na Halmashauri zake ya kuwafikia wananchi katika jitihada zao mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maisha, hasa kujikwamua kiuchumi na kuimarisha afya zao” alisema Ayubu.
=30=

USAID TULONGE AFYA WATAKIWA KUTUMIA FEDHA ZA MRADI KWA MALENGO KUSUDIWA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watekelezaji wa mradi wa USAID Tulonge Afya wametakiwa kutumia fedha za utekelezaji kwa mujibu wa taratibu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao cha kuutambulisha mradi wa USAID Tulonge Afya kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hills iliyopo mjini Iringa jana.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Ayubu alisema kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zinatolewa na serikili ya Marekani kupitia shirika la maendeleo la Marekani USAID. 

Naomba fedha hizi zikatumike kwa kufuata utaratibu ili kufanikisha kufikia malengo yake. Nataka niwakumbushe kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kikamilifu katika kusimamia na kufuatilia matumizi sahihi ya fedha za wadau wa maendeleo na za serikali kwa lengo la kuhakikisha kuwa thamani ya fedha kwenye miradi ya maendeleo inazingatiwa na watekelezaji” alisema Ayubu.

Alisema kuwa mradi huo unalenga kuhamasisha wanajamii kutumia huduma za afya zinazotolewa kwenye vituo vya afya. 

Ninawahakikishia kuwa serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana nanyi katika uboreshaji wa huduma ili wananchi wakishahamasika waweze kwenda vituoni na kupata huduma zilizo bora” alisema Ayubu.
=30=