Tuesday, September 25, 2012

IRINGA TUMIENI FURSA YA UTALII




Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amewataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya maadhimisho ya siku ya utalii duniani yanayofanyika kimkoa katika manispaa ya Iringa kutembelea maonesho hayo na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ili kuweza kupata elimu na taarifa z utalii.

Wito huo ameutoa katika hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya utalii duniani yanayofanyika kimkoa katika uwanja wa Samora, Manispaa ya Iringa.   
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (wa kwanza kulia) akiwa katika moja ya mapango ya kihistoria katika kuhamasisha utalii wa ndani.

Dkt. Christine amesema “natoa wito kwa wananchi wote kutumia fursa hii kutembelea maonesho na kushiriki  katika shughuli mbalimbali za maadhimisho haya”.

Amesema maonesho hayo yatatoa fursa ya kufahamiana na kupanua wigo wa kufanya biashara za utalii. Amesema kuwa maadhimisho yatahusisha maonesho ya bidhaa na shughuli mbalimbali za kitalii, michezo, kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo mkoani Iringa na kutoa elimu kuhusu uendeshaji wa biashara za utalii.

Akielezea madhumuni ya maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa madhumuni ya maadhimisho hayo ni Kutoa umuhimu wa sekta ya utalii kwa maendeleo ya mwanadamu katika nyanja mbalimbali. Amezitaja nyanza hizo kuwa ni pamoja na utamaduni, uchumi, mazingira pamoja na nyingine.

Dkt. Christine amesema kuwa matokeo ya maadhimisho hayo hayawezi kuonekana kwa muda mfupi kwa sababu ni suala linalohitaji hamasa ya muda mrefu. Ameelezea matumaini yake kuwa Mkoa wa Iringa utazidi kuendeleza kwa kasi iliyopo, ukuaji wa utalii na hatimae wananchi kunufaika na utalii huo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mkoa wake umejaaliwa kuwa na vivutio Vinci vya utalii ambavyo bado havijafahamika sana kwa wananchi na wadau wengine. Amevitaja vivutio vilivyopo kuwa ni pamoja na mila na desturi za watu wa ukanda huo, maeneo ya hifadhi za mimea na wanyama, mandhari nzuri na za kuvutia, maeneo ya kilimo, maporomoko ya maji na maeneo ya kihistoria.

Nae mwenyekiti wa Kamati ya kuendeleza utalii kwa mkoa wa Iringa ambae pia ni katibu Tawala msaidizi, Sehemu ya Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Adam Swai amesema kuwa malengo mahususi ya kufanya maadhimisho katika manispaa ya Iringa ni kuhamasisha wadau mbalimbali kutambua umuhimu wa sekta ya utalii katika kujiletea maendeleo. Ameyataja maadhimisho hayo kuwa ni chachu ya kuendeleza sekta ya utalii katika ukanda wa Kusini ili wananchi waweze kufaidika na utalii huo.

Ikumbukwe kuwa Mkoa wa Iringa ulitangazwa na serikali kuwa kutovu cha kuendeleza utalii kwa Ukanda wa kusini mwaka 2009. aidha, maadhimisho hayo yatafanyika kwa siku tatu, kuanzia tarehe 25 hadi 27 Septemba 2012.
=30=

Friday, September 21, 2012

NENDA KWA USALAMA KUKUMBUSHA SHERIA NA TARATIBU



Wiki ya nenda kwa uslama barabrani inalenga kuwakumbusha madereva na watumiaji wa barabara juu ya sheria na taratibu za matumizi mazuri ya barabara kwa usalama wa watumiaji na vyombo vya moto nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkaguzi wa Polisi, Abel Baetazal Swai kutoka Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani, Kitengo cha Elimu alipokuwa aliwaelimisha wananchi wa Manispaa ya Iringa katika Banda la Polisi lililopo katika uwanja wa maonesho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yanayoendelea mjini Iringa.
Mkaguzi Swai amesema kuwa maana halisi ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani n kufanya marejeo kwa madareva ambao wamepitia mafunzo ya udereva kuweza kukumbushwa sheria na taratibu pindi wanapokuwa barabarani. Amesema kuwa polisi wanakuwa wanatoa elimu kwa makundi mbalimbali yanayotumia vyombo vya moto kwa namna moja na ambayo hayatumii vyombo hivyo kwa namna nyingine. Amesema kuwa katika kipindi hicho kazi nyingine zinazofanyika ni pamoja na kukagua magari bure. 

Akielezea tathmini yake juu ya hali ya usalama barabarani Mkaguzi wa Polisi Swai amesema kuwa hali si mbaya kwa sababu elimu inayotolewa imekuwa ikiwasaidia sana madereva na watumiaji wengine wa barabara kurejea katika sheria na taratibu za usalama barabarani.  Amesema kuwa elimu hiyo imekuwa ikitolewa katika shule na mikusanyiko mbalimbali, na majaribio ya tathmini yaliyofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani inaonesha kupungua kwa ajali za barabarani. 

Mkaguzi wa Polisi Swai amesema kuwa elimu hiyo imekuwa ikitolewa kwa shule za msingi na sekondari na kupitia vipindi mbalimbali vya redio na vyombo vingine vya habari.
Akielezea vyanzo vya ajali, Swai amevitaja vyanzo hivyo kuwa ni miundombinu duni, makosa ya kibinadamu na vyombo vyenyewe. Amesema mkusanyiko wa vyanzo hivi ndiyo huchangia sana katika ajali za barabarani.

Wakati huohuo, Afisa wa Polisi, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kitengo cha kuzuia Uhalifu, Mariam Mruma wakati akifafanua juu dhana ya kuzuia uhalifu katika makazi na vyombo vya moto amesema kuwa ni vema wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari zote dhidi ya uhalifu katika maeneo yao. Amesema Jeshi la Polisi linatumia maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kutoa elimu kwa jamii dhidi ya kuzuia uhalifu katika makazi na vyombo vya moto. Amesema katika magari ni vizuri wananchi kukokuacha vitu vya thamani ndani ya magari kwa sababu vitu hivyo vinawashawishi wahalifu kutenda kosa na kushauri pia wanapoyapaki magari yao kuyapati katika maeneo yaliyo wazi na yenye mwanga si maeneo ya vificho. 

Mruma amesema kuwa katika makazi si vizuri kuwakaribisha nyumbani watu wasio fahamika vizuri kwa sababu wanaweza kutumia nafasi hiyo kusoma mazingira ya nyumbani hapo na hatimae kufanya uhalifu. Amesema ni vizuri kwa serikali za mitaa kufahamishwa juu ya ugeni wowote unaofika katika maeneo yao na majirani kwa tahadhali ya kiusalama. Aidha, ametoa wito kwa wazazi kuwaelimisha mtoto wao juu ya kuchukua tahadhari dhidi ya vitendovya udhalilishaji na pindi vinapotokea waweze kutoa taarifa kwao au kwa walimu kwa wale wao shule.
=30=

WANANCHI LINDENI MIUNDOMBINU YA ELIMU



 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa jukumu la ulinzi wa miundombinu ya elimu kama majengo ni jukumu la jamii nzima na sijukumu la jeshi la polisi wala shule husika pekee. 

Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akiongea na wananchi wa kata ya Ifunda iliyopo wilayani Iringa kuhusu nafasi ya jamii katika ulinzi wa miundombinu ya elimu hasa baada ya shule ya sekondari ya St. Mary’s Ulete kuungua kwa baadhi ya mabweni na kusababisha uharibifu wa mali za shule na wanafunzi alipokwenda kukagua shule hiyo.

Amesema “tufanye kazi moja muhimu nayo ni kulinda shule na sehemu nyingine ili moto usitokee tena na kila mmoja lazima awe na uchungu kuona moto ukitokea na kuteketeza mali za shule na wanafunzi” alisisitiza Dkt. Ishengoma. Amesema kuwa shule hizo pamoja na kumilikiwa na serikali na taasisi bado zinawahudumia wananchi wote hivyo usalama ni jukumu la jamii nzima. Amesema kuwa pindi shule zinapoathiriwa na majanga ya moto husababisha wanafunzi kufunga shule na kurudi nyumbani. Amesema kuwa jambo hilo limekuwa likisababisha ufumbufu mkubwa kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kupoteza muda wa masomo. 

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameagiza kufanyika kwa mafunzo ya mgambo katika kata ya Ifunda ili kuwafanya wananchi wawe wakakamavu na kujihakikishia ulinzi na usalama katika eneo lao. Amesema kuwa mafunzo ya mgambo ni mafunzo muhimu sana na hufanyika kwa muda mfupi lakini huwa na matokea chanya katika jamii.
Katika taarifa fupi ya shule iliyosomwa na Mkuu wa Shule, Matholinus Kibuga amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na tatizo la moto wa mara kwa mara katika eneo la mabweni. Amesema kuwa ndani ya miezi miwili shule hiyo imekumbwa na majanga ya moto mara mbili na kusababisha hasara kubwa. Amesema kuwa tarehe 20 Julai, 2012 moto ulisababisha uharibifu wa mali za shule na wanafunzi zenye thamani ya shilingi milioni 9. Amesema moto wa tarehe 15 Septemba, 2012 ulisababisha hasara ya mali zenye thamani ya shilingi milioni 80, 400,000. 

Amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na tatizo la wizi wa mali za shule na ukosefu wa nishati ya kudumu kwa ajili ya mwanga na matumizi mengine. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni ukosefu wa uzio kwa ajili ya kusaidia ulinzi na usalama kwa wanafunzi na mali za shule. 

Akielezea hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo, Mkuu wa shule hiyo amesema kuwa shule yake imeajiri walinzi kutoka kampuni ya ulinzi ya Mwazuma iliyopo mjini Iringa kwa lengo la kukabiliana tatizo la wizi na moto wa mara kwa mara shuleni hapo. Amesema kuwa majadiliano yanafanyika ili kuhakikisha uzio wa shule hiyo unajengwa haraka. Kuhusu changamoto ya nishati, amesema kuwa katika kipindi hiki shule yake inatumia jenereta dogo na kwa dharura kama chanzo cha nishati ya mwanga na kuiomba serikali kufanya juhudi za makusudi za kufikisha nishati ya umeme katika shule hiyo.
Akielezea nafasi ya kanisa katika kuihudumia jamii, Paroko msaidizi wa Parokia ya Ulete, Padre Augustine Kamunyuka ambaye parokia yake ndio wamiliki wa shule hiyo ya sekondari, amesema kuwa lengo la msingi la kanisa ni kumlea mwanadamu kiroho na kimaadili. Amesema kwa msingi huo ili kufanikisha jukumu hilo kanisa pia linahudumia pia mwili pamoja na mambo mengine. 

Amesema katika kufanikisha hilo, kanisa limekuwa likiendesha shule ya ufundi ya ushonaji, ujenzi na uselemala. Amesema pia kanisa katika parokia hiyo limekuwa likiendesha shule ya sekondari, zahanati, shule ya chekechea na kutoa huduma za maji kwa jamii. Amesema kanisa limekuwa likitoa huduma hizo pasipo kufikiria kujipatia faida bali kwa kutekeleza wito wao.

Shule ya sekondari St. Mary’s ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza 35. Kwa sasa shule hiyo inawanafunzi 376 wakiwa ni wasichana 160 na wavulana 216. Kati ya mwaka 2010-2011 wanafunzi wote walifauli wa kidato cha nne katika mitihani ya kitaifa.
=30= 

Tuesday, September 18, 2012

WIKI YA NENDA KWA USALAMA KITAIFA IRINGA

 Mwenyekiti wa Baraza la Nenda kwa Usalama Barabarani, Salim Abri na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka (kushoto) wakiwa katika wakati wa furaha ndani ya uwanja wa Samora yanapofanyika maonesho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarari yanayofanyika kitaifa mkoani hapa.


 Maandamano ya wadau mbalimbali wakiingia katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa kwenye Maonesho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarari yanayofanyika kitaifa mkoani hapa.


 Bendi ikiongoza Maandamano ya wadau mbalimbali kuingia katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa kwenye Maonesho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarari yanayofanyika kitaifa mkoani hapa.

Picha ya pamoja ya wadau wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi (wanne kulia waliokaa) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (wa tano kulia waliokaa) katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa.


MITIHANI YA DARASA LA SABA KUANZA KESHO


Mikoa ya Iringa na Njombe imejipanga kuhakikisha kuwa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2012 inafanyika katika hali nzuri na kutokuruhusu mianya yoyote ya udanganyifu na kusababisha kufutiwa kwa matokeo kwa baina ya shule za msingi.

Akifafanua maandalizi ya mitihani hiyo ofisini kwake, Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Joseph Mnyikambi aliyepewa pia jukumu la kusimamia mitihani hiyo kwa mikoa ya Iringa na Njombe amesema kuwa tayari semina zimeendeshwa na kamati ya usimamizi wa mitihani ya mkoa katika Halmashauri zote nane za mikoa ya Iringa na Njombe. Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Njombe, Mufindi, Makete, Ludewa, Kilolo, Iringa, Njombe Mji na Iringa Manispaa.

Akiongelea maandalizi amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na leo ndiyo siku ya kuwapeleka wasimamizi katika vituo vyao ya kusimamia mitihani hiyo. Amesema “kwa mujibu wa sheria zetu huwezi kumwambia msimamizi atasimamia wapi mtihani huo”. Amesema kuwa lengo ni kuzuia udanganyifu na hongo kutoka kwa jamii kwenda kwa msimamizi na kutoka kwa msimamizi kwenda kwa jamii pamoja na wanafunzi.

Kuhusu taratibu, Mwalimu Mnyikambi amesema kuwa taratibu ni za kawaida na zilizozoeleka isipokuwa kitu kipya ni mwaka huu watahiniwa wote watatumia penseli na fomu maalumu kujibu mitihani hiyo kwa kusiliba kwa sababu kwa mara ya kwanza itatumika teknolojia mpya ya ‘optical mark reader’ (OMR). Amesema kuwa majibu yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta.

Amesema kuwa mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili na itaanza kesho tarehe 19 -20 Septemb, 2012. masomo yatakayotahiniwa ameyataja kuwa ni Sayansi, Hisabati na Kiswahili. Mengine ni Kiingereza na Maarifa ya Jamii.

Ni kwa namna gani mkoa umejipanga kukabiliana na udanganyifu unaoweza kusababisha wanafunzi kufutiwa matokea, Afisa elimu mkoa wa Iringa amesema “kama mkoa tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa udanganyifu haufanyiki katika mikoa ya Iringa na Njombe kwa kuzingatia taratibu zote za mitihani”. Ameitaja miongoni mwa mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kila mwanafunzi kukaa katika dawati lake na kukaa mmoja ili kuondoa uwezekano wa kutizamiana. Amesema katika semina kwa wasimamizi wa mitihani, msisitizo ulikuwa ni kuhakikisha hakuna udanganyifu wowote utakaopewa nafasi katika mtihani huo ili kuhakikisha kila mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza anajua kusoma na kuandika na anakwenda kwa kufaulu vizuri.

Mwalimu Mnyikambi ameitaja idadi ya wanafunzi watakaofanya mitihani hiyo ya kumaliza elimu ya msingi kwa mikoa ya Iringa na Njombe kuwa ni 43,499 kati yao wasichana ni 23,015 na wavulana ni 20,484. amesema jumla ya shule zote ni 887.
=30=