Sunday, May 31, 2015

RC MASENZA AITAKA JAMII KUWEKEZA KWENYE MICHEZO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Jamii imetakiwa kuwekeza katika michezo kwa wanafunzi ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Selemani Mzee wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMISSETA ngazi ya Kanda ya nyanda za juu kusini yanayofanyika katika Manispaa ya Iringa.

“Wakati taifa kwa sasa likikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, ni vema tukaelekeza nguvu katika kuimarisha sekta ya michezo hapa nchini. Ni imani yangu kuwa endapo michezo itaimarishwa, vijana wengi watapata ajira kuanzia kwenye vilabu vya michezo, vyama vya michezo, mawakala wa wachezi na timu za taifa” alisema Masenza. Vijana wenye weledi wa michezo watakaochukuliwa na timu zilizopo ndani na nje ya nchi na kulipwa vizuri watakuwa na uwezo wa kuwekeza hapa nchini na kuweza kutoa ajira kwa vijana wengine ambao sio wanamichezo. Amesema kuwa wote ni mashahidi kuwa watu wanaoongoza kulipwa fedha nyingi ni wachezaji wenye uweledi.

Amesema kuwa mataifa ya Scandinavia yameweza kupunguza gharama za matibabu katika hospitali mbalimbali kwa wananchi wake kutokana na kuwekeza katika sekta ya michezo. Kutokana na hali hiyo ametaka jamii kushirikiana zaidi katika kukuza sekta ya michezo nchini. “Kwa kufanya hivyo tutaweza kuimarisha afya za wananchi wa mikoa yetu na taifa kwa ujumla na fedha nyingi tunazoelekeza katika sekta ya afya zitawekezwa katika miradi mingine ya maendeleo. Napenda nitoe wito kwa wananchi wa Kanda ya nyanda za juu kusini na taifa kwa ujumla tujenge tabia ya kuipenda michezo ili tuweze kuimarisha afya zetu” alisisitiza Mazenza.

Akiwasilisha taarifa ya UMISSETA Kanya, Mwenyekiti wa UMISSETA Kanda ya nyanda za juu kusini, Mwalimu Asheli Komba amesema kuwa mashindano hayo yanakabiliwa na changamoto za uhaba wa vifaa vya kichezo na viwanja vya michezo. Nyingine ni uhaba wa wataalam wa michezo na baadhi ya shule binafsi kutochangia michezo na kuona shule hizo si sehemu ya mashindano. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni ufinyu wa bajeti zinazotengwa serikalini kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za michezo.
Mwalimu Komba amependekeza halmashauri ziendelee kutenga fedha kadri fursa inavyopatikana ili kuendeleza wataalam wa michezo waliopo katika halmashauri hizo. Aidha, ameshauri kuwa mikoa na halmashauri ziendelee kuhamasisha wadau wa ndani na nje ya mikoa ili waweze kuchangia shughuli za michezo. 

Mashindani ya UMISSETA kitaifa yatafanyika mkoani Mwanza kuanzia tarehe 8-20 Juni, 2015 na Kanda ya nyanda za juu kusini itawakilishwa na wanamichezo mahili 136 wakati michezo itakayoshindaniwa ni mpira wa miguu, kikapu, wavu, riadha, netiboli, meza na bao. Michezo mingine ni tamthilia na ngoma. Kaulimbiu ya mashindano hayo mwaka huu ni michezo ni amani, upendo na mshikamano tujitokeze kuchagua viongozi bora.
=30=

RC IRINGA ATAKA HALMASHAURI ZIHAMASISHE MATUMIZI YA EFD



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza amezitaka Halmashauri kuhimiza matumizi ya mashine za kieletroniki za kodi (EFDs) kwa lengo la kuongeza mapato ya serikali.

Masenza amesema hayo alipokuwa akichangia katika taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mkoa wa Iringa kwa mwaka 2015/2016 iliyowasilishwa na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, Manispaa ya Iringa.

Masenza amesema “umefika wakati kwa kila halmashauri kuhimiza na kuhamasisha matumizi ya mashine za kieletroniki za kodi katika kuongeza mapato ya serikali. Mapato ya serikali yanakwamishwa na wafanyabiashara wasio na nia njema ya kulipa kodi halali ya serikali kwa kukwepa kutumia mashine hizi’’. Amesema halmashauri zina wajibu wa kuwahamasisha wafanyabiashara kutumia mashine hizo katika biashara zao.

Amesema kuwa atashangaa kusikia halmashauri inatetea wafanyabiashara kutotumia mashine hizo. Amesema kwa kuwa serikali inatumia kile kinachokusanywa kujiendesha ni jukumu la jamii nzima kuhimiza matumizi ya mashine hizo. 

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu amesema pamoja na kuwa jukumu la kukusanya kodi ni muhimu sana kwa mustakabali wa serikali, kulipa kodi kwa hiari ni kitendo cha kizalendo. Ameitaka jamii kujivunia kulipa kodi kwa hiari hasa wafanyabiashara. Amesema kuwa halmashauri nyingi zinashindwa kujiendesha kutokana na mianya iliyopo katika ukusanyaji wa mapato ya serikali. 

Akiongelea umuhimu wa matumizi ya mashine hizo, Ayubu amesema kuwa mashine hizo zinauwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi ya mali ya biashara bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano na kuondokana na usumbufu wa kuchapisha vitabu vya risiti kwa kipindi chote hicho.
=30=

MASENZA AVITAKA VYAMA VYA SIASA KUDUMISHA AMANI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Vyama vya siasa mkoani Iringa vimetakiwa kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifunga kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.

Masenza amesema “Iringa hatuhitaji vurugu kwa wananchi wetu. Vyama vya siasa waambieni wafuasi wenu kuwa Iringa hatuhitaji vurugu kwa namna yoyote katika kipindi chote kuelekea uchaguzi mkuu na katika uchaguzi mkuu wenyewe. Kamati ya Ulinzi na Usalama ipo makini muda wote na itashughulika na wote watakaojipanga kufanya vurugu”. Amewataka kuingia katika uchaguzi mkuu wakiwa wamoja na kudumisha mshikamano uliopo. 

Mkuu wa Mkoa amewataka kuendelea kushirikiana na kutengeneza timu itakayowezesha kufanikisha majukumu ya kiutekelezaji. Amepongeza juhudi na usimamizi wa Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika mchakato wa kuanzisha na kusimamia ugawanaji wa watumishi na mali baina ya Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga. “Napongeza kazi nzuri iliyofanywa na Katibu Tawala Mkoa kutokana na uzoefu wake. Yapo maeneo ambayo mgawanyo ulifanyika vibaya kwa kupeleka watu wasiokubalika eneo moja na kufanya utendaji wa kazi kuwa mgumu” alisema Masenza.

Awali akijibu hoja juu ya ushirikishwaji wananchi kwa lengo la kuondoa migongano baina ya wananchi na serikali katika uanzishwaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu amesema kuwa mgawanyo uliofanyika ni shirikishi na umezingatia hali na mahitaji ya kijiografia hasa maeneo ambayo wananchi walikuwa wanapata changamoto zaidi. Amesema kuwa ramani inaendelea kuandaliwa inayoonesha uhalisia wa maeneo yaliyogawanywa. Akijibu hoja ya changamoto ya mawasiliano, amesema kuwa lengo la mgawanyo huo ni kufanya huduma ya mawasiliano iwe bora kwa wananchi wote.
=30=

JIMBO JIPYA LA UCHAGUZI LA MJI WA MAFINGA KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kuanzishwa kwa Jimbo la uchaguzi la Mji wa Mafinga litatoa uwakilishi wa watu na kusaidia upatikanaji wa rasilimali na huduma kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Wilfred Myuyu alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya kugawa Majimbo ya Uchaguzi wilaya ya Mufindi katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo katika Manispaa ya Iringa.

Myuyu amesema kuwa mapendekezo ya kugawa Majimbo ya Uchaguzi wilaya ya Mufindi yatatoa nafasi kubwa ya uwakilishi wa watu katika maeneo. Amesema kuwa mapendekezo hayo yatasaidia upatikanaji wa rasilimali na kurahisisha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Amesema kufuatia kugawanywa kwa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na kuzaliwa kwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, pendekezo la kuongeza Jimbo moja la Uchaguzi ambali ni Jimbo la Mji wa Mafinga. Amesema kuwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga ambayo itakuwa na Jimbo la Mji wa Mafinga ina kilometa za mraba 953. Halmashauri ya wilaya ya Mufindi itabaki na Majimbo ya Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini ikiwa na kimometa za mraba 6,170. 

Akiongelea mipaka ya kiutawala, Myuyu amesema “Jimbo la Mji wa Mafinga litakuwa na Kata tisa, Jimbo la Mufindi Kaskazini Kata 11 na Mufindi Kusini Kata 14. Eneo kubwa la Jimbo la Mji wa Mafinga ni tambarare wakati Majimbo ya Mufindi Kaskazini na Kusini yana maeneo ya milima, tambarare na sehemu za mabonde. kwa mujibu wa makisio ya ongezeko la watu hadi Oktoba, 2015 kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ni watu 77,364 kwa Mji wa Mafinga, 159,991 kwa Mufindi Kusini na 105,757 kwa Jimbo la Mufindi Kaskazini”.

Myuyu amesema “kama maombi yetu yatakubalika itaepusha mwakilishi mmoja kutumikia Halmashauri mbili tofauti kwa sababu Halmashauri mpya ya Mji wa Mafinga imetokana na Majimbo yote mawili ya Mufindi Kaskazini na Kusini. Kwa sabau hiyo Majimbo mawili ya Mufindi Kaskazini na Kusini yatabaki Halmashauri ya wilaya ya Mufindi wakati Jimbo la Mji wa Mafinga litakuwa Halmahauri ya Mji wa Mafinga”.

Kamati ya ushari ya mkoa wa Iringa imeridhia kwa kauli moja uanzishwaji wa Jimbo la uchaguzi la Mji wa Mafinga.
=30=

RCC IRINGA YABARIKI JIMBO LA UCHAGUZI KILOLO KUGAWANYWA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa imeridhia kwa kauli moja mapendekezo ya kugawa Jimbo la uchaguzi la Kilolo lililopo katika wilaya ya Kilolo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa kimepitisha kwa kauli moja mapendekelezo ya kugawa Jimbo la uchaguzi la Kilolo na kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Ilula.

Akiwasilisha mapendekezo ya kugawa Jimbo la uchaguzi la Kilolo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga amesema “wilaya ya Kilolo ipo katika mchakato wa kuanzisha Halmashauri mpya ya wilaya ya Ilula, kwa sababu hiyo tunawasilisha mapendekezo ya kuligawa Jimbo la uchaguzi la Kilolo kuwa Majimbo mawili ya uchaguzi yaani Jimbo la uchaguzi la Kilolo na Jimbo la uchaguzi la Ilula”. 

Amesema kuwa mapendekezo haya yamepitishwa na vikao vya kisheria katika ngazi ya Halmashauri na wilaya na kuvitaja vikao vya Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala, Baraza la Madiwani na Kamati ya Ushauri ya Wilaya. Amesema kuwa vikao vyote vimeridhia uanzishwaji wa Jimbo la uchaguzi la Ilula ili kuwezesha kila Halmashauri kuwa na Jimbo lake la uchaguzi na kuepuka Jimbo moja kuwa ndani ya Halmashauri mbili. Sababu nyingine ameitaja kuwa ni kusaidia upatikanaji wa rasilimali na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akiongelea hali ya Majimbo yanayopendekezwa kugawanywa, Millinga amesema kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu makadirio ya idadi ya watu katika wilaya ya Kilolo ifikapo Oktoba, 2015 ni watu 235,556. Amesema Majimbo yanayopendekezwa yanakadiriwa kuwa na idadi ya watu kama ifuatavyo; Jimbo la Kilolo watu 115,164 na Ilula watu 120,392. Aidha, ukubwa wa Jimbo la kilolo ni Km za mraba 2,642.5 na Jimbo la Ilula ni Km za mraba 5,232.1. 

Mipaka ya kiutawala, Millinga amesema kuwa Jimbo la Kilolo litakuwa na Kata 12 wakati Ilula Kata 14. 

Afisa Habari ya Wilaya ya Kilolo, Filemon Namwinga amesema kuwa mapendekezo ya kugawa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo na Jimbo la uchaguzi la Kilolo yanafanyika katika muda muafaka. Amepongeza vyombo vya maamuzi kufikia hatua hiyo na kusema huo ni uamuzi wa kimkakati unaolenga kuwafikishia wananchi huduma bora. Amesema kuwa sababu za kijiografia na ukubwa wa maeneo ni changamoto kuwa katika kufikisha huduma stahiki kwa wananchi. “Kwa mfano changamoto ya kijiografia kama ukanda wa juu wenye msimu mrefu wa masika na msimu mfupi sana wa kiangazi tofauti na ukanda wa chini wenye msimu mrefu wa kiangazi na masika muda mfupi sana.
=30=