Wednesday, October 4, 2017

MATUKIO KATIKA PICHA KILELE CHA SIKU YA UTALII DUNIANI,MAONESHO YA UTALII KARIBU KUSINI NA MAONESHO YA SHUGHULI ZA WAJASIRIAMALI WA VIWANDA































ELIMU YA UJASIRIAMALI KWA WAJASIRIAMALI YATOLEWA



Na Dennis Gondwe, IRINGA
Maadhimisho ya siku ya utalii ya utalii duniani, maonesho ya karibu kusini na maonesho ya wajasiriamali wa viwanda vidogo mikoa ya nyanda za juu kusini yamefanikiwa kutoa elimu ya ujasiriamali na utalii.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika salamu zake wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za wajasiriamali wa wa viwanda vidogo wa mikoa ya nyanda za juu kusini yaliyofanyika mkoani Iringa jana.
Mhe Amina Masenza

Masenza alisema kuwa maonesho hayo yamekuwa ya manufaa kwa jamii. “Maonesho haya yametoa elimu ya masuala ya utalii na ujasiriamali, ajira kwa watoa huduma mbalimbali wakati wa maonesho na washiriki wameweza kubadilishana uzoefu na kupata masoko ya bidhaa” alisema Masenza. 

Mafanikio mengine, mkuu wa mkoa wa Iringa aliyataja kuwa ni kuongezeka kwa wadau wanaotaka kuwekeza katika mikoa ya nyanda za juu kusini.

Masenza alisemaa kuwa maonesho ya karibu kusini mwaka 2017 yalijumuisha maeneo sita ikilinganishwa na maeneo matatu ya mwaka 2016. Aliyataja maeneo hayo kuwa ni ziara za kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na baadhi ya vivutio, maonesho ya wanyama hai, maonesho ya ngoma za asili, kongamano la utalii endelevu na uendeshaji viwanda kwa mikoa ya nyanda za juu kusini na maonesho kwenye mabanda kwa kuonesha bidhaa za wajasiriamali wa viwanda vidogo na watoa huduma za utalii. 

Maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za wajasiriamali wa SIDO yamehusisha mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Songwe, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam, Geita, Lindi, Morogoro, Kilimanjaro, Tabora na nchi ya Kenya. Maonesho hayo yamehusisha mashine mbalimbali, bidhaa za usindikaji, bidhaa zilizosindikwa, bidhaa za ngozi, kazi za mikono na dawa.
=30=

HALMASHAURI ZATAKIWA KUSHIRIKI MAONESHO YA UTALII KARIBU KUSINI



Na Dennis Gondwe, IRINGA
Halmashauri za mikoa ya nyanda za juu kusini zatakiwa kushiriki kikamilifu maonesho ya utalii karibu kusini ili kutangaza fursa za utalii na viwanda vidogo vilivyopo maeneo yao.

Kauli hiyi ilitolewa na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa afrika mashariki, kikanda na kimataifa Dr. Augustino Mahiga alipokuwa akifunga maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya wajasiriamali wa viwanda vidogo nyanda za juu kusini yaliyofanyika mjini Iringa.
Balozi Dr Augustino Mahiga

Dr. Mahiga alisema “natoa wito kwa halmashauri zote na wadau katika mikoa ya nyanda za juu kusini kuanza kujiandaa kikamilifu kushiriki katika maonesho haya ili kutumia nafasi hii kujitangaza na kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na viwanda”. 

Waziri huyo aliwataka SIDO kufanya kazi kwa kujituma ili wajasiriamali waliojitokeza wabadilike na kuwa wafanyabiashara wakubwa. Aliongeza kuwaa wjasiriamali watakapobadilika na kuwa wafanya biashara wakubwa waendelee kuwasaidia wajasiriamali wengine ili wakue.

Dr. Mahiga alielezea matumaini yake kuwa maonesho ya mwaka 2018 yatakuwa yenye ufanisi mkubwa kwa kushirikisha wadau wengi kutoka sehemu mbalimbali za nchi na nchi jirani. 

Tuzingatie tu kuwa utalii hauna mipaka na ni vema sasa tuanze kujitangaza pia kwa nchi jirani za Zambia, Malawi, Msumbiji, na hata Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo pamoja na kutumia balozi zetu za nje” alisema Dr. Mahiga.

Maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za wajasiriamali wa SIDO yamehusisha mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Songwe, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam, Geita, Lindi, Morogoro, Kilimanjaro, Tabora na nchi ya Kenya. Maonesho hayo yamehusisha mashine mbalimbali, bidhaa za usindikaji, bidhaa zilizosindikwa, bidhaa za ngozi, kazi za mikono na dawa.
=30=

WAJASIRIAMALI WANAKABILIWA NA TATIZO LA KUJITANGAZA



Na Dennis Gondwe, IRINGA
Wajasiriamali wengi wanakabiliwa na tatizo la kujitangaza jambo linalosababisha washindwe kufikia masoko ya bidhaa kwa urahisi.

Kauli hiyo ilitolewa na meneja wa SIDO Mkoa wa Ruvuma, Martin Chang’a alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliotembelea banda la SIDO katika maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) kwa mikoa ya nyanda za juu kusini yaliyofanyika mkoani Iringa hivi karibuni.

Chang’a alisema kuwa wajasiriamali wengi wanajuhudi ya kuzalisha bidhaa nzuri kutokana na mafunzo wanayoyapata kutoka SIDO, changamoto ni jinsi ya kufikia masoko. Alisema kuwa tatizo kubwa linalowakabili wajasiriamali ni mbinu za kujitangaza na kutangaza bidhaa zao. 

Mbinu za kujitangaza ni muhimu sana kwa wajasiriamali kwa sababu zinawasaidia katika kufikia masoko kirahisi. Kwa kuona tatizo hilo, SIDO tumetoa mafunzo ya jinsi ya kuboresha mbinu za kujitangaza kwa wajasiriamali wanaoshiriki maonesho haya ili kuwasaidia kuwa na uwezo wa kujitangaza” alisema Chang’a.

Akiongelea lengo la maonesho hayo kwa upande wa SIDO, Meneja wa SIDO mkoa wa Ruvuma alisema kuwa maonesho hayo yanalenga kuwatangaza wajasiriamali na shughuli wanazofanya ili zijulikane kwa watu. Aliongeza kuwa, maonesho hayo yanawawezesha wajasiriamali kukutana na kubadilishana uzoefu katika shughuli zao.

Maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za wajasiriamali wa SIDO yamehusisha mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Songwe, Mwanza, Pwani, Dsm, Geita, Lindi, Morogoro, Kilimanjaro, Tabora na nchi ya Kenya. Maonesho hayo yamehusisha mashine mbalimbali, bidhaa za usindikaji, bidhaa zilizosindikwa, bidhaa za ngozi, kazi za mikono na dawa.
=30=

Sunday, October 1, 2017

MAONESHO YA UTALII KARIBU KUSINI NA SIDO KUTANGAZA FURSA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Maonesho ya utalii karibu kusini na wajasiriamali wa SIDO yatumike kutangaza shughuli, fursa na vivutio vilivyopo mikoa ya nyanda za juu kusini.

Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa kufungua maadhimisho ya siku ya utalii Duniani, maonesho ya Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) mjini Iringa jana.
Prof. Jumanne Maghembe

Prof. Maghembe alisema “kipekee nimefurahishwa na maonesho ya karibu kusini mwaka 2017 ambayo kwa mwaka huu yamejumuisha wajasiriamali wa SIDO ambao ni wazalishajai wa bidhaa mbalimbali zinazoweza pia kutumiwa na watalii na kutoa huduma za kitalii nchini. Karibu kusini ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa ya nyanda za juu kusini na kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea vivutio hivyo”. 

Aliongeza kuwa nchi ya Tanzania ina maeneo mengi yenye fursa za uwekezaji ambazo hazijaendelezwa ipasavyo.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni ukanda wa nyanda za juu kusini wenye vitutio vingi na vizuri vya utalii wakiwemo wanyama pori. Vivutio vingine alivitaja kuwa ni hifadhi za misitu asili, mandhari nzuri za kuvutia, bonde la usangu na mto ruaha, ziwa nyasa na kimondo. 

Vivutio hivi hutoa fursa na kuendeleza utalii katika ukanda huu. Aidha, ni wakati muafaka wa kuzitangaza fursa hizi ili kuvutia wawekezaji waje kuwekeza katika ukanda huu” alisema Prof. Maghembe.

Nae mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alisema kuwa mkoa wake daima utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ya mfano na kukua kwa kasi.
 =30=