Saturday, December 1, 2012

UMASIKINI CHANZO CHA UKIMWI IRINGA




Hali ya umasikini na mila potofu zimeendelea kuchangia katika maambukizi ya VVU na UKIMWI katika Mkoa wa Iringa na kusababisha madhara makubwa kuanzia ngazi ya familia.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akipata maelezo ya shughuli zinazofanywa na AMREF katika banda lao katika uwanja wa RUCO.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma alipotembelea banda la Ushauri nasaha na kupima VVU.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani katika Mkoa wa Iringa yalifanyika katika Chuo Kikuu kishiriki cha Ruaha.

Dkt. Christine amesema “hali ya maambukizi inatisha, madhara ya maambukizi ya VVU na UKIMWI ni makubwa hasa kutokana na sababu za umasikini, mila na desturi. Madhara haya ambayo huanzia katika ngazi ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vifo vya watu ambao ni nguvu kazi ya Taifa la Tanzania”.

Amesema kuwa vifo vya wazazi husababisha kuongezeka kwa watoto yatima ambao wanahitaji msaada wa elimu, malazi, chakula na matibabu.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wake kwa kushirikiana na Halmashauri na mashirika yasiyo ya kiserikali wanatekeleza shughuli mbalimbali katika kukabiliana na kasi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Ameyataja maeneo maeneo ya ushirikiano kuwa ni katika kinga, huduma za kuzuia maambukizi mapya kwa watu ambao hawana maambukizi pamoja na wale wenye maambukizi kutokupata maambukizi mengine. Eneo lingine amelitaja kuwa ni tiba na huduma kwa walioathirika na janga la UKIMWI.

Dkt. Christine amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2011 hadi Juni 2012 jumla ya watu 130,882 walipata ushauri nasaha na kupima afya zao na kati yao 15,361 walikuwa na maambukizi ya VVU sawa na asilimia 10.5%.

Akiongelea utoaji wa huduma za upimaji wa VVU baada ya kushauriwa na mtoa huduma kwa mteja yoyote aendae hospitali akiwa anaumwa magonjwa mengine au kusindikiza, imesaidia sana kuwafanya watu wengi kujua hali ya afya zao kuhusiana na maambukizi ya VVU. Amesema katika jumla ya watu 23,184 waliopata huduma ya upimaji wa VVU baada ya kushauriwa na mtoa huduma,jumla ya watu 1,772 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU.

Aidha, huduma ya tohara kwa wanaume ni miongoni mwa njia zinazotumika katika kupunguza maambukizi ya VVU kwa wanaume.
Amesema kuwa huduma za tohara zimekuwa zikitolewa katika vituo vya huduma kama huduma ya kawaida. Mkuu wa Mkoa amesema “katika zoezi hilo jumla ya wanaume 113,076 wamekwisha tahiriwa katika mikoa ya Iringa na Njombe. Ili tohara kwa wanaume ilete mafanikio katika kupunguza maambukizi ya V.V.U., Mkoa unatarajia kutahiri jumla ya wanaume 264,990 ifikapo mwaka 2015”.

Wakati huohuo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni tano kwa vituo vinne vya watoto yatima leo. Akitoa maelezo ya msaada huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Theresia Mahongo amesema kuwa Manispaa ya Iringa inao utaratibu wa kutoa misaada mbalimbali kwa watoto yatima kulingana na majira na mahitaji. Miongoni mwa vitu vilivyotolewa kwa ajili ya watoto yatima ni pamoja na mchele, mafuta ya kupikia, maharage, unga, unga wa ngano, sabuni za kufulia na kuoga.
=30=

Friday, November 30, 2012

WAHASIBU WATAKIWA KUBADILIKA


Wahasibu nchini wametakiwa kubadilika na kuendana na mabadiliko ya kimfumo hasa imapoanzishwa kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa kazi na kupunguza upotevu wa fedha za Serikali.

Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa alipokuwa akiongea na maafisa wa Serikali Mkoani Iringa muda mfupi kabla ya kuhudhuria Mahafari ya Chuo kikuu cha Ruaha Iringa (RUCO).

Akifafanua kuhusu changamoto za mfumo wa Epicor 9.05 katika utekelezaji wa kazi za kihasibu na malipo, Dkt. Mgimwa ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kalenga amesema kuwa lengo la Serikali kuanzisha mfumo huo ni kuhakikisha ufanisi katika matumizi ya fedha za serikali na kuondoa mianya ya upotevu wa fedha hizo. Amesema “tumekuwa na kipindi kifupi sana cha kuwawezesha wahasibu wetu juu ya kuutumia mfumo wa Epicor 9.05”. Akiufafanua mfumo huo, amesema kuwa mfumo huo ulianzia Marekani mwaka 1996 na kuanzishwa nchini kutokana na uwezoz wake wa kuchukua maagizo ya kimalipo kwa wingi, ukubwa, wepesi na haraka na sifa yake nyingine ni kukidhi viwango vya kihasibu vya kimataifa. Amesema kuwa mfumo huo pia unauwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa nyingi kwa wakati. 

Amesema kuwa ili kuweza kuenda vizuri na mfumo huo ni lazima wahasibu wakubali kubadilika na kuwa wepesi zaidi kuyakubali mabadiliko hayo.

Akiongelea uidhinishwaji wa fedha za miradi ya maendeleo ambao umekuwa ukilaumiwa sana kuwa umekuwa ukichelewa sana, Waziri wa Fedha amesema kuwa mchanganuo wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ni muhimu sana na ndio unaozingatiwa kabla ya kuidhinishwa malipo wengine ya miradi ya maendeleo. Amesema kuwa thamani ya fedha ni jambo linalopewa uzito katika miradi yote ya maendeleo ili fedha ya serikali inayotolewa iendane na mradi uliokusudiwa. Amesema kuwa changamoto iliyopo katika kodi ya Serikali ikihusishwa na miradi ya maendeleo, amesema “tunaruhusiwa kutoa asilimia tano tu iliyopatikana na kupeleka katika miradi ya maendeleo na asilimia nyingine inabaki kwa ajili ya kulipa mishahara na shughuli nyingine za uendeshaji wa Serikali” amesisitiza Dkt. Mgimwa.  

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe ameelezea changamoto inayoukabili Mkoa wa Iringa kuwa ni ukomo wa bajeti hasa katika miradi ya maendeleo. Amesema kuwa katika miradi ya maendeleo fedha hizo zimepungua kutoka shilingi bilioni 1 hadi milioni 274. Ametolea mfano miradi inayoendelea kuwa ndiyo inayoathirika zaidi, kama ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa mwaka 2012/2013 imetengewa shilingi milioni 51 tu kati ya milioni 700 zinazohitajika.

Aidha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ameiomba Hazina kuwa inatoa kipaumbele kwa miradi ya maendeleo inayoendelea. Akiongelea fedha za matumizi ya kawaida amesema kuwa kupungua kwa fedha hizo kumekuwa kukisababisha kutokueleweka katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Amesema mfano mwaka 2011/ 2012 fedha za matumizi mengine Mkoa ulipangiwa shilingi bilioni 2.7 ingawa hazikutolewa zote. Aidha, mwaka 2012/2013 Mkoa umepangiwa shilingi bilioni 1.9.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amempongeza Waziri wa Fedha kwa kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo na kuomba ushirikiano wa viongozi na wadau wote katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
=30=

Wednesday, November 28, 2012

CHANJO YA MPYA KUZINDULIWA JAN, 2013




Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma ametoa wito kwa wananchi kuondokana na hofu pale chanjo ya mpya za magonjwa ya kuhara na nimonia zitakapoanzishwa mkoani Iringa.

Rai hiyo ameitoa alipokuwa akifungua kikao cha kamati ya huduma ya afya ya msingi Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.


Dkt. Christine amesema kuwa mara nyingi chanjo mpya zinapoanzishwa wananchi wanakuwa na hofu na minong’ono mbalimbali. Amesema “napenda kuwahakikishia wananchi kuwa chanjo hizi ni salama na zimefanyiwa utafiti wa kina, hivyo ni salama kwa matumizi ya binabamu”. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kupatiwa chanjo hizo ili kuweza kupunguza na hatimae kuondoa kabisa vifo vya watoto wadogo.

Akiwasilisha mada juu ya kuanzishwa kwa chanjo mpya za “Rotavirus na Pneumococcal” Mratibu wa huduma za chanjo Mkoa wa Iringa, Naftal Mwalongo amesema kuwa chanjo ni moja kati ya afua madhubuti na nafuu za kuzuia magonjwa na vifo. Amesema chanjo inazuia magonjwa, ulemavu na inaokoa mamilioni ya watoto kila mwaka.

Akiongelea nafasi ya chanjo katika utekelezaji wa malengo ya milenia, Mwalongo amesema “chanjo ni afua muhimu kufikia lengo namba nne la milenia la kupunguza vifo vya watoto  chini ya mwaka mmoja ifikapo 2015”.

Mwalongo amesema kuwa hali ya ugonjwa wa kuharisha kwa Mkoa wa Iringa mwaka 2010-2011, idadi ya wagonjwa wa kuharisha chini ya miaka mitano kwa mwaka 2010 ilikuwa ni 35,424 sawa na asilimia 12 kati ya wagonjwa waliopata matibabu ya nje na mwaka 2011 idadi ya wagonjwa wa kiharisha chini ya miaka mitano ilikuwa 34,941 sawa na asilimia 11 kwa wagonjwa waliopata matibabu ya nje.

Amesema kuwa chanzo cha ugonjwa wa kuharisha ni kula au kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi chenye virusi. Aidha, amesema kuwa muda wa uambukizo hadi dalili kujitokeza ni kati ya saa 24 hadi 48. Amesema kundi linaloathirika zaidi ni watoto chini ya umri wa miaka miwili.

Mratibu wa huduma za chanjo Mkoa wa Iringa, amezitaja dalili za ugonjwa wa kuhara kuwa ni kuharisha, kutapika, kupungukiwa maji na chumvi mwilini na mara chache huambatana na homa.

Amesema kinga yake ni pamoja na kunyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee na kuimarisha usafi wa mazingira. Kinga nyingine ameitaja kuwa ni kuimarisha usafi wa mtu binafsi kwa kunawa mikono kwa sabuni na nyongeza ya virutubishovya Zinc huchangia katika kupunguza kuenea kwa Rotavirus, pamoja na kupatiwa chanjo ya Rotavirus.

Kikao hicho kilichojumuisha maafisa waandamizi, viongozi wa dini, waandishi wa habari na watu maarufu, wataalamu toka sekta ya afya kilikuwa na lengo la kutoa uelewa wa pamoja kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi juu ya chanjo hizo zitakazoanza mapema mwezi Januari, 2013.
=30=

Monday, November 26, 2012

UKATILI WA KIJINSIA...WANAUME WAWAJIBIKE



Unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa nchini kutokana na baadhi ya dhana na mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka na kuwanyima wanawake haki zao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake wakati wa uzinguzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia maadhimisho yaliyofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa Manispaa ya Iringa.

Dkt. Christine amesema “unyanyasaji wa kijinsia unaweza kutokea kwa jinsi yeyote ile, mwanamke, mwanaume au watoto. Ila huwapata sana kina mama na vijana hasa watoto wa kike. Unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa ulimwenguni kote, nchini Tanzania, kadhalika katika mikoa yetu ya Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi”. Amesema kuwa baadhi ya dhana kama umasikini, mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka na kuwanyima wanawake haki zao ni moja klati ya viini vinavyopelekea unyanyasaji wa kijinsia nchini. Amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Tanzania Demographic Health Survey mwaka 2010, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inakuwango cha wastani wa vitendo unyanyasaji wa kijinsia. Amesema “Iringa 54%, Ruvuma 55%, Mbeya 55%, Mtwara 26%, Lindi 22% na Rukwa 56%” amesema kuwa kwa mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa wastani wa kiwango ni mkubwa ukilinganisha na na kiwango cha wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 44.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa katika kupambana na hali hiyo, Serikali kupitia Mpango wa kupambana na Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA), mabadiliko ya Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, imefanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo la ukatili wa kijinsia. Aidha, amesema kuwa Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau utaendelea kuwajengea uwezo watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali ili waweze kutatua na kuzifanyia kazi kesi zinazohusi ukatili wa kijinsia.

Miongoni mwa jitihada hizo, Mkuu wa Mkoa amezitaja kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi na kusisitiza kuwa wananchi wahamasishwe kwenda kutoa taarifa, kuhakikishiwa usalama wao na kuamini kuwa madawati yale yako kwa ajili yao. Amesema katika kuliwekea mkazo tatizo hilo, Mkoa umeziagiza Halmashauri kuendelea kutenga bajeti katika mipango yao kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, haki za binadamu, sheria na madhara yatokanayo na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Dkt. Christine amesema “yatupasa tukumbuke kuwa ukatili wa kijinsia sio suala la wanawake ama watoto pekee. Ni muhimu sana kwa wakati huu; hasa kwa kina baba kuwa chachu ya mabadiliko kwa kupinga vitendo vya ukatili na hata kukemea tabia hizo”. Amesema ni vema viongozi na jamii ikatumia ushawishi wake kuamsha majadiliano juu ya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia, kuvipinga kwa nguvu zote na kuwa mfano bora wa kuigwa ili kuimarisha ustawi wa nchi ya Tanzania.
=30=

MUFINDI WAJIDHATITI KUFIKISHA PEMBEJEO VIJIJINI




Wilaya ya Mufindi imehakikisha usambazaji wa pembejeo unafanikiwa kwa kuhakikisha mbadala wa mawakala waliopungukiwa na uwezo wa kusambaza pembejeo za kukuzia baada ya kutoa taarifa kwa uongozi wa wilaya na wakala mwingine kuendeleza usambazaji huo haraka ili kutokuwachelewesha wakulima.

Hayo yamesemwa na Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Wilaya ya Mufindi, Edna Kaduma wakati akiwasilisha taarifa ya usambazaji wa pembejeo kwa wilaya ya Mufindi mwaka 2011/2012 na 2012/2013 katika kikao cha kamati ya vocha ya mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Edna amesema kuwa miongoni mwa changamoto ilikuwa ni mawakala kupungukiwa uwezo wa kusambaza pembejeo hasa wakati ilipoanza kutumika mbolea ya kukuzia. Amesema kuwa mawakala hao walitoa taarifa kwa uongozi wa Wilaya na haraka walipatikana mawakala wengine kwa lengo la kuendeleza huduma hiyo pasipo kuwachelewesha wakulima kutumia mbolea hiyo ya kukuzia. Amesema katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, kamati ya vocha Wilaya ya Mufindi ilifanya mikutano mitatu na mawakala wote kwa lengo la kutathmini uwezo wa kila mmoja na kukubaliana maeneo ya kuhudumia kulingana na uwezo wa kila wakala aidha, wale wenye uwezo mkubwa walikubali kutoa huduma kwa maeneo yaliyokosa mawakala.   

Amesema ili kuweka uwazi katika mchakato huo, kamati ya vocha ya wilaya ilifanya mikutano ya hadhara na wananchi kwa kila kata na pamoja na kukutana na kamati za vocha za vijiji kwa ajili ya kutoa maelekezo ya utaratibu wa mpito wa usambazaji wa pembejeo kwa kutumia vocha. Amesema miongoni mwa changamoto ni kupanda kwa bei za pembejeo baadhi ya wakulima wameshindwa kutumia pembejeo bora. Amesema miongoni mwa changamoto pia ni kupungua kwa wanufaika kutokana na kupungua kwa idadi ya vocha na kuchelewa kuwa vocha za ruzuku kusababisha baadhi ya vijiji kutotumia vocha za mbegu bora.

Edna amesema kuwa ili kuhakikisha usambazaji unafika katika maeneo yote suala la mawasiliano lilipewa uzito unaostahili. Amesema mawasiliano na ufuatiliaji wa mara kwa mara ulifanyika kati ya wilaya na vijiji ili kuhakikisha maeneo yote usambazaji unakwenda vizuri na pembejeo zinauzwa kwa bei iliyokubalika katika vikao.

Akiongelea maadalizi ya pembejeo kwa msimu wa mwaka 2012/2013, Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wilaya ya Mufindi amesema kuwa mahitaji ya mbolea kwa wilaya ya Mufindi, jumla ya tani 13,720 na mahitaji ya mbegu ni jumla ya tani 887. Amesema “msimu huu wilaya imepokea mgao wa vocha seti 22,188 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 50 ikilinganishwa na mgao wa msimu uliopita.
=30= 

Wednesday, November 21, 2012

KAMPUNI ZAIDI YA 10 KUSAMBAZA MBOLEA IRINGA




Kampuni za mbolea zaidi ya 10 zimejitokeza kuhudumia wakulima katika Wilaya ya Iringa kwa ajili ya kusambaza vocha za pembejeo za kilimo kwa mwaka 2012/2013 na 2013/2014.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa utoaji wa pembejeo zenye ruzuku kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2011/2012 na maandalizi ya kilimo msimu wa mwaka 2012/2013 katika kikao cha kamati ya pembejeo cha mkoa wa Iringa, Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea utaratibu mpya kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wa usambazaji wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali kwa wakulima wa mahindi na mpunga kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013.

Amesema kuwa utaratibu wa kutumia vocha utaendelea ila mawakala watakaosambaza pembejeo hizo kwa wakulima wanufaika na kampuni ya pembejeo ndiyo itasambaza pembejeo hizo badala ya kamati ya pembejeo ya wilaya kama ilivyokuwa awali.
Amesema lengo la kampuni za pembejeo kupewa jukumu la kuteua mawakala ni kuhakikisha pembejeo zenye ubora zinawafikia wakulima kwa wakati muafaka. Amesema kuwa kazi ya kamati ya pembejeo ya wilaya itakuwa ni kusimamia na kufuatilia utaratibu mzima wa pembejeo katika mchakato wote.

Lucy amesema jumla ya kampuni 13 za mbolea na mbegu zimejitokeza kuhudumia wakulima wa Wilaya ya Iringa. Amesema makampuni hayo yameteua mawakala wawakilishi saba na mawakala wasaidizi 46. Akiongelea uhamasishaji wa matumizi ya mbolea ya minjingu mazao pamoja na utaratibu wa usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 na 2013/2014 umefanyika katika vijiji vya Nyabula, Lupembelwasenga, Usengelindeti, Makombe, Kihanga, Ng’enza, Magulilwa na Tagamenda. Uhamasishaji huo unaendelea sambamba na usambazaji wa vocha za pembejeo.

Wakati huohuo, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea mgao wa pembejeo zenye ruzuku kwa mwaka 2012/2013 zenye thamani ya shilingi 1,828,654,000. Akielezea aina ya pembejeo hizo, Afisa Kilimo, mifugo na ushirika amesema kuwa mbolea ya kupandia vocha (22,000), mbolea ya kukuzia (22,000), mbegu ya mahindi (chotara) (5,409),mbegu ya mahindi mchanganyiko (9,309), mbegu ya mpunga (7,282).

Lucy ameyataja mafanikio yaliyotokana na mfumo wa vocha kuwa ni upatikanaji wa pembejeo katika ngazi ya kijiji umefikiwa ambapo wakulima wanaweza kununua pembejeo katika maeneo ya vijiji vyao. Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni ongezeko la uzalishaji kutoka gumia 3-5 za mahindi hadi kufikia wastani wa gunia 12-22 kwa ekari, kwa zao la mpunga ongezeko kutoka gunia 8-10 hadi kufikia wastani wa gunia 16-25.  Aidha, idadi ya wakulima wanaolima kitaalamu imeongezeka na matumizi ya pembejeo kwa wakulima yameongezeka.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amekiaarifu kikao hicho kuwa msimu wa kilimo umefika na kuwa mvua zimeanza kunyesha katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mufindi na wakulima wameanza kupanda. Aidha, aliwataka wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima katika kuwafundisha na kuwaelekeza mbinu bora za kilimo. 

=30= 

JAPAN KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA AFYA



Serikali ya Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali hasa sekta ya afya na kilimo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akimkabidhi kitabu cha profile ya Mkoa wa Iringa Balozi wa Japan nchini Tanzania

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika ziara iliyolenga kusaini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Balozi Okada amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha uchumi unakuwa kwa kasi zaidi kwa kukuza biashara baina ya nchi mbili hizo. Amesema kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo, ni lazima kipato chao kiongezeke ili waweze kunufaika na kilimo hicho kama shughuli yao kuu ya kiuchumi. Amesema kuwa Serikali yake inao mpango wa kuisaidia sekta ya kilimo nchili ili kuhakikisha kilimo cha mpunga kinaongezeka mara dufu kwa kuwa nchi ya Japan inasifika kwa uzalishaji wa mpunga duniani.

Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuahidi kuziunga mkono juhudi hizo kwa karibu.

Awali katika salamu za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesifu juhudi za Serikali ya Japan katika kusaidia maendeleo kwa mkoa wa Iringa na kusema ni juhudi za kupongezwa sana. Amesema kupitia misaada ya Japan, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweza kupata ufadhili katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, kilimo, maji na umwagiliaji.

Akiongelea maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kwa kujibu wa utafiti wa mwaka 2008, mkoa wa Iringa ulikuwa na takribani asilimia 16 ya maambukizi, kiwango ambacho ni karibu mara tatu ya kiwango cha maambukizi kitaifa. Amesema kuwa hali hiyo haikubaliki na zinaihitajika juhudi za pamoja kati ya Tanzania na Japan katika kuendeleza mapambano hayo. Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Japan za kuisaidia Tanzania katika sekta ya afya na ustawi wa jamii kupitia miradi mbalimbali kwa lengo la kuboresha afya ya mama na familia katika  mkoa wa Iringa.

Balozi wa Japan nchini Tanzania yupo mkoani Iringa kwa ajili ya utiaji saini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga unaogharimu dola za kimarekani 123,339 kwa lengo la kuongeza ubora wa huduma za afya na kupunguza vifo vya wanawake na watoto mkoani Iringa.
=30=


Monday, November 19, 2012



TAMKO LA ASKOFU METHODIUS KILAINI

Askofu Methodius Kilaini

Kwa masikitiko makubwa nimesoma katika gazeti la Mwananchi kwamba nimeiponda safu ya uongozi na sekretariati ya CCM. Mimi sijaongea na gazeti lolote juu ya uongozi wa CCM na wala sina nia au sababu ya kuuponda uongozi huo. 

 Ni vibaya kwa gazeti lo lote lile kutumia jina la mtu kwa kueneza maoni yake. Kama ni waugwana natumaini watasahihisha waliyoyaandika. Nasikitika sana kwa kunikwazwa na hilo. 
 

Askofu Method Kilaini
Bukoba Catholic Diocese