Sunday, January 26, 2014

SERIKALI KUWASAIDIA WACHIMBAJI HARAMU KUPATA AJIRA



Magdalena Nkulu, Shinyanga
Serikali mkoani Shinyanga imelaani na kukemea tabia ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya migodi kwa lengo la kuiba mchanga wa madini kwa kuwa ni kinyume cha sheria na hatari kwa maisha ya wananchi hao.
 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally N. Rufunga akishuhudia shimo hilo alipotembelea kuona shughuli za wachimbaji haramu katika mgodi wa Mwadui wilaya ya Kishapu jana, kushoto kwake ni Afisa Tarafa ya Mondo Bi.Maria Makoye na aliyesimama mbele ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu Wilson Nkhambaku.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally Nasoro Rufunga ametoa tamko hilo alipotembelea Mgodi wa Almasi Mwadui katika wilaya ya Kishapu jana na kujionea hali ya uchimbaji haramu unavyofanyika katika mgodi huo na pia kuzungumza na wachimbaji hao wanaojulikana kwa jina la Wabeshi, ambapo amewaahidi serikali itawasaidia kutafuta shughuli mbadala na kuwataka waachane na shughuli hiyo mara moja.

Mhe. Rufunga amewaambia wabeshi hao kuwa, serikali itahahakisha wanapata ajira halali kupitia viwanda vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa mkoani hapa, kuwakopesha mitaji kwa mfuko wa maendeleo ya vijana wa asilimia 5, pamoja na kufanya taratibu za kuwapatia maeneo madogo ili wachimbe kihalali iwapo wataacha na biashara hiyo.

Amewaambia kuwa, uchimbaji huo ni kuwaibia wawekezaji na kuwakwamisha kulipa mapato kwa serikali, kwani nchi inapata kodi kutoka kwa wawekezaji waliopata leseni halali ya uchimbaji, kodi ambayo inawanufaisha wananchi wenyewe katika shughuli za maendeleo.

Amewaasa kuacha kutumiwa na watu wenye uwezo kuhatarisha maisha yao kwa kigezo cha ugumu wa maisha na kusema serikali ya mkoa inawabaini watu hao na itawashughulikia muda mfupi. 

Kwa upande wao wachimbaji hao wamekiri mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa, ni kweli wanafahamu kazi hiyo si halali na wamemuahidi kuachana nayo kama watasaidiwa shughuli mbadala kwani wanafanya hivyo kujitafutia riziki kutoka na hali ngumu ya maisha na masharti ya mikopo kuwa ni magumu.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amewaagiza wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa Mwadui kwanza kutoa elimu kwa wananchi hasa vijana na kuwakataza kufanya uchimbaji haramu, kwani tabia hiyo imeshaota mizizi na kuonekana ni halali katika jamii hiyo, pamoja na kuwasidia vijana hao katika kuibua miradi kutokana na fedha zinazotolewa na mgodiwa Mwadui kila Mwezi. Vilevile, kuwa na uhusiano mzuri na mwekezaji kwa manufaa ya vijiji hivyo.

Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Elisha Nkhamba kusimamia uundwaji wa vikundi vya vijana ili wawezeshwe kufanya shughuli za kuwaiingiziakipato.

Mhe. Rufunga pia ameutaka uongozi wa Mgodi kuimarisha ulinzi katika eneo lao kwa kushirikia na Kamanda wa Polisi wa Mkoa. Amewapongeza na kuwataka kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya mgodi na jamii ya Mwadui kwa kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo na za kuwainua kiuchumi wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Nae Meneja Mkuu wa Mgodi wa Mwadui Arlen Loehmer ameishukuru serikali kwa ushirikiano na kusaidiana kujua na kutatua changamoto mbalimbali, na anaamini katika mahusiano haya mazuri kunaimarisha juhudi za uwekezaji.

Magdalena Nkulu,
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Shinyanga
0766-289802




 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally N. Rufunga akizungumza   na wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa Mwadui jana alipotembelea mgodini hapo kuona uchimbaji haramu unaofanywa na wananchi wa vijiji hivyo.kushoto kwake ni Meneja mgodi Bw. Arlen Loehmer na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu Wilson Nkhambaku




Tuesday, January 7, 2014

MAPOKEZI YA RAIS KIKWETE MKOANI IRINGA KUONGOZA MAZISHI YA MAREHEMU DKT. MGIMWA





















SERIKALI IONGEZE SHULE ZA VIPAJI MAALUM



Serikali imeshauriwa kuandaa mkakati wa kitaifa wa kuongeza idadi ya shule za sekondari za bweni na vipaji maalum kutokana na idad ya wanafunzi kufaulu na kupanda kila mwaka ili kuwatendea haki na kulinda vipaji vya watoto.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista Kalalu wakati akichangia katika kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mkoa wa Iringa kilchofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.

Bibi. Kalalu amesema ufaulu wa wanafunzi unapanda na kuongezeka lakini sekondari za bweni na vipaji maalum haziongezeki jambo linalosababisha kutokuwatendea haki wanafunzi wengi waliofaulu vizuri kukosa nafasi katika shule hizo. Ameshauri kuwa uwepo mkakati wa kitaifa wa kuongeza shule za bweni na vipaji maalum ili kuwapatia fursa watoto wengi zaidi.

Wakati huohuo, Mbunge wa Mufindi Kusini, Bw. Menrad Kigola ameshauli viwepo vyuo vikuu vya vipaji maalum nchini ili kulinda vipaji vya wanafunzi wanaomaliza shule za sekondari. “Tunazo shule za sekondari za vipaji maalum chakushangaza watoto wetu wanapomaliza sekondari wanajiunga na vyuo vikuu vya kawaida jambo linalochangia kupoteza vipaji vya watoto wetu. Umefika wakati wa serikali kuwa na vyuo vikuu vya vipaji maalum ili kulnda na kuendeleza vipaji vya watoto wetu” amesisitiza Bw. Kigola.  

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa kikao hicho ambae pia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Bibi. Wamoja Ayubu amewataka wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti na kuanza masomo shule zitakapofunguliwa. Aidha, amewataka kuhakikisha vikao vya tathmini ya elimu na kuzipongeza shule zilizofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013. 

Bibi. Ayubu amewata kuweka mikakati endelevu ili mwaka 2014 Mkoa wa Iringa ufikie asilimia 70 ambalo ni lengo la Matokeo Makubwa Sasa kwa mwaka huo. Vilevile, amewataka kuhakikisha Kata ambazo zimechukua wanafunzi wengi zaidi kuliko uwezo wa vyumba vya madarasa vilivyopo, kuhakikisha madarasa yanajengwa haraka ili kukidhi idadi ya wanafunzi stahili. Katika kuendeleza ubora wa elimu mkoani, Kaimu Katibu Tawala Mkoa amewataka wakurugenzi kuhakikisha usimamizi na ufuatiliaji unakuwa wa karibu zaidi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara shuleni ili kuondoa tatizo la wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.  
=30=

HALMASHAURI ZA MKOA WA IRINGA ZAPONGEZWA KUVULA MALENGO YA BRN




Halmashauri za Mkoa wa Iringa zimepongezwa kwa kazi nzuri katika sekta ya elimu hadi kufanikisha kuvuka lengo la Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kuuwezesha Mkoa kushika nafasi ya tatu kitaifa katika Mtihani wa darasa la saba kitaifa. 

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wanafunzi wa kujunga na kidato cha kwanza Mkoa wa Iringa, Bibi. Wamoja Ayubu katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Uchaguzi wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 Mkoa wa Iringa kilchofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.

Bibi. Ayubu amesema “kiwango cha ufaulu ni kizuri sana na Mkoa wa Iringa umeshika nafasi ya tatu kati ya mikoa 25 ya Tanzania bara. Pia kiwango cha ufaulu kimepanda kwa Halmashauri zote. Kwa hiyo, nachukua nasafi hii kuzipongeza Halamshauri zote kwa kuvuka lengo la matokeo makubwa sasa ambalo ni asilimia 60 kwa mwaka 2013”.

Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 Mkoa wa Irnga, Afsa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Joseph Mnyikambi amesema kuwa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifanyika tarehe 11-12 Septemba, 2013. Amesema kuwa shule za msingi 449 kati ya shule 482 ndizo likukuwa na watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. 

Akiongelea mahudhurio siku za mitihani, Mwalimu Mnyikambi amesema kuwa mahudhurio yameongezeka kutoka asilimia 98.3 ya mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 99 mwaka 2013 likiwa ni ongezeko la asilimia 0.7. Amesema kuwa kiwango cha kumaliza elimu ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 82 (2012) hadi kufikia asilimia 84 (2013) likiwa ni ongezeko la asilimia 2. Aidha, wanafunzi ambao hawakufanya mtihani mwaka 2013 ni asilimia 1 ukilinganisha na asilimia 1.2 mwaka 2012 kutokana na sababu za utoro, vifo, ugonjwa na mimba.

Akiongelea hali ya ufaulu kwa kila Halmashauri katika Mkoa wa Iringa, Afisa Elimu Mkoa amesema kuwa Iringa Manispaa asilimia 81.9 (1), Mufindi asilimia 63.9 (2), Iringa asilimia 62.2 (3) na Kilolo asilimia 60.3 (4).

Amezitaja shule 10 bora katika Mkoa wa Iringa kuwa ni Sipto (1), Ummu Salaama (2), Ukombozi (3), St. Dominic Savio  (4), Star (5), Wilolesi (6), St. Charles (7) zote za Manispaa ya Iringa. Nyingine ni Brooke Bond (8), Southern Highland (9) Mufindi na Mapinduzi (10) Manispaa ya Iringa.
=30=

Friday, January 3, 2014



OFISI YA WAZIRI MKUU
RATIBA YA MAZISHI YA ALIYEKUWA WAZIRI WA FEDHA
DKT. WILLIAM A. MGIMWA
TAREHE
SIKU
MUDA
TUKIO
WAHUSIKA
4.1.2014
JUMAMOSI
7.00 MCHANA
MWILI WA MAREHEMU KUWASILI UWANJA WA NDEGE WA MWALIMU NYERERE – TERMINAL II NA KUPELEKWA NYUMBANI MIKOCHENI B
NDUGU
VIONGOZI
WANANCHI
KAMATI
11.00 JIONI
MWILI KUPELEKWA HOSPITALI YA LUGALO
KAMATI
5.1.2014
JUMAPILI
3.00 – 4.00 ASUBUHI
CHAKULA NYUMBANI KWA MAREHEMU
KAMATI
4.30 ASUBUHI
MWILI KUWASILI NYUMBANI
KAMATI
5.30 – 8.00 MCHANA
MWILI KUPELEKWA UKUMBI WA KARIMJEE, KWA AJILI YA IBADA NA HESHIMA ZA MWISHO
KAMATI
8.00 MCHANA
MWILI KUPELEKWA UWANJA WA NDEGE WA MWALIMU NYERERE – TERMINAL 1
KAMATI YA KI - TAIFA
10.00 JIONI
MWILI KUWASILI IRINGA
(NDULI AIRPORT) NA KUAGWA KATIKA UKUMBI WA SIASA NI KILIMO - IRINGA
MKUU WA MKOA
KAMATI YA MKOA
KAMATI YA KI - TAIFA
11.30 JIONI
KUELEKEA KIJIJINI MAGUNGA
MKUU WA MKOA
KAMATI YA MKOA
KAMATI YA KI - TAIFA
6.1.2014
JUMATATU
6.00 MCHANA
SHUGHULI ZA MAZISHI KIJIJINI KWA MAREHEMU MAGUNGA
MKUU WA MKOA
KAMATI YA MKOA
KAMATI YA KI - TAIFA




TANZIA



TANZIA
WAKUU WA IDARA/VITENGO
WATUMISHI WOTE
WIZARA YA FEDHA

TUNASIKITIKA KUTANGAZA KIFO CHA WAZIRI WA FEDHA MHE. DKT. WILLIAM A. MGIMWA (MB) KILICHOTOKEA TAREHE 01 JANUARI, 2014 HUKO AFRIKA KUSINI, KATIKA HOSPITALI YA KLOOF MEDI – CLINIC, PRETORIA.  MWILI WA MAREHEMU UNATARAJIA KUWASILI SIKU YA JUMAMOSI TAREHE 04/01/2014 NA UTASAFIRISHWA KWENDA MKOANI IRINGA SIKU YA JUMAPILI TAREHE 05/01/2014 KWA MAZISHI.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU
MAHALI PEMA PEPONI.  AMEN

2 JANUARI, 2014