Wednesday, July 8, 2015

CMT H/W IRINGA ITEKELEZE MPANGO NA BAJETI MWAKA 2015/2016



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Menejimenti ya halmashauri ya wilaya ya Iringa yatakiwa kufanya maamuzi sahihi kwa kufuata mpango na bajeti wa mwaka 2015/2016 ili kutokujitengenezea madeni.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, bibi Amina Masenza wakati wa uvunjaji wa Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Iringa lililofanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Mkuu wa mkoa amewataka kuhakikisha maamuzi yatakayofanywa baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani yanakuwa yale tu yaliyo ndani ya mpango na bajeti ya halmashauri wa mwaka 2015/2016 kama ilivyoidhinishwa na Baraza la Madiwani. Amewataka kutunza vizuri nyaraka zote za maamuzi yatakayofanyika katika kipindichote baada ya Baraza hilo kuvunjwa. “Natambua kuwa waheshimiwa madiwani wote na hata watendaji mnatambua kuwa wakati madiwani watakuwa hawapo katika nafasi zao ndani ya halmashauri, maamuzi ambayo yangefanywa na madiwani sasa yatafanywa na Kamati ya Menejimenti ya halmashauri (CMT), wafanye maamuzi ya busara na yenye manufaa kwa halmashauri” alisema bibi Masenza. 

Amesema kuwa mkoa utaendelea kuwa karibu na halmashauri kwa ushauri na ufuatiliaji wa masuala ya serikali za mitaa. Aidha, amezitaka serikali za mitaa mkoani Iringa kuomba usaidizi unaotakiwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya halmashauri.

Mkuu wa mkoa wa Iringa amewahakikishia madiwani hao kuwa serikali itaendelea kujivunia michango yao waliyoitoa na kuifanya halmashauri ya wilaya ya Iringa kuwa mfano kwa kuongoza katika ukusanyaji wa mapato ya ndani mwaka 2013/2014, kupata hati safi, kuwa mshindi wa mkoa katika mashindano ya nanenane kikanda yaliyofanyika mkoani Mbeya mwaka jana na kuwa halmashauriya kwanza kimkoa katika mashindano ya ukimbizaji Mwenge wa Uhuru mwaka jana.

Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa amesema kuwa anajivunia uhusiano mzuri baina ya baraza lake na watendaji wa halmashauri katika kufanikisha shughuli za kuwahudumia wananchi. Ameitaka halmashauri kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuboresha huduma kwa wananchi. Amesema kuwa mapato ya ndani ya halmashauri ndiyo msingi wa kuwaletea maendeleo wananchi kwa sababu mipango na matumizi yake inaendana na mazingira halisi ya halmashauri.
=30=

MIRADI 35 KUPITIWA NA MWENGE WA UHURU IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mwenge wa Uhuru utaweka mawe ya msingi, kukagua, kuzindua na kufungua miradi 35 yenye thamani ya shilingi 4,985,562,793 katika mkoa wa Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Bibi Amina Masenza alipokuwa akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajab Rutengwe katika eneo la Ruaha Mbuyuni wilayani kilolo.
Bibi. Masenza amesema “Mwenge wa Uhuru katika mkoa wa Iringa utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 35 yote ikiwa na thamani ya shilingi 4,985,562,793 ambapo kati ya fedha hizo serikali kuu imechangia shilingi 2,193,787,197 halmashauri za wilaya na manispaa shilingi 1,191,486,781, michango ya wananchi shilingi 1,158,299,859 na wadau wa maendeleo shilingi 441,988,956”. Amesema kuwa jumla ya miradi 6 itafunguliwa, miradi 18 itazinduliwa, miradi 5 itawekewa mawe ya msingi na miradi 6 itakaguliwa na Mwenge wa Uhuru. Miradi hiyo inatokana na sekta za kilimo, mifugo, maji, maliasili, ujenzi, barabara, afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zimebeba ujumbe usemao “tumia haki yako ya kidemokrasia; chini ya kaulimbiu; jiandikishe na kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2015. Amesema kuwa ujumbe huo ni muhimu katika kipindi ambapo watanzania wanapaswa kushikamana zaidi na kudumisha amani na utulivu licha ya tofauti za itikadi ya vyama.
Amesema kuwa ujumbe maalumu umeambatana na jumbe za kudumu nne ambazo ni mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya ukimwi na mapambano dhidi ya malaria.
=30=

Tuesday, June 2, 2015

SEKTA YA MADINI KUINGIZA WATU 6,000 MKOANI NJOMBE



Christopher Philemon - NJOMBE
Zaidi ya wachina 6,000 wanatarajiwa kuingia katika Mkoa wa Njombe kwenye sekta ya madini hasa makaa ya mawe  na chuma kwenye eneo la Liganga na Mchuchuma wilayani Ludewa.

Hayo yamesemwa  jana kwenye Ukumbi wa Lutheran Makambako na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dk. Rehema Nchimbi alipokuanaongea na watumishi wa Halmashuri ya Mji Makambako, alisema kuwa Mradi wa Linganga  na Mchuchuma unatarajiwa kuanza kuchimbwa makaa ya m awe na chuma hivi karibuni utatoa ajira zaidi ya 30,000 zikiwepo  za wazawa na wageni.

Kutokana na hilo amewataka watumishi wa Halmashauri ya Mji Makambako hasa sekta ya Ardhi kuakikisha wanaweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi na kupima viwanja ili kuwavutia wawekezaji mbalimbali katika ujenzi wa Hoteli za kisasa na halmashuri kuakikisha wanaboresha miundombinu ya Maji na barabara .

Dk. Nchimbi alisema kuwa mpaka sasa shirika la maendeleo ya Taifa (NDC) limeanza mchakato wa uthamini  wa mali za wananchi ili waweze kulipwa fidia kupisha mradi huo.

Aliwataka wananchi wa  Makambako na Njombe kwa Ujumla kujiandaa na ujio wa wageni mbalimbali kwa kufuga kuku, ng’ombe pamoja na mifugo mingine ili  kuweza kuwauzia wageni hao na kuongeza kipato cha familiya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako Hanana Chesco Mfikwa alisema kuwa  wanajiandaa kwa kuwapokea wageni hao kwa kuakikisha wanaweka mipango mizuri ambayo itasaidia wageni kuwekeza zaidi katika eneo la Makambako.
=30=

NJUWASA YAPOKEA BIL. 2.6 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI NJOMBE




Christopher Philemon - NJOMBE

Mamlaka ya Maji Mkoa wa Njombe (NJUWASA)  imepokea kiasi cha fedha 2.6 ( 2,577,138,890.00)  bilioni  kutoka Wizara ya Maji  toka mwaka 2013 kwa ajili ya kuboresha hudumaya maji katika Mji wa Njombe.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mkoa wa Njombe Mhandisi, Daudi Majani amesema kuwa mpaka sasa fedha hizo zimetumika kujenga chanzo cha maji  cha Nyenga,matanti matatu ya maji na utandazaji wa mabomba ya maji ambapo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi wa saba mwaka huu.

Alisema kuwa mpaka sasa Ujenzi wa kidakio cha maji umekamilika  na ujenzi wa matanki matatu yaliyopo katika maeneo ya Airport, Kambalage, Igeleke na Nzengelendete  na kila tenki linauwezo wa ujazo wa lita 135,000 kila mojaHatua inayoendelea sasa ni utandazaji wa mabomba ya maji katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Njombe.
Mradi huo ukikamilika utawezesha kufanya mji wa Njombe kuongeza upatikanaji wa maji kutoka  asilimia 55 hadi 80  na kufanya mji huo kuondoka na huwaba wa maji .

Majani amesema hayo jana kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dk. Rehema Nchimbi alipotembelea vyanzo vya maji na kuangalia mtandao wa maji katika mji wa Njombe.

Mkuu huyo wa Mkoa amezitaka Halmashuri za Mji wa Njombe kushirikiana na mamlaka ya maji Mkoa wa Njombe kuakikisha wanatoa elimu kwa wananchi waliopo kwenye vyanzo vya maji ili kutunza vyanzo vya hivyo.
=30=





DR. NCHIMBI AWATAKA WATUMISHI KUHAMIA WANGING'OMBE



Christopher Philemon - NJOMBE
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dk.Rehema Nchimbi amewataka  watumishi walioamishiwa  na walioajiliwa katika halmashuri ya Wiaya ya Wanging’ombe   kuakikisha wamehamia kimakazi  katika wilaya hiyo.

Dk. Rehema Nchimbi,amesema kuwa wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe  watakiwa kupata huduma kutoka kwa watumishi hao na anashangaa kuona watumishi wanaishi Njombe mjini na kufanyakazi katika halmashuri ya wilaya ya Wanging’ombe ambayo ipo zaidi ya umbali wa kilometa 40 kutoka Njombe Mjini.

Nchimbi ametoa wiki mmoja toka leo kuakikisha watumishi hao wawe wameamia na kuishi katika Wilaya hiyo ili kuongeza ufanisi wa kazi na kuwa karibu na wananchi, aliyasema hayo kwenye ukumbi wa halmashuri ya wilaya ya Wang’ingombe wakati akifanya mkutano wa watumishi wa halmshauri hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Fedrick Mwakalebela  alisema kuwa Wilaya hiyo inamahitaji yote  muhimu kama vile ofisi, miundombinu ya maji na barabara  na kuwasihi watumishi hao wakikishe wanahamia katika wilaya hiyo haraka iwezekanazo kwani maendeleo ya Wanging’ombe yataletwa na wananchi wa Wanging’ombe kwa kushilikiana na watumishi. 

Mkurungenzi wa Wilaya hiyo Melizedeki Humbe alisema kuwa watumishi wengi katika wilaya hiyo bado wanaishi Njombe mjini lakini wamewaka mikakati ambayo ndani ya wiki mmoja waliopewa kuakikisha watumishi hao wote wanaamia katika wilaya hiyo mpya iliyo anzishwa mwaka 2012.
=30=