Wednesday, September 23, 2015

FOX APONGEZWA KWA KAZI ZA KIJAMII MUFINDI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza amepongeza kazi za kijamii zinazofanywa na muwekezaji Geoff Fox kwa lengo la kuwapunguzia umasikini wananchi wa Mufindi.
Pongezi hizo alizitoa alipotembelea shughuli za maendeleo zinazofanywa na muwekezaji huyo wilayani Mufindi kwa lengo la kujifunza pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa. “Nimefurahishwa na kazi za kijamii zinazofanywa na muwekezaji za kuisaidia jamii katika sekta za afya, elimu na ustawi wa jamii. Kazi hizi ni jukumu letu kama serikali lakini kutokana na sera yetu ya ushirikishaji jamii na sekta binafsi, sekta binafsi inapata fursa ya kusaidia juhudi hizi za kimaendeleo” alisema Masenza.
Alipotembelea zahanati ya Mdabulo inayomilikiwa na kanisa katoliki Jimbo la Iringa, mkuu wa mkoa alipongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na zahanati hiyo iliyoanzishwa mwaka 1946 ikiwa umbali wa km 48 kutoka mjini Mafinga. Masenza alishauri uandaliwe utaratibu wa kutoa elimu ya magonjwa ya kisukari na saratani na mlango wa kizazi kutokana na magonjwa hayo kutokupewa kipaumbele. “Magonjwa ya kisukari na saratani ya mlango wa kikazi yamekuwa hayapewi umuhimu sana lakini yanachangia sana katika vifo vya wananchi wetu. Ni vizuri mkaweka utaratibu wa kuwa mnatoa elimu ya utambuzi na kujikinga na magonjwa haya ili kupunguza hatari ya vifo” alisema Masenza. Masenza aliiagiza halmashauri kununua mitungi …na siki ili kusaidia uchunguzi wa saratani hiyo.
Mkuu wa mkoa aliwaagiza wataalamu wa sekta ya afya wa halmashauri ya wilaya ya mufindi kuweka utaratibu wa kuitembelea zahanati ya Mdabulo mara kwa mara na kutoa ushauri wa kitaalam.
Kutokana na zahanati hiyo kuwahudumia wananchi wengi, mkuu wa mkoa alimuagiza mganga mkuu wa mkoa kufuatilia mchakato wa kuipandisha hadhi zahanati ya Mdabulo kuwa kituo cha afya ufanyike haraka…ili…
=30=
 

WATUMISHI FEKI HAWANA NAFASI IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umejipanga kukabiliana na watumishi feki katika sekta ya afya ili kutoa huduma za kitaalam kwa wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na vyombo vya habari juu ya mkoa ulivyojipanga kukabiliana na changamoto ya watumishi wasio na sifa katika sekta ya afya mkoani hapa kufuatia wimbi la watumishi wasio na sifa kubainika wakitoa huduma katika hospitali za serikali.
Ayubu alisema kuwa mkoa wa Iringa upo makini kimfumo na rasilimali watu kukabiliana na tatizo la watumishi feki. Alisema mifumo ya kuhakiki watumishi imeboreshwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni kwa lengo la kukabiliana na watumishi feki.
“Mtumishi yeyote anapoajiliwa anawasilisha vyeti vyake vya kitaaluma alivyonavyo na vinakaguliwa. Kutokana na wimbi la kugushi vyeti, mkoa umepanua wigo kwa kushirikisha taasisi zote zinazohusika na utoaji vyeti husika kama NECTA, NACTE, vyuo vikuu ili wathibitishe uhalali wa vyeti hivyo”, alisisitiza Ayubu.
Aliongeza kuwa mfumo wa kieletroniki wa malipo na mishahara ulioanza mwaka 2011, umeongeza ufanisi katika udhibiti wa vyeti feki kwa sababu mfumo unaingiza vyeti vyote kasha vinaenda kuhakikiwa Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Alisema kuwa pamoja na kusaidia kubaini watumishi wenye vyeti feki chini mfumo huo umeondoa tatizo la watumishi kulipwa zaidi ya mara moja na kuondoa changamoto ya mishahara hewa. Katika mfumo huu kama mtumishi alishaajiliwa serikalini mfumo utamgundua kirahisi hivyo kuwa vigumu kulipwa mshahara zaidi ya mmoja. Alisema kuwa hata ule mchezo wa watu kutumia vyeti vya watu wengine unapatiwa tiba.
Ayubu aliongeza kuwa watumishi wote wa serikali wanavaa vitambulisho vya vya kazi vinavyomtambulisha jina kamili na cheo ili iwe rahisi kwa anayepewa huduma kumtambua mtoa huduma. Ameongeza utaratibu huo unaondoa malalamiko kwa wananchi kwa sababu kila mtumishi anafahamika kwa jina na cheo chake.
Ayubu alisema mwaka 2011 mkoa ulifanya uhakiki wa taarifa za watumishi wa umma ili kubaini uwepo wa watumishi hewa. Alisema kuwa anajivunia kutokuwepo kwa watumishi hewa na mishahara hewa.
Afisa utumishi katika ofisi ya mkuu wa mkoa, Gasto Andongwisye alisema katika kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa na watumishi wenye sifa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma na kudhibiti mishahara hewa, ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia sehemu ya utawala na rasilimali watu imeendelea kufanya uhakiki kila mwezi kwa watumishi na ‘payroll’.
Andongwisye aliongeza kuwa katika kuhakikisha hakuna mtumishi mamluki anayejipenyeza katika hospitali za serikali mkoani hapa na kutoa huduma, idara zote katika hospitali wamekuwa wakifanya vikao vya kila siku kupeana taarifa za kazi na vikao vya watumishi wote kila idara kwa lengo la kufahamiana na kujadili changamoto zilizopo.
=30=




MKOA WA IRINGA WAFANIKIWA KUZUIA MIMBA ZA WANAFUNZI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umejitahidi kudhibiti mimba kwa wasichana wa shule za msingi na kuongeza idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya msingi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa kamati ya mitihani mkoa wa Iringa, Mwl Euzebio Mtavangu alipokuwa akifafanua maandalizi ya mkoa wa Iringa katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015 utakaofanyika kuanzia kesho nchini nzima.
Mwl Mtavangu ambaye pia ni Kaimu afisa elimu wa mkoa wa Iringa alisema kuwa mwaka 2015 idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya msingi ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wavulana kutokana na mkoa kudhibiti tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike katika shule za msingi. Alisema kuwa kati ya watahiniwa 21,323 wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015, wasichana ni 11,448 na wavulana ni 9,875. Alisema kuwa tofauti na miaka ya nyuma ambayo idadi ya wasichana waliokuwa wakihitimu elimu ya msingi ilikuwa ndogo kutokana na wasichana wengi kupata ujauzito na kushindwa kumaliza elimu ya msingi. Alisema kwa kutambua umuhimu na nafasi ya mtoto wa kike katika jamii, mkoa wa Iringa utaendelea kudhibiti mimba kwa wasichana ili wote waweze kumaliza elimu ya msingi na kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa. Akifafanua ongezeko hilo kwa kila halmashauri, alilitaja ongezeko hilo kwa kila halmashauri kama ifuatavyo; Manispaa ya Iringa Wasichana (1,748) na wavulana (1,534), halmashauri ya wilaya ya Iringa Wasichana (3,046) na wavulana (2,618), halmashauri ya wilaya ya Kilolo wasichana (3,088) na wavulana (2,776) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi wasichana (3,566) na wavulana (2,947).
Mwl Mtavangu alisema kuwa jumla ya shule 457 zitafanya mhihani huo kwa mkoa wa Iringa, ikiwa ni Manispaa ya Iringa shule (41), halmashauri ya wilaya ya Iringa (142), halmashauri ya wilaya ya Kilolo (106) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi (168). Alisema kuwa katika mtihani huo, jumla ya mikondo 977 katika shule hizo 457 itahusika ikiwa na wasimamizi 977.
Aliwataja watahiniwa wengine kuwa ni watahiniwa wasioona watano wasichana wakiwa watatu na wavulana wawili. Wengine ni watahiniwa wenye uono hafifu 33, wasichana (18) na wavulana (15).
Kwa upande wa shule zenye mchepuo wa kiingereza alisema kuwa shule hizo zipo 10 zenye jumla ya watahiniwa 455, wasichana wakiwa 222 na wavulana 233. Katika siku ya kwanza mitahani ya sayansi, hisabati na Kiswahili itafanyika ikifuatiwa na mitihani ya kiingereza na maarifa ya jamii.
Akiongelea matarajio ya ufaulu kwa mkoa wa Iringa, alisema kuwa mkoa unatarajia kupanda hadi nafasi ya pili kitaifa kutoka nafasi ya nne ya mwaka 2014 huku watahiniwa wakitarajiwa kufaulu kwa zaidi ya asilimia 75 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2014 wa asilimia 68.58. Ikumbukwe kuwa mkoa wa Iringa umekuwa ukishika kati ya nafasi ya tatu na nne kwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa miaka 18 mfululizo.
=30=

Wednesday, July 8, 2015

CMT H/W IRINGA ITEKELEZE MPANGO NA BAJETI MWAKA 2015/2016



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Menejimenti ya halmashauri ya wilaya ya Iringa yatakiwa kufanya maamuzi sahihi kwa kufuata mpango na bajeti wa mwaka 2015/2016 ili kutokujitengenezea madeni.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, bibi Amina Masenza wakati wa uvunjaji wa Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Iringa lililofanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Mkuu wa mkoa amewataka kuhakikisha maamuzi yatakayofanywa baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani yanakuwa yale tu yaliyo ndani ya mpango na bajeti ya halmashauri wa mwaka 2015/2016 kama ilivyoidhinishwa na Baraza la Madiwani. Amewataka kutunza vizuri nyaraka zote za maamuzi yatakayofanyika katika kipindichote baada ya Baraza hilo kuvunjwa. “Natambua kuwa waheshimiwa madiwani wote na hata watendaji mnatambua kuwa wakati madiwani watakuwa hawapo katika nafasi zao ndani ya halmashauri, maamuzi ambayo yangefanywa na madiwani sasa yatafanywa na Kamati ya Menejimenti ya halmashauri (CMT), wafanye maamuzi ya busara na yenye manufaa kwa halmashauri” alisema bibi Masenza. 

Amesema kuwa mkoa utaendelea kuwa karibu na halmashauri kwa ushauri na ufuatiliaji wa masuala ya serikali za mitaa. Aidha, amezitaka serikali za mitaa mkoani Iringa kuomba usaidizi unaotakiwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya halmashauri.

Mkuu wa mkoa wa Iringa amewahakikishia madiwani hao kuwa serikali itaendelea kujivunia michango yao waliyoitoa na kuifanya halmashauri ya wilaya ya Iringa kuwa mfano kwa kuongoza katika ukusanyaji wa mapato ya ndani mwaka 2013/2014, kupata hati safi, kuwa mshindi wa mkoa katika mashindano ya nanenane kikanda yaliyofanyika mkoani Mbeya mwaka jana na kuwa halmashauriya kwanza kimkoa katika mashindano ya ukimbizaji Mwenge wa Uhuru mwaka jana.

Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa amesema kuwa anajivunia uhusiano mzuri baina ya baraza lake na watendaji wa halmashauri katika kufanikisha shughuli za kuwahudumia wananchi. Ameitaka halmashauri kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuboresha huduma kwa wananchi. Amesema kuwa mapato ya ndani ya halmashauri ndiyo msingi wa kuwaletea maendeleo wananchi kwa sababu mipango na matumizi yake inaendana na mazingira halisi ya halmashauri.
=30=

MIRADI 35 KUPITIWA NA MWENGE WA UHURU IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mwenge wa Uhuru utaweka mawe ya msingi, kukagua, kuzindua na kufungua miradi 35 yenye thamani ya shilingi 4,985,562,793 katika mkoa wa Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Bibi Amina Masenza alipokuwa akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajab Rutengwe katika eneo la Ruaha Mbuyuni wilayani kilolo.
Bibi. Masenza amesema “Mwenge wa Uhuru katika mkoa wa Iringa utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 35 yote ikiwa na thamani ya shilingi 4,985,562,793 ambapo kati ya fedha hizo serikali kuu imechangia shilingi 2,193,787,197 halmashauri za wilaya na manispaa shilingi 1,191,486,781, michango ya wananchi shilingi 1,158,299,859 na wadau wa maendeleo shilingi 441,988,956”. Amesema kuwa jumla ya miradi 6 itafunguliwa, miradi 18 itazinduliwa, miradi 5 itawekewa mawe ya msingi na miradi 6 itakaguliwa na Mwenge wa Uhuru. Miradi hiyo inatokana na sekta za kilimo, mifugo, maji, maliasili, ujenzi, barabara, afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zimebeba ujumbe usemao “tumia haki yako ya kidemokrasia; chini ya kaulimbiu; jiandikishe na kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2015. Amesema kuwa ujumbe huo ni muhimu katika kipindi ambapo watanzania wanapaswa kushikamana zaidi na kudumisha amani na utulivu licha ya tofauti za itikadi ya vyama.
Amesema kuwa ujumbe maalumu umeambatana na jumbe za kudumu nne ambazo ni mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya ukimwi na mapambano dhidi ya malaria.
=30=