Saturday, December 16, 2017

WADAU WA VVU/UKIMWI IRINGA WATAKIWA KUJITATHMINI



Na Ofisi ya mkuu wa Mkoa
Wadau wa mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na Ukimwi wametakiwa kujitathmini katika utekelezaji wa mkakati wa kupambana na VVU baada ya mbinu za awali kuonesha kushindwa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao cha kuutambulisha mradi wa USAID Tulonge Afya kilichofanyika katika hoteli ya Gentle Hills iliyopo mjini Iringa.
 
RAS Wamoja Ayubu
Ayubu alisema matokeo ya utafiti wa VVU na UKIMWI (2016/2017) yameonesha kuwa maambukizi ya VVU mkoani Iringa yameongezeka kutoka asilimia 9.1 hadi 11.3. “Maambukizi ya VVU mkoani Iringa yameongezeka kutoka asilimia 9.1 ya awali (2011/12) kufikia asilimia 11.3 (2016/17). Hii ni ishara wazi kuwa maambukizi mapya yameongezeka kwa asilimia 2.2” alisema Ayubu.

Aidha, aliwataka wadau wa mapambano dhidi ya VVU kujitathmini ili kuona maeneo ambayo hawakufanya vizuri. 

Tunatakiwa tujitathmini kuona ni wapi ambapo hatujafanya vizuri katika utekelezaji wa program zetu za mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU” alisema Ayubu.

Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa wadau wa maendeleo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika kuwaletea maendeleo na kuboresha afya za wananchi mkoani Iringa. 

Uwepo wenu katika Mkoa huu umeongeza kasi ya serikali ya Mkoa na Halmashauri zake ya kuwafikia wananchi katika jitihada zao mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maisha, hasa kujikwamua kiuchumi na kuimarisha afya zao” alisema Ayubu.
=30=

USAID TULONGE AFYA WATAKIWA KUTUMIA FEDHA ZA MRADI KWA MALENGO KUSUDIWA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watekelezaji wa mradi wa USAID Tulonge Afya wametakiwa kutumia fedha za utekelezaji kwa mujibu wa taratibu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao cha kuutambulisha mradi wa USAID Tulonge Afya kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hills iliyopo mjini Iringa jana.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Ayubu alisema kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zinatolewa na serikili ya Marekani kupitia shirika la maendeleo la Marekani USAID. 

Naomba fedha hizi zikatumike kwa kufuata utaratibu ili kufanikisha kufikia malengo yake. Nataka niwakumbushe kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kikamilifu katika kusimamia na kufuatilia matumizi sahihi ya fedha za wadau wa maendeleo na za serikali kwa lengo la kuhakikisha kuwa thamani ya fedha kwenye miradi ya maendeleo inazingatiwa na watekelezaji” alisema Ayubu.

Alisema kuwa mradi huo unalenga kuhamasisha wanajamii kutumia huduma za afya zinazotolewa kwenye vituo vya afya. 

Ninawahakikishia kuwa serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana nanyi katika uboreshaji wa huduma ili wananchi wakishahamasika waweze kwenda vituoni na kupata huduma zilizo bora” alisema Ayubu.
=30=




MRADI WA USAID TULONGE AFYA WAPONGEZWA KWA KUTUMIA APROCHI YA ‘SBCC’



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
USAID Tulonge Afya wapongezwa kwa kuchagua kutumia mbinu za mabadiliko ya tabia kwa wanajamii (Social Behavior Change Communication approach) katika kufanikisha malengo ya mradi huo.

Pongezi hizo zilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao cha kuutambulisha mradi wa USAID Tulonge Afya unaotekelezwa na shirika la FHI 360 kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hills mjini Iringa jana.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Ayubu alisema kuwa mradi huo umechagua kutumia mbinu za mabadiliko ya tabia kwa wanajamii (SBCC). 

Nimefurahishwa sana kwa kutambua umuhimu wa mbinu hii mliyoichagua katika kuleta mabadiliko hasa pale inapotumika kwa ufasaha” alisema Ayubu. 

Aidha, alimtaka meneja mradi wa kanda kusimamia vizuri mradi huo ili mwisho wa utekelezaji mabadiliko chanya ya tabia za wananchi yaweze kuonekana.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa aliutaka mradi wa USAID Tulonge Afya kusaidia kuongeza kasi katika utekelezaji wa mkakati wa Mkoa wa kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi. 

Natambua pia mkakati wa Mkoa ni kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI, kuhakikisha wanaoishi na maambukizi ya VVU wanakuwa na ufuasi mzuri wa dawa, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kupunguza maambukizi ya Malaria pamoja na kuongeza matumizi ya huduma za uzazi wa mpango” alisema Ayubu.
=30=

KAMATI ZA UENDESHAJI MITIHANI MKOANI IRINGA ZAPONGEZWA KUDHIBITI UDANGANYIFU



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kamati za uendeshaji wa mitihani ngazi za Wilaya na Mkoa zimepongezwa kwa usimamizi madhubuti wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na kudhibiti udanganyifu.

Pongezi hizo zilitolewa na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa jana.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Ayubu alisema kuwa mwaka 2017 Mkoa wa Iringa haukukumbwa na tuhuma za udanganyifu. “Kipekee nazipongeza kwa dhati kamati za uendeshaji wa mitihani za Wilaya na ya Mkoa kwa usimamizi mzuri. Nitoe wito kuwa usimamizi huu uendelee  kwa mitihani ya kitaifa ya ngazi zote ili kuepukana na suala la udanganyifu ambalo kwa kiasi kikubwa madhara yake ni makubwa kwa mwanafunzi mwenyewe, mwalimu aliyehusika na udanganyifu na Taifa kwa ujumla” alisema Ayubu.

Akiongelea idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani, alisema kuwa
watahiniwa 24,784 (wavulana 11,421 na wasichana 13,363) sawa na 99.5% walifanya mtihani. Aliongeza watahiniwa 20,606 (wavulana 9513 na wasichana 11,093) sawa na asilimia 83.14 wamefaulu mtihani huo. Alisema wanafunzi walioshindwa kufaulu mtihani huo ni 4,178 ikiwa wavulana 1,908 na wasichana 2,270 sawa na asilimia 16.86

“Kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 0.27 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana ambapo ufaulu ulikuwa ni 82.87%. Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wadau wote wa elimu katika Mkoa wetu ambao mchango wao ni mkubwa kwa ongezeko hili la ufaulu na kuufanya Mkoa wetu kuwa wa Nne (4) kitaifa kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara alisema Ayubu.

Mwaka 2017 Mkoa wa Iringa ulikuwa na watahiniwa 24,905 waliosajiliwa kufanya mtihani, wakiwemo wavulana 11,490 na wasichana 13,415 katika shule 481.
=30=

MKOA WA IRINGA UMEONGEZA KIWANGO CHA UFAULU KWA 0.27%



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2017 kwa asilimia 0.27 na kushika nafasi ya nne kitaifa.

Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika hotuba yake ya ufunguzi kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Ayubu alisema “watahiniwa 20,606 (wavulana 9,513 na wasichana 11,093) sawa na asilimia 83.14 wamefaulu mtihani huo. Hali kadhalika walioshindwa kufaulu mtihani huo ni 4,178 ikiwa wavulana 1,908 na wasichana 2,270 sawa na asilimia 16.86.
Kiwango hiki cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 0.27 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana ambapo ufaulu ulikuwa ni 82.87% ninapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wadau wote wa elimu katika Mkoa wetu ambao mchango wao ni mkubwa kwa ongezeko hili la ufaulu na kuufanya Mkoa wetu kuwa wa Nne kitaifa kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara”.

Ayubu ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alisema kuwa ongezeko hilo la ufaulu ni jambo jema na kutahadharisha kuwa linaibua changamoto ya uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari. “Ongezeko la ufaulu ni jambo jema kwetu lakini linaibua changamoto ya uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa katika shule zetu za sekondari au ujenzi wa shule mpya za Sekondari ili kuweza kuwachukua wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza” alisema Ayubu.

Aidha, aliwataka wajumbe kuangalia jinsi ya kuongeza vyumba vya madarasa au kujenga shule za sekondari maeneo ambayo yamekuwa na wanafunzi wengi wanaofaulu hasa mijini. Aliongeza kuwa ongezeko la ujenzi wa vyumba vya madarasa liambatane na uongezaji wa meza na viti ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata meza na viti.

Mkoa wa Iringa ulikuwa na watahiniwa 24,905 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2017, kati yao wavulana 11,490 na wasichana 13,415 katika shule 481.
=30=