Sunday, October 1, 2017

IRINGA KITOVU CHA UTALII KUCHOCHEA UCHUMI



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Mkoa wa Iringa uliteuliwa kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini kwa maana ya kuwa kichocheo cha kukuza uchumi kwa ukanda wa kusini.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza katika salamu zake katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya utalii Duniani, maonesho ya Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo (SIDO), yaliyofanyika katika uwanja wa kichangani Manispaa ya Iringa jana.

Mheshimiwa Masenza alisema kuwa mkoa wa Iringa uliteuliwa kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya kusini na wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2002. Alisema katika mwaka huo maonesho ya Utalii Karibu Kusini yalifanyika kwa mara ya kwanza katika ukanda huo. 
Kwa msingi huo tupo hapa leo kuendeleza jitihada hizo za kuendeleza utalii. Lakini kwa kuwa serikali yetu inahimiza maendeleo ya viwanda, maonesho haya ya Utalii ya Karibu Kusini yanafanyika sambamba na maonesho ya shughuli za wajasiriamali (SIDO) katika kuenzi na kuendeleza maendeleo ya viwanda” alisema mheshimiwa Masenza.

Mkuu wa mkoa wa Iringa, alisema kuwa hulka ya sekta ya utalii, maendeleo yake yanategemea na sekta nyingine, “mikoa ya nyanda za juu kusini inatupasa kuendeleza sekta nyingine kama kilimo, ufugaji, usindikaji wa bidhaa mbalimbali, matumizi ya teknolojia bora na nafuu, uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya utunzaji mazingira na kutafuta mitaji na masoko kwa ajili ya kukuza biashara ya utalii” alisema mheshimiwa Masenza.

Aidha, aliahidi kuwa mkoa wake daima utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ya mfano na kukua kwa kasi.
Siku ya utalii Duniani, maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo SIDO yanalenga kuelimisha umuhimu wa sekta ya utalii na viwanda kwa maendeleo ya wananchi wa mikoa ya kusini. 
=30=


No comments:

Post a Comment