Sunday, October 1, 2017

JAMII YATAKIWA KUJIVUNIA RASILIMALI ZA NCHI



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Jamii imetakiwa kujivunia nchi na rasilimali zilizopo pamoja na vivutio vya utalii na kuvilinda ili viwe endelevu.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa wilaya ya Mufindi, Jamhuri William aliyemuwakilisha mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza katika usiku wa Utalii Karibu Kusini uliofanyika katika chuo cha ualimu Kreluu mjini Iringa jana.

William alisema kuwa jamii ya mikoa ya nyanda za juu kusini inatakiwa kujivunia nchi yao na rasilimali zilizopo hasa utunzaji na uhifadhi wa vivutio vya utalii. “Utalii ni uzalendo, lazima tujivunie nchi yetu na rasilimali tulizonazo. Vivutio vya utalii vyote tunavyoviona na kuvisikia ni sehemu ya rasilimali muhimu za nchi ambazo lazima tuzitunze ili nazo zituletee uchumi” alisema William.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William

Mkuu wa wilaya ya Mufindi alishauri rasilimali vivutio vya utalii kuhifadhiwa na kutunzwa ili visiharibiwe na kutoweka. “Katika utunzaji wa vivutio vya kitalii, ndiyo vitatuletea fedha nyingi na hatimae kukuza uchumi wa nchi yetu” alisema William.

Alisema kuwa serikali imeamua kuutangaza utalii kisayansi ili ulete matokeo kwa wananchi. Aliwaomba wananchi kuwa sehemu ya kutangaza utalii ili kuleta mafanikio makubwa zaidi.

Akitoa maoni yake, mwanafunzi wa chuo cha ualimu Kreluu, Yuster Tweve alisema kuwa usiku wa Utalii Karibu Kusini ni fursa nzuri ya kuwakutanisha wadau mbalimbali pamoja na kujadili fursa zilizopo katika sekta ya utalii. Alishauri kuwa usiku wa utalii uwe unafanyika siku zote za maonesho ya Utalii Karibu Kusini ili wadau mbalimbali wapate nafasi ya kukaa na kubadilishana mawazo yatakayochangia katika kukuza utalii.
=30=

No comments:

Post a Comment