Wednesday, November 2, 2011

WALIMU WATOE DARASA LA VVU/UKIMWI

Walimu Mkoani Iringa wameshauriwa kutumia muda wao kuzungumzia masuala ya VVU/UKIMWI na madhala yake katika jamii pindi wanapokuwa wakifundisha katika utaratibu wao wa kawaida ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa ofisini kwake katika utaratibu wake wa kawaida wa kukutana na waandishi wa habari mara kwa mara na kujadili masuala ya maendeleo na changamoto katika Mkoa.

Dk. Ishengoma amesema “ukimwi ni tatizo sana katika Mkoa wetu wa Iringa hivyo hata kama haupo katika mitala ya elimu lakini ni vizuri kila mwalimu akachukua angalau dakika tano anapoanza au anapomaliza kipindi kuelezea masuala ya UKIMWI”.

Amesema katika kukabiliana na janga hili ni lazima elimu itolewe kwa umakini mkubwa kuanzia darasa la tatu na kuendelea kwa misingi ya kuwaandaa vijana na mapambano hayo.

Akiongelea dawa ya kudumu dhidi ya UKIMWI amesema ipo wazi nayo ni wananchi kubadili tabia sambamba na elimu dhidi ya kujikinga na maambukizi. Amesema kwa wale waaminio basi watumie maandiko matakatifu kama kinga na wale wasioweza kabisa basi zana zitumike, “ila dawa ni wewe mwenyewe kubadili tabia”.

Mkuu wa Mkoa huyo aliwaagiza waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari na makala zinazoelezea madhara ya UKIMWI katika jamii ili kuweza kueneza habari hizo na hatimae kuifikishia jamii taarifa sahihi ili kuweza kuinusuru na kuongeza nguvu kazi katika Mkoa na Taifa.  

IRINGA YAPATA MGAO WA VOCHA

Mkoa wa Iringa unatarajia kupata mgao wa jumla ya vocha 693,000 za pembejeo za kilimo kwa mwaka wa fedha 2011/ 2012.

Akiwasilisha mapendekezo ya mgao wa vocha za pembejeo za kilimo kwa kila Halmashauri kwa msimu wa mwaka 2011/2012 katika kamati ya vocha ya mkoa wa Iringa, Afisa Kilimo Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni ameyataja mapendekezo hayo kwa kila Halmashauri kuwa ni Mufindi (kupandia 44,300, kukuzia 44,300, chotara 44,000, mpunga 300), Makete (kupandia 23,700, kukuzia 23,700, chotara 23,700), Iringa (kupandia 45,000, kukuzia 45,000, chotara 43,500, mpunga 2,500), Njombe Mji (kupandia 21,000, kukuzia 21,000, chotara 21,000), Manispaa (kupandia 4,000, kukuzia 4,000, chotara 4,000), Kilolo (kupandia 26,000, kukuzia 26,000, chotara 25,800, mpunga 200), Njombe (kupandia 42,500, kukuzia 42,500, chotara 42,500) na Ludewa (kupandia 24,500, kukuzia 24,500, chotara 24,000 na mpunga 500).

Akiongelea thamani za vocha moja moja msimu katika msimu wa mwaka 2011/ 2012  Nyoni amesema kuwa vocha za kupandia kilo 50 ni shilingi 28,000, kukuzia kilo 50 ni shilingi 18,500, mahindi chotara kilo 50 ni shilingi 20,000 na mpunga kilo 50 ni shilingi 12,000.

Ili kuhakikisha usimamiaji wa vocha hizo za pembejeo unakuwa madhubuti, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amewaagiza wakuu wa Wilaya kusimamia vizuri mchakato mzima wa vocha katika wilaya zao. Vilevile, amewaagiza Wakuu hao wa Wilaya kutokuwafumbia macho mawakala wasio na vigezo ili huduma hiyo iweze kufanikiwa na kuwanufaisha wananchi kama yalivyo madhumuni ya Serikali.

Amesema “mfumo huu wa vocha ni mzuri sana ila una mianya ya rushwa hivyo tusichague mawakala matapeli bali  tuchague mawalaka wenye rekodi nzuri na wasio na madeni” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

KAMATI YA VOCHA NAYO YANYOOSHEWA KIDOLE

Kamati ya vocha ya ruzuku ya pembejeo za kilimo ngazi ya Mkoa wa Iringa imetakiwa kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa katika kusimamia menejimenti ya vocha za pembejeo za kilimo ikiwa ni pamoja na mfumo wa uchaguzi wa mawakala unaozingatia vigezo na uwezo.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo ngazi ya mkoa ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma “kamati na kila mmoja ni lazima awe mwangalifu katika kusimamia menejimenti ya ugawaji na usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo ili kuhakikisha zoezi zima linafanikiwa”. Ameongeza kuwa lazima utumike mfumo mzuri na madhubuti wa kuwapata mawakala utakaozingatia vigezo na uwezo wao ili kuondoa ubabaishaji ambao umekuwa ukijitokeza na kusababisha wakulima kutokunufaika na ruzuku hiyo ya serikali wakati mawakala wakiendelea kutajirika kupitia migogo ya wakulima. Amesisitiza kuwa ni vizuri kuwa na mawakala wachache wenye vigezo kuliko kuwa na mawakala wengi wasio na vigezo.     

Akiwakilisha taarifa ya upatikanaji na usambazaji wa vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mwaka 2010/2011, Afisa Kilimo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni amesema kuwa Mkoa umepokea vocha zenye thamani ya shilingi Bilioni 21.6. Amesema vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo zilizopokelewa na Mkoa ni za kutosha Kaya 336,635 ambazo ni sawa na vocha 1,009,905 kwa ujumla wa nakala moja moja ya vocha.

Akiongelea idadi ya mawakala kwa Mkoa wa Iringa katika kipindi husika, Nyoni amesema kuwa Mkoa ulikuwa na mawakala 514 waliofanya kazi ya kusambaza pembejeo za kilimo. Amesema miongoni mwa mawakala hao mawakala 390 ndio waliofanya kazi ya kusambaza pembejeo katika ngazi ya vijiji na kata kwa utaratibu wa mfumo wa ruzuku ya pembejeo.

Nyoni amesema changamoto kubwa ni malalamiko kutoka kwa wakulima juu ya kuongezeka kwa bei ya mbolea ilikinganishwa na msimu uliopita. Amesema msimu uliopita bei mkulima alichangia shilingi 48,000 hadi 65,000 ikilinganishwa na msimu 2010/2011 aliochangia shilingi 85,000 hadi 90,000 kwa pembejeo za ekari moja yaani mbegu bora, mbolea ya kupandia na kukuzia. 

MA DC WAAGIZWA KUSIMAMIA VOCHA



MKUU wa Mkoa wa Iringa amewaagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia vizuri mchakato wa vocha za pembejeo za kilimo kwa kutokuwafumbia macho mawakala wababaishaji na wanaojinufaisha kupitia migongo ya wakulima ili kuondoa manung’uniko na wakulima kunufaika na mfumo huu wa vocha za ruzuku za serikali.


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma 
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa kamati ya vocha za pembejeo ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika kikao cha kamati ya vocha za pembejeo mkoa wa Iringa kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.   

Dk. Ishengoma amesema “ili kuhakikisha usimamiaji wa vocha hizo za pembejeo unakuwa madhubuti, ni lazima wakuu wa Wilaya kusimamia vizuri mchakato mzima wa vocha katika wilaya zenu”. Aidha, amewataka Wakuu hao wa Wilaya kutokuwafumbia macho mawakala wasio na vigezo ili huduma hiyo iweze kufanikiwa na kuwanufaisha wananchi kama yalivyo madhumuni ya Serikali.

Amesema “mfumo huu wa vocha ni mzuri sana ila una mianya ya rushwa hivyo tusichague mawakala matapeli bali  tuchague mawalaka wenye rekodi nzuri na wasio na madeni na wasio wababaishaji kwa sababu lengo la serikali ni kumsaidia mkulima kwa kumpunguzia gharama katika pembejeo za kilimo” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa aliagiza kamati ya vocha ya Wilaya na Wataalam wa kilimo kuwaelimisha wakulima juu ya utaratibu wa awali wa kufikisha pembejeo kwa wakulima kulingana na fomu zalizowasilishwa ma Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Akiwasilisha mapendekezo ya mgao wa vocha za pembejeo za kilimo kwa kila Halmashauri kwa msimu wa mwaka 2011/2012 katika kamati ya vocha ya Mkoa wa Iringa, Afisa Kilimo Mkuu katika Ofisi ya Mkuu Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni ameyataja mapendekezo hayo kwa kila Halmashauri kuwa ni Mufindi (kupandia 44,300, kukuzia 44,300, chotara 44,000, mpunga 300), Makete (kupandia 23,700, kukuzia 23,700, chotara 23,700), Iringa (kupandia 45,000, kukuzia 45,000, chotara 43,500, mpunga 2,500), Njombe Mji (kupandia 21,000, kukuzia 21,000, chotara 21,000), Manispaa (kupandia 4,000, kukuzia 4,000, chotara 4,000), Kilolo (kupandia 26,000, kukuzia 26,000, chotara 25,800, mpunga 200), Njombe (kupandia 42,500, kukuzia 42,500, chotara 42,500) na Ludewa (kupandia 24,500, kukuzia 24,500, chotara 24,000 na mpunga 500).

Akiongelea thamani za vocha moja moja msimu katika msimu wa mwaka 2011/ 2012  Nyoni amesema kuwa vocha za kupandia kilo 50 ni shilingi 28,000, kukuzia kilo 50 ni shilingi 18,500, mahindi chotara kilo 50 ni shilingi 20,000 na mpunga kilo 50 ni shilingi 12,000.

Nyoni amesema kuwa Mkoa unatarajia kupata mgao wa jumla ya vocha 693,000 za pembejeo za kilimo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

VIJANA PUNGUZENI KASI YA VVU/ UKIMWI


VIJANA mkoani Iringa wametakiwa kuwa wajumbe makini katika kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kujilinda kwa kutumia mafundisho ya MUNGU kama silaha kubwa katika kujilinda na ugonjwa huo.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akifunga semina ya siku mbili ya vijana iliyoandaliwa na Kanisa Katoliki Parokia ya Kihesa katika manispaa ya Iringa.

Dk. Ishengoma amesema “mkoa wetu sasa unaongoza kwa maambukizi ya UKIMWI ukiwa na kiasi cha asilimia 15.7 ya maambukizi”. “Naomba kila mmoja wetu awe mjumbe katika kupunguza kasi ya maambukizi haya”. Amesema kwa kufanya hivyo kiasi cha maambukizi kitapungua sana. Aidha, amewasisitiza vijana kujilinda kwa kufuata mafundisho ya Mungu kama silaha kubwa katika kujilinda huko. Akikariri Kitabu cha Waefeso 6:11 “vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani”.

Vilevile, amewaasa vijana wote kujenga tabia ya kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali kwa malengo ya kuimarisha afya zao, uwezo wa kufikiri na kujipatia ajira.

Amewaomba walimu na viongozi wa dini kuhakikisha vijana wanafanikiwa. Amesema “walimu wa mafundisho ya dini ni nguzo muhimu katika kuhakikisha vijana wanafanikiwa, nawaomba walimu wote na viongozi mbalimbali wa taasisi za dini tutumie nguvu zetu zote kuwapa elimu vijana wetu” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Ameshauri kuwa vijana ni taifa linalotegemewa hivyo kwa kutumia karama ya ualimu. Ni vizuri wakatumia tunu hiyo kuufikisha ujumbe wa Mungu kwa vijana na waumini wote. Ameshauri kuendelea kuwafundisha maadili mema ili wafanikiwe katika maisha. Amesema kuwa wapo vijana wakorofi ambao huchangia pia kuharibu nidhamu ya vijana wengine hao wanahitaji mtumie bisara na utu zaidi ili warudi katika nidhamu inayotakiwa.

Akiongelea suala la anami iliyopo nchini, Dk. Ishengoma amesema  “niwakumbushe suala la amani iliyopo nchini kwa sasa”. Watanzania siku zote tunaishi kwa amani na mshikamano mkubwa. Amesema “hivi vyote vimejengwa na waasisi wetu ambao walituunganisha tukawa kitu kimoja”. Amesisitiza kuwa wote kwa pamoja kuimarisha na kudumisha zaidi mshikamano na amani iliyopo ili watanzania waendelee kuishi kwa utulivu na upendo.

Katika mmomonyoko wa maadili, Dk. Ishengoma amesema “katika jamii yetu wote tumeshuhudia mmomonyoko wa maadili, tumeshuhudia vijana wakilewa, wakikosa hekima na busara, dharau, vijana kuvuta na kusafirisha dawa za kulevya”. Amesema mmomonyoko huu unatokana na kutofuata mafundisho ya Mungu. Aidha, aliuomba uongozi wa kanisa kusaidia kwa kadri iwezekanavyo kuwafundisha maadili mema vijana na waumini wao kwa ujumla.

Kanisa Katoliki Parokia ya Kihesa kupitia umoja wa vijana umeandaa semina kwa vijana kwa lengo la kuwaimarisha kimwili na kiroho pamoja na kuwapokea vijana waliohitimu shule ya msingi na kujiunga na umoja huo ili kuweza kuepukana na majanga mbalimbali yanayowakumba vijana kulingana na hali halisi ya utandawazi.


Monday, October 24, 2011

IKAMA YA WATUMISHI 662 IRINGA


MKOA wa Iringa umeidhinishiwa IKAMA ya watumishi 662 katika mwaka wa fedha 2011/ 2012 katika kutekeleza majukumu yake.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Sehemu ya Utumishi na Utawala kwa mwezi Julai hadi Septemba 2011/ 2012 katika kikao cha kudhibiti Mapato na Matumizi ya serikali katika ofisi yake, kwa niaba ya Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Afisa Tawala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Neema Mwaipopo amesema kuwa “kwa kipindi cha Julai- Septemba 2011/ 2012 Sekretarieti ya Mkoa ilipokea IKAMA iliyoidhinishwa mikoa ya Iringa na Njombe”.

Amesema Mkoa wa umeidhinishiwa kuwa na watumishi 662. Amesema kuwa watumishi waliopo ni 578 na nafasi wazi kuwa 84 na kati ya hizo ajira mbadala ni 48 na ajira mpya ni 36.

 Neema Mwaipopo, Afisa Tawala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa

Amesema kuwa mkoa wa Njombe umeidhinishiwa kuwa na watumishi 423 kati ya 71 waliopo na nafasi wazi 352. Amesema kati ya hizo ajira mbadala ni 10 na ajira mpya ni 342. Aidha, amesema kuwa maombi ya kujaza nafasi wazi 378 katika Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa na Njombe na maombi ya kibali cha ajira mbadala 58 yamewasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Akiongelea mafunzo kwa watumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mwaipopo amesema katka kipindi hicho watumishi wanne wameanza kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu katika chuo kikuu cha Tumaini na chuo cha Uhasibu (TIA). Amesema kuwa madhumuni ya mafunzo hayo ni kuimarisha utendaji kazi na ufanisi katika kazi kwa mujibu wa mpango wa mafunzo wa mkoa.

Akifunga kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) amewataka wafanyakazi katika Ofisi yake kufanya kazi kwa umakini mkubwa na uwajibikaji ili kuleta tija katika mkoa na taifa kwa ujumla. Aidha, amewataka kila mtumishi kurejea kipengele kinachomhusu katika Ilani ya uchaguzi ya chama kinachotawala na kuweka utaratibu wa utekelezaji wake.

Kikao cha kudhibiti mapato na Matumizi hufanyika kila baada ya miezi mitatu na hujadili pamoja na mambo mengine mapato na matumizi ya fedha za serikali.

RC AAGIZA MATUMIZI MAZURI YA FEDHA ZA SERIKALI

MKUU wa Mkoa wa Iringa ameagiza matumizi mazuri ya fedha za serikali kadri zilivyopangwa ili ziweze kuwanufaisha wananchi walio wengi katika jitihada za kuondoa umasikini na kuinua maisha ya kila siku.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) katika kikao cha robo ya kwanza cha kudhibiti Mapato na Matumizi ya serikali katika ofisi yake kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake. 

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. christine Ishengoma (Mb.)

Dk. Ishengoma aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho amesema “lazima fedha za serikali zitumike vizuri kadri zilivyopangwa hasa upande wa miradi ya maendeleo ili ziwanufaishe wananchi wengi”.
Amesisitiza kufuatwa kanuni na taratibu za kihasibu ikiwa ni pamoja na ulipwaji wa madai mbalimbali kwa muda ili kuongeza ufanisi wa kazi na hatimae mkoa kupata hati safi ya kiukaguzi.

Aidha, Mkuu wa Mkoa ameagiza kufanyiwa kazi mapungufu yote yaliyobainishwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mthibiti mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2009/ 2010 mapema na kuwasilisha taarifa hiyo sehemu husika na kuhakikisha mapungufu hayo hayajitokezi kwa mara nyingine. 

Akiwasilisha taarifa ya Mkaguzi wa Nje kuhusu mapungufu yaliyojitokeza katika ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010 kwa mkoa wa Iringa, Mkaguzi Mkazi, Ismail Mbiru amesema kuwa ripoti hiyo imebaini mapungufu kadhaa yaliyoainishwa kwa kila Halmashauri kwa ajili ya kuyatolea majibu sahihi ili kuleta ufanisi katika kusimamia mapato ya Halmashauri.
Mbiru ameyataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa zenye mapungufu makubwa, taarifa zenye nyaraka pungufu, taarifa za halmashauri ambazo fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo hazijatumika na kuwasilisha taarifa zenye hati zenye shaka.

Mapungufu mengine ameyataja kuwa ni kuwasilisha taarifa yenye wadaiwa wasiolipa na wasiolipwa, kuwasilisha taarifa zenye mishahara isiyolipwa na haikurejeshwa Hazina na kuwasilisha taarifa ya vitabu vya maduhuli ambayo hayajarejeshwa na mawakala wa kukusanya mapato.

Wednesday, October 19, 2011

WELLINGTON HARRISON TURNER GONDWE-Jr


Wellington Harrison Turner Gondwe, alizaliwa tarehe 11 Oktoba, 1987 mjini Morogoro.

Alibatizwa mwaka 1990 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Usharika wa Bugando na alipata Kipaimara mwaka 2001 katika Usharika huohuo.

Alijiunga na shule ya msingi Mlimani mwaka 1994 na kuhitimu darasa la Saba katika Shule ya Msingi ya Lake mwaka 2002.
Aidha, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Murutunguru iliyopo Wilayani Ukerewe mwaka 2003 hadi Juni, 2004.

Baada ya hapo alihamia katika Shule ya Sekondari ya Thaqaafa Julai, 2004- 2006. Kutokana na ugonjwa hakuweza kufanya mitihani yake ya kidato cha Nne iliyotarajiwa kuanza 22 Oktoba, 2006.

Wellington alianza kuugua Malaria kali tarehe 3 Oktoba, 2006. Aidha, alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando tarehe 10 Oktoba, 2006.

Pamoja na jitihada za Madaktari za kunusuru maisha yake kushindikana na roho kushindana na mauti, alifariki tarehe 20 Oktoba, 2006 saa 12 kamili jioni.

BWANA alitoa na BWANA ametwaa jina lake lihimidiwe.


WATUMISHI WA UMMA NA HUDUMA BORA


Watumishi wa Umma wamekumbushwa kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii na kuhakikisha jamii inaridhika na huduma hiyo pamoja na changamoto zilizopo.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. George Masaju (kulia) akiongea na wafanyakazi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa hawapo pichani na Kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bw. Aseri Msangi (kushoto)
Masaju amesema “tunatambua kuwa sisi ni watumishi wa Umma na tuna maadili yetu ya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 na mabadiliko yake Na. 17 ya mwaka 2007”. Amesema kwa msingi huo wa utumishi wetu wa Umma “sote kwa pamoja lazima huduma zetu tuzitoe kwa ubora na kwa viwango vya kuridhisha kwa Umma”.
Amesema “nawajibika kuwakumbusha wajibu wetu sote kwa Serikali na tukumbuke kuwa sisi ndio watendaji wa kuwasaidia viongozi wetu wa juu”.
Aidha, amewakumbusha kuwa wafanyakazi katika ngazi za mikoa na Halmashauri ndio walio karibu zaidi na wananchi hivyo wanawajibika kufanya kazi kwa uwezo wao na viwango kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema utoaji wa huduma bora kwa wananchi unasaidia katika kuondoa kero na kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya Serikali yao.
Akisisitiza dhana ya ubora wa huduma kwa wananchi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa ubora huo ujikite katika utoaji wa maamuzi sahihi na yanayotolewa katika muda muafaka.
Ametolea mfano wa huduma zikitolewa vizuri katika idara ya polisi na mahakama kutasaidia kupunguza uhalifu.
Vilevile, amesisitiza kuwa jukumu la kudhibiti uhalifu nchini si la idara ya polisi na mahakama pekee bali ni jukumu linalohitaji msukumo wa pamoja baina ya mamlaka zinazohusika na wananchi kwa umoja wao.

Sunday, October 9, 2011

KKKT DAYOSISI YA KUSINI KUJENGA CHUO KIKUU

Askofu mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kusini Njombe ameazimia kuanzisha ujenzi wa chuo kikuu cha dayosisi katika ukanda wa kusini ili kuendeleza na juhudi za kanisa katika kuiletea jamii ustawi.
Kauli hiyo imetolewa na Askofu mteule Isaya Japhet Mengele baada ya kusimikwa kazini na Mkuu wa KKKT nchini Askofu. Dk. Alex Malasusa katika kanisa kuu, Dayosisi ya Kusini-Njombe.
Akiongelea mipango yake ya baadae Askofu Mengele amesema ni ujenzi wa chuo kikuu cha dayosisi katika ukanda huo wa kusini ili kuwanufaisha wananchi wengi katika sekta ya elimu.
Aidha, akiongelea dhana ya kilimo kwanza, Askofu. Mengele ameipongeza serikali kwa hatua hiyo na kuishauri kuwa kilimo kwanza ili kitoe matokeo mazuri kifanyike kwa kanda kutokana na mazao yanayozalishwa katika kanda husika ili kuongeza chachu na kuinua kilimo ili kiwanufaishe wananchi wengi zaidi.
Akiongelea sekta ya elimu amesema ataendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha utoaji wa elimu nchini. Aidha, ameishauri Serikali huongeza kasi katika kuifanya hospitali teule ya Ilembula kuwa hospitali ya rufaa ikiwa ni pamoja na kuisaidia gari la kubebea wagonjwa ili kuwasaidia wananchi wengi.
Katika salamu za Mkoa wa Iringa, zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amempongeza Askofu mteule Mengele kwa uteuzi wake. Aidha, amewaomba viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wao kukaa chini na kutafakari juu ya nchi na kuiombea ili iendelee kuwa na amani, upendo na utulivu.
Vilevile, Dk. Ishengoma imelishukuru kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania kwa michango na ushiriki wake katika kuiletea maendeleo jamii. Ameitaja michango hiyo kuwa ni pamoja na kuijenga jamii katika maadili na kuwafanya wananchi wake kuwa raia wema, mingine ni elimu na afya. 
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika aliyemuwakilisha Waziri Mkuu aliyepo safarini nchini Brazili amewataka viongozi wa dini kukemea maovu, na kuwataka waumini kufuata mfundisho ya dini na kujitolea kulijenga kanisa lao na nchi yao.

RASILIMALI ZA NCHI ZIWANUFAISHE WANANCHI

Serikali imeshauriwa kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kwa maslahi ya nchi na kuwanufaisha wananchi wenyewe walio wengi.
Ushauri huo umetolewa na Askofu mteule wa Dayosisi ya Kusini- Njombe, Askofu. Isaya Japhet Mengele katika ibada ya kumsimika na kumuingiza kazini msaidizi wa Askofu, Mch. Dk. George Mark Fihavango iliyoongozwa na Mkuu wa KKKT nchini Askofu. Dk. Alex Malasusa iliyofanyika katika kanisa kuu, Dayosisi ya Kusini Njombe.
Askofu. Mengele amesema kuwa rasilimali za nchi zinapogawanywa kwa maslahi ya nchi na wanufaikaji wakawa ni wananchi, nchi hutawaliwa kwa amani na utulivu. Aidha, ameshauri pia migodi itakayoanzishwa katika ukanda wa kusini mwa nchi, uanzishwaji, uratibu na usimamizi wake lazima uwe mzuri ili kuepusha migogoro inayoshuhudiwa katika ukanda wa kaskazini mwa nchi.
Akiongelea uhifadhi wa mazingira, amesema kuwa ni muhimu kwa Serikali na wadau wengine wote wa maendeleo na wenye mapenzi mema na nchi hii kutilia mkazo dhana ya uhifadhi wa mazingira ili kuinusuru nchi na uharibifu unaotokana na uharibifu wa mazingira ili nchi iwe mahali salama kwa ustawi wa binadamu wake.
Askofu mteule Mengele ameipongeza Serikali katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na kusifu Serikali kutojiingiza katika masuala la kidini hali inayochangia ukuaji na ustawi wa uhuru wa kuabudu unaoendana na misingi ya kidemokrasia nchini.
Akimsimika rasmi, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Askofu. Dk. Alex Malasusa amewataka viongozi wa dini kutokutumia nafasi zao kwa maslahi ya kisiasa.
Katika salamu za Mkoa wa Iringa, zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amempongeza Askofu mteule Mengele kwa uteuzi wake. Aidha, amewaomba viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wao kukaa chini na kutafakari juu ya nchi na kuiombea ili iendelee kuwa na amani, upendo na utulivu.
Vilevile, Dk. Ishengoma imelishukuru kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania kwa michango na ushiriki wake katika kuiletea maendeleo jamii. Ameitaja michango hiyo kuwa ni pamoja na kuijenga jamii katika maadili na kuwafanya wananchi wake kuwa raia wema, mingine ni elimu na afya. 

Saturday, October 8, 2011

MKUU WA MKOA WA IRINGA AONGEA NA WAZEE NA VIONGOZI WA DINI IRINGA

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amewaomba wazee wa Mkoa wa Iringa kumpatia ushirikiano wa kutosha katika jukumu lake la kuuongoza Mkoa huo kwa pamoja waweze kuuletea maendeleo.
Dkt, Ishengoma ameyasema hayo alipoongea na wazee wa Iringa alipokutana nao katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (kulia) akiongea na wazee wa Mkoa wa Iringa, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Aseri Msangi
Dkt. Ishengoma amesema kuwa wazee ni hazina kubwa katika Mkoa hivyo ushirikiano wao ni muhumu sana katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo. Amesema “ninaamini kuwa wazee ni chachu ya kuleta maendeleo kwa sababu mumefanya kazi kwa muda mrefu na kukutana na changamoto na mambo mengi katika Mkoa wetu wa Iringa”.
Mkuu huyo wa Mkoa amewafahamisha wazee hao kuwa Ofisi yake ipo wazi muda wote kwa ajili ya kupokea ushauri, kushauri na kushauriana katika mambo ya kuuendeleza Mkoa wa Iringa.
Aidha, amechukua fursa hiyo kuwafahamisha wazee hao kuwa Mkoa unatarajia kuadhimisha maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru tarehe 7 hadi 9 Novemba, 2011 itakayoenda sambamba na kukimbiza Mwenge wa Uhuru Mkoani Iringa. Amesema mwaka huu tofayuti na miaka mingine Mwenge wa Uhuru hautakimbizwa Mkoa mzima bali utakimbizwa katika makao makuu ya Mkoa na Iringa utakesha katika uwanja wa Samora.
Wakati huohuo Mkuu huyo wa Mkoa wa Iringa amekutana na viongozi wa madhehebu ya dini ya Iringa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa majira ya mchana.
Dkt. Ishengoma amesema “viongozi wa dini ndio mliowashika watu hivyo tukishirikiana kwa pamoja mambo yanayohusu maendeleo yatafikiwa haraka”. Amesema kuwa ushirikiano huo baina ya Serikali na madhuhebu ya dini utasaidia hata malezi ya vijana kwa sababu vijana wengi wanaokengeuka wanatoka katika madhehebu ya dini yanayoongozwa na viongozi hao.
Wazee wa Mkoa wa Iringa wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Iringa (hayupo pichani) 
Askofu wa Kanisa la Aglikana Dayosisi ya Ruaha, Bw Joseph Mgomi amesema kuwa Dayosisi yake imekuwa ikifanya kazi nyingi za kijamii kwa kushirikiana na Serikali ili kumletea maendeleo mwananchi wa Iringa na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali. Amesema miongoni mwa shughuli hizo kuwa ni miradi ya maji na kilimo.  

MUFINDI WASHAURIWA KUANZISHA CHUO KIKUU

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewashauri wanamufindi kuangalia uwezekano wa kuwa na chuo kikuu ili kuwasogezea karibu huduma hiyo muhimu wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na watumishi wa Serikali kuu, Halmashauri na taasisi mbalimbali katika ukumbi mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Karibu Wilayani Mufindi, Mhe. Mkuu wa Mkoa
Dkt. Ishengoma amesema “pamoja na kuwa na mafanikio makubwa katika nyanja za uzalishaji na uchumi, Mufindi tufikirie kuwa na chuo kikuu”. Amesema kuwa chuo kikuu ni muhimu sana katika kuzalisha wanataaluma watakaosaidia kusukuma zaidi gurudumu la maendeleo Wilayani hapo. Amesema uanzishwaji wa chuo kikuu Wilayani Mufindi utawasaidia wananchi wengina wa maeneo ya jirani kuvutika katika kujiendeleza kielimu.
Akiongelea sekta ya maji, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa sekta hiyo bado inaasilima zilizo chini jambo linalowakoshesha wananchi wengi huduma hiyo. Amesema “kwa pamoja ni lazima tujitahidi ili kuongeza kasi ili tufikie malengo ya matakwa ya sera ya maji”.
Aidha, ameishauri Halmashauri hiyo kuangalia vyanzo vingine vinavyoweza kuiletea mapato ili kuiwezesha Halmashauri hiyo kujiendesha vizuri zaidi. Amesema kuwa Halmashauri inapojiimarisha kimapato inapanua wigo wake wa utoaji huduma kwa wananchi na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Mufindi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista Kalalu amesema kuwa ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400, wilaya yake imeongeza miradi ya maji na kuongeza idadi ya watu wenye uwezo wa kupata maji safi na salama kutoka asilimia 40 mwaka 2005/2006 kwa wakazi wa mjini, hadi asilimia 53 mwaka 2010/2011. Aidha, idadi imeongezeka kutoka asilimia 56 mwaka 2005/2006 kwa wakazi wa vijijini, hadi asilimia 61 mwaka 2010/2011.


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista kalalu akisisitiza jambo

Amesema kuwa miradi hiyo ni ya uchimbaji wa visima 35 ambavyo vimewapatia maji wananchi wapatao 8,750 pamoja na ujenzi wa mtego mmoja wa maji ambao unawanufaisha wananchi 2000.
Bibi. Kalalu amesema kuwa uhifadhi wa vyanzo vya maji na rasilimali za maji umeongezeka kutoka vyanzo 100 vilivyokuwa vimehifadhiwa mwaka 2005 hadi kufikia vyanzo 705 mwaka 2010.  Amesema vyanzo hivyo ni vile ambavyo hutiririsha maji yake katika mto wa Ruaha.

Friday, October 7, 2011

TUMIENI SKIMU YA MWAGILIAJI -RUAHA MBUYUNI



Wananchi wa Kata ya Ruaha Mbuyuni wametakiwa kuitumia skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni kwa shughuli za kilimo ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi.

Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za kilimo katika skimu hiyo ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni iliyopo katika kata ya Ruaha Mbuyuni.

Dkt. Ishengoma amesema “Ruaha Mbuyuni mnalo bonde zuri sana ila halitumiki ipasavyo kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji, lazima hali za wanaruaha mbuyuni zibadilike kutokana nakuinuka baada ya serikali yenu kuwatengenezea mrefeji na banio la maji”. Amesema baada ya kulitembelea bonde hilo na skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni ni dhahili kuwa shuguli za kilimo bado kipo chini sana na kushauri hamasa itolewe kwa wananchi kuitumia skimu hiyo kwa kilimo cha kisasa ili waweze kuvuna zaidi ya mara moja.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji wa kijiji cha Ruaha Mbuyuni Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Nassoro Almasi amesema kuwa mwezi Aprili mwaka 2008 mto Lukosi ulihama katika mkondo wake wa asili na kuacha miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo banio kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha ukanda wa juu wa Wilaya ya Kilolo. 

Amesema kuwa madhara ya mvua hizo yalisababisha ekari 500 za mazao ya chakula ambayo ni mahindi, mpunga, maharage, vitunguu, nyanya na mbogamboga kuathirika kwa ukame na kusimamisha shughuli za kilimo.

Skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni ilianza miaka ya sabini baada ya wakulima wenyewe kuchepusha maji kwa kutumia mawe, magogo, matete na majani ili kumwagilia mashamba yao.