Monday, August 13, 2012





 

HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA GERTRUDE K. MPAKA WAKATI WA KUFUNGA MAFUNZO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI MWAKA 2012 KWA WAANDISHI WA HABARI WA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI PAMOJA NA MIKOA YA LINDI NA MTWARA YALIYOFANYIKA CHUO KIKUU RUAHA IRINGA,  TAREHE 13 AGOSTI, 2012


Ndugu Mwenyekiti,
Mratibu wa Mratibu wa Sensa Mkoa,
Watendaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Watendaji kutoka Sekretarieti ya Mkoa,
Ndugu Washiriki wa Mafunzo,
Mabibi na Mabwana,


Ndugu Mwenyekiti,kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa na kuhudhuria mafunzo haya hadi kufikia hatua ya mwisho yaani hatua ya kumaliza.  Aidha nachukua fursa hii kuwashukuru sana washiriki wote kwa kuheshimu mwaliko wa kuhudhuria mafunzo haya muhimu ambayo yalihusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na nafasi ya vyombo vya habari katika kufanikisha zoezi hilo.

Ndugu Mwenyekiti, nilipopata mwaliko kuwa Mgeni Rasmi kufunga mafunzo haya kwanza nilifurahi kwa kuwa niliona nimepata fursa ya pekee kukutana na kundi kubwa la waandishi wa habari kwa pamoja kitu ambacho ni nadra kutokea katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku. Pili nimefarijika na mwaliko wenu kwa kuwa utanipa fursa ya kuchangia mawazo katika baadhi ya maeneo ambayo yamezungumziwa katika mafunzo haya.

Ndugu Mwenyekiti, mafunzo haya nimeelezwa kuwa yamezungumzia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi iliyopangwa kufanyika tarehe 26 Agosti, 2012. Nimeelezwa kuwa jumla ya mada tano ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa kina ambapo pia washiriki walipata fursa ya kufanya mazoezi kwa vitendo kwa baadhi ya mada walizojifunza.

Kwa ujumla nimeelezwa kuwa mada zote ziliibua majadiliano na hoja mbali mbali pamoja na changamoto za hapa na pale lakini jambo muhimu ni kuwa lengo la majadiliano hayo yalilenga katika kujifunza zaidi na kuongeza ufahamu kwa kila mshiriki juu ya masuala ya msingi kuhusu Sensa. Mimi naamini kuwa wataalamu wetu hapa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu wamejitahidi kadri ya utaalamu wao na uwezo waliojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuyafafanua kinagaubaga masuala yote yanayohusu Sensa ambayo yalihitaji maelezo ya ziada ya yale yaliyowasilishwa. Mbali ya maelezo ya wataalamu nimeelezwa kuwa mmepatiwa nyaraka muhimu zenye kueleza na kufafanua masuala ya msingi ya Sensa. Nyaraka hizo zitawasaidia kuongeza ufahamu wenu kuhusu suala zima la Sensa.

Ndugu Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo ninaamini kuwa ndugu washiriki mmefaidika na maelezo hayo na sasa mmekamilika katika suala zima linalohusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Maana yake ni kuwa sio tu mko katika nafasi nzuri ya kuandika na kutangaza kwa usahihi habari za Sensa lakini pia mafunzo haya yatakuwa yamewatia shime na ari ya kushiriki katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012. Matarajio yetu basi ni kuona taarifa zaidi za Sensa hasa zile za kuhamasisha wananchi kushiriki zinatolewa mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini na hususan vyombo vyetu vilivyomo katika mikoa ya kanda yetu.

Ndugu Mwenyekiti, nafasi niliyopewa ni kuyafunga mafunzo haya lakini kabla ya kufanya hivyo ningependa kusisitiza mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la ushirikiano. Waswahili tuna msemo usemao ‘kidole kimoja hakivunji chawa’. Kama ilivyoelezwa na wataalamu, mafanikio ya Sensa yanategemea sana ushiriki na ushirikishwaji wa kila mdau katika nchi. Kwa maana hiyo ni ukweli usiopingika kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikisha Sensa kwa sababu mchakato wake ni mkubwa unaohitaji ushiriki wa wadau wa kila aina na kutoka sekta mbalimbali. Miongoni mwa wadau hao ni vyombo vya habari.

Hivi sasa nchi yetu inajivunia utajiri mkubwa wa vyombo vya habari ambavyo ni matokeo ya mabadiliko ya sheria ya umiliki wa vyombo habari iliyopitishwa na Serikali. Dhamira ya Serikali kufanya marekebisho hayo ni kuwapa fursa zaidi watanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa kuamini kuwa vyombo hivi vitatumika kuwaendeleza wananchi kwa kuwaelimisha, kuwahabarisha na kuwaburudisha.

Historia ya nchi yetu inaonyesha kuwa vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Serikali sio tu katika kuboresha hali ya maisha ya kila mwananchi bali pia katika kuimarisha uzalendo na mshikamano miongoni mwa wananchi. Hivyo, wito wa Serikali kwa vyombo vya habari ni kuviomba viendeleze ushirikiano na mshikamano wa watanzania kama vinavyovyofanya katika masuala mengine yenye maslahi na Taifa letu ili kufanikisha Sensa.   

Ndugu Mwenyekiti, naelewa kuwa Serikali haina shaka hata kidogo kuhusu uwezo wa vyombo vya habari katika kulieleza jambo hili kwa usahihi kwani mnalifahamu na kwa mafunzo na uzoefu mlionao nyinyi ni walimu na wasemaji wazuri hivyo tumieni ujuzi na uwezo wenu huo kuwaeleza wananchi kwa ufasaha kuwa Sensa ni muhimu kwao na kwa Taifa lao hivyo wasisite kushiriki. Kwa hiyo, matarajio ya Serikali ni kuona kuwa mnakuwa waelimishaji wazuri na wahamasishaji makini wa Sensa ili kila mwananchi kwa hiari yake aone kuwa ana wajibu wa kuhakikisha anahesabiwa na anahesabiwa mara moja tu.

Ndugu Mweneykiti,
Jambo la pili ni suala la kutoa taarifa sahihi na kwa wakati. Leo zimebaki siku 12 tu kufika siku ya Sensa tarehe 26 Agosti 2012. Hivyo vyombo vya habari na wasemaji wote wa Sensa hawana budi kuepuka kufanya makosa katika uhamasishaji na zaidi walenge katika mambo muhimu ambayo mwananchi anapaswa kuyafahamu. Mambo hayo aliyaeleza Mkuu wa Mkoa wakati alipofungua mafunzo haya nami sina budi kuyarudia ili kuweka msisitizo.

1.0      Kuwa Sensa ya Watu na Makazi itafanyika tarehe 26 Agosti, 2012.
2.0      Watakaohesabiwa ni wale tu watakaokuwa nchini usiku wa Jumamosi tarehe 25 Agosti kuamkia Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012.
3.0      Watakaohesabiwa katika Kaya ni wale watakaokuwa wamelala katika Kaya usiku wa kuamkia Siku ya Sensa ambao, kama nilivyoeleza awali, ni usiku wa Jumamosi ya tarehe 25 Agosti, 2012 kuamkia Jumapili terehe 26 Agosti, 2012 pamoja na wanakaya wanaofanya kazi za usiku ambao kwa usiku ule hawakulala kwenye Kaya.  Hawa ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya, ulinzi na usalama na hata sekta ya habari.
4.0      Ni muhimu Mkuu wa Kaya akaweka kumbukumbu sahihi za watu wake wote zikiwemo za umri,kiwango cha elimu, ajira anayofanya, mahali anaposhinda mwanakaya wakati wa mchana na kwa wanawake hali zao za uzazi.

Ndugu Mwenyekiti, mwisho, ningependa kueleza furaha yangu kwa washiriki wote kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa na uvumilivu wakati wote wa mafunzo. Ushirikiano na uvumilivu wenu huo ulikuwa muhimu katika kufanikisha mafunzo haya hadi sasa tunayafunga rasmi. Nichukue fursa hii kuwatakia safari njema wageni wetu wote kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na wenzetu kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara.

Baada ya kusema hayo naomba sasa nitamke kuwa Mafunzo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa waandishi wa habari wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja mikoa ya Lindi na Mtwara yamefungwa rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza
 
SENSA KWA MAENDELEO: JIANDAE KUHESABIWA



Sunday, August 12, 2012

Mratibu Msaidizi wa Sensa Mkoa wa Iringa Conrad Millinga (kulia) na na Mwandishi wa Habari wa gazeti la Mwananchi, Tumaini Msowoya walipowasili katika viwanja vya Ikulu Ndogo Iringa kushiriki FUTARI iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma.

Katibu wa Mkuu wa Mkoa, Bahati Golyama akimuongozi kingozi wa dhehebu la dini ya Orthodox kuingia katika viwanja vya Ikulu Ndogo kwa ajili ya Futuru.

 Waumini wa Dini ya kiislamu waliojumuika pamoja katika swala ya Magharibi wakai wa hafla ya FUTARI iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma.

Wageni waalikwa katika hafla hiyo wakishiriki kupakua FUTARI katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa.

Wageni waalikwa katika hafla hiyo wakishiriki kupakua FUTARI katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa.

Wageni waalikwa katika hafla hiyo wakishiriki kupakua FUTARI katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa.



Wageni waalikwa katika hafla hiyo wakishiriki kupakua FUTARI katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa.

Wageni waalikwa katika hafla hiyo wakishiriki kupakua FUTARI katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa.

Viongozi vijana wakipanga mikakati, Bahati Golyama, Katibu wa RC Iringa (katikati), Gasto Mwambigija Andongwisye, Afisa Utumishi (kulia) na Mathias (kushoto) katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akitoa neno la shukraki kwa waalikwa wa FUTARI.


Baadhi wa waumini walioshiri katika FUTARI hiyo. Mhe. Evarista Kalalu, DC Mufindi (kulia), Bibi. Gertrude Mpaka, RAS Iringa (wa pili kulia)



DKT. ISHENGOMA AFUTURISHA MKOANI IRINGA



Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amewaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi juu ya umuhimu wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika nchi nzima kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012.

Ameyasema hayo katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa alipokuwa akitoa neno la shukrani kwa viongozi wa dini mbalimbali na wageni waalikwa katika futari aliyoiandaa kwa ajili yao kwa ajili ya kutakiana heri katika mfungo mtukufu wa Ramadhani.

Amesema viongozi hao wa madhehebu ya dini wanao wajibu na mchango mkubwa katika kuwahamasisha wananchi washiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa kwa maslahi ya nchi.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa jukumu hilo linakuja kutokana na dhamana waliyonayo ya kuliwakilisha na kuliongoza kundi kubwa la waumini katika jamii. Amesema kutokana na umuhimu huo anawaomba viongozi hao washiriki kikamilifu ili Serikali iweze kupanga sawia mipango ya maendeleo. Amesema kuwa mipango ya maendeleo ili ifanikiwe takwimu za watu zinahitajika sana.

Akiongelea umuhimu wa zoezi hilo amesema kuwa zoezi hilo litaisaidia  Serikali kupanga mipango ikiwa na lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi wake. Amesema kujulikana kwa idadi hiyo ya watu ni muhimu kwa sababu kutaisaidia Serikali kuyatambua makundi mbalimbali ya watu katika jamii na kuwafikishia mahitaji yao maalumu ili waweze kufurahia uhuru wao katika nchi yao.

=30=


SIKU RC ALIPOFUTURISHA IRINGA


 Baadhi ya Waumini wa Dini ya kiislam wakipata swala kabla ya FUTARI iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma


 Baadhi ya Waumini wa Dini ya kiislam wakipakua FUTARI. Picha kwa hisani ya Blog ya Francis Godwin 

 Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka (Picha kwa hisani ya Blog ya Francis Godwin )

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (kushoto) akishiriki katika FUTARI (Picha kwa hisani ya Blog ya Francis Godwin )


 Baadhi ya wageni waalikwa akipata FUTARI

Wageni waalikwa akisikiliza nasaha za Mkuu wa Mkoa (hayupo pichani)







Thursday, August 9, 2012

WILAYA ZATAKIWA KUJIFUNZA KILOLO


Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita ametoa wito kwa wilaya nyingine kuitembelea wilaya yake kwa lengo la kujifunza mikakati inayowawezesha kulima kwa ubora na uhifadhi wa mazingira.
Kauli hiyo ameitoa alipofanya mahojiano na gazeti hili katika banda la Wilaya ya Kilolo lililopo katika uwanja wa Maonesho wa John Mwakangale Uyole, Jijini Mbeya.

Guninita amesema kuwa wilaya yake imegawanyika katika ukanda wa juu unaohusisha tarafa ya Kilolo wenye miinuko na mabonde jambo linalofanya ugumu katika matumizi ya zana bora za kilimo kama powatila na matrekta.

Amesema ukanda wa chini wenye tarafa za Mazombe na Mahenge una maeneo ambayo ni tambarare pamoja na kuwa na ukame maeneo hayo yanafaa kwa matumizi ya zana bora za kilimo yakiwemo matrekta.

Guninita amesema pamoja na changamoto hiyo ya kijiografia na mabadiliko ya tabia nchi, bado wilaya yake inajivunia utaratibu wa wananchi wake wa kutunza mazingira hasa utunzaji wa vyanzo vya maji. Amesema utunzaji huu wa vyanzo vya maji una mchango mkubwa katika shughuli za kilimo jambo linalowawezesha wakulima wa wilaya hiyo kuweza kulima kwa mwaka mzima. Ameyataja mazao yanayolimwa zaidi kuwa ni maharage, njegere, mahindi, mbogamboga, magimbi, muhogo, na viazi mviringo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo amesema kuwa wilaya yake imefanikiwa katika uhifadhi wa mazingira kwa uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wadau wengine kuwekeza katika elimu ya uhifadhi wa mazingira. Amesema katika ziara zake za kutembelea wilaya yake baada ya uteuzi wake mapema mwaka huu, katika kata zote 22 alizotembelea amekuwa akisisitiza utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji. Aidha, wananchi wamehamasishwa kuacha vitendo vya uchomaji moto miti ya asili na misitu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkakati mwingine ameutaja kuwa ni wananchi kuhamasishwa katika ulinzi shirikishi unaohusika katika kulinda misiti na hifadhi ya mazingira. Amesema “katika hili la uhifadhi wa mazingira baada ya kutoa elimu na hamasa wale wote watakaobainika watafikishwa katika mkondo wa sheria. Tumekuwa tukisisitiza sana Sheria ya Uhifadhi wa Mazingira ya mwaka 2004, inayotoa adhabu isiyopungua sh. 2,000,000, kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Akiongelea tuzo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya utunzaji wa Mazingira kwa wilaya yake ya kilolo, Guninita amesema “katika kudhihirisha tabia ya uhifadhi wa mazingira kwa wilaya ya Kilolo, wilaya yetu imekuwa mshindi wa kwanza kitaifa. Kata ya bora ni Bomalang’ombe na taasisi bora imetoka katika wilaya yetu nayo ni gereza la Kihesa Mgagao”.

Amesema tuzo hiyo ya Rais, imeendelea kuamsha ari kwa wilaya yake, kuendelea kuhamasisha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira. Ameitaja kampuni ya New Forest kuwa nayo inachangia kutoa hamasa kwa wananchi ya kupanda miti kwa wingi na kujiongezea kupato.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa katika kuhakikisha mkulima wa Kilolo anaendelea kuwa na lishe nzuri, wilaya yake imeendelea kuhamasisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Amesema katika kuhakikisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa unashika kasi, wananchi wamehamasishwa kuzitumia rasilimali walizonazo kufuga kisasa na ufugaji wenye tija. Amesema ufugaji wa kisasa na wenye tija ni ule wa ng’ombe wachache ambao mfugaji anaweza kuwahudumia vizuri na kuepuka mfugaji kuwa mtumwa kwa ngo’mbe wake.

Amesema Halmashauri yake kupitia DADPs imekuwa ikifanya vizuri katika hilo na ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma imeamsha ari zaidi ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani hapo.
=30=

KILIMO HAI KIPEWE MSISITIZO ZAIDI



Wakulima wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wameshauriwa kutumia kilimo hai katika kujihakikishia uhai wa mazingira na usalama wa chakula kwa kukuza kipato na kupunguza gharama za uwekezaji katika kilimo.

Ushauri huo umetolewa na Lawrence Mgora, mkulima mwezeshaji wa kilimo hai kutoka taasisi ya uenezi wa elimu ya ugani na kilimo hai.

Akiongelea maana ya kilimo hai amesema kuwa ni kilimo kinachoangalia uhai wa mazingira, uhakika na usalama wa mlaji na usalama wa chakula jambo ambalo linamuhakikishia mkulima kipato kwa kutumia fursa alizonazo mkulima.

Mgora amesema kuwa ili kilimo kiwe kilimo hai ni lazima ulimaji wake ufuate kanuni za kilimo hicho. Amezitaja kanuni hizo kuwa ni pamoja na matumizi ya mbolea ya asili kama mchuzi wa mmea, uji wa mmea na lishe ya mmea katika uzalishaji wa mazao kwa kupandia na kukuzia. Kanuni nyingine amezitaja kuwa ni dawa za asili katika kudhibiti mmea shambani na katika hifadhi ya mazao pamoja na tiba asilia kwa mifugo wa aina yote. 

Akiongelea kwa mifano hai mafanikio ya kilimo hai kwa mkulima na jamii, Mkulima mwezeshaji huyo ameyataja kuwa ni kuongezeka kwa mapato kwa heka. Amesema kuwa kwa mujibu wa tafiti walizofanya, mavuno ya mahindi yanayopatikana ni magunia 34 kwa heka kwa kutumia kanuni za kilimo hai ukilinganisha na magua 18 kwa kutumia kilimo cha kisasa. Ameongeza kuwa uzito wa mazao nao huongezeka, kwa debe la mahindi lililolimwa kwa kanuni za kilimo hai huwa na uzito wa kilo 22 ukilinganisha na kilo 18 kwa debe la mahindi lililolimwa kisasa. Akiongelea uhufadhi wa mazingira, amesema kuwa kilimo cha kisasa uharibu udongo jambo linalomlazimu mkulima kutumia mbolea mara kwa mara wakati kilimo hai kinahifadhi mazingira.

Akielezea nafasi ya ushirika katika kumsaidia mkulima wa Wilaya ya Kilolo, Afisa Uhirika Wilaya, Biezel Malia, amesema kuwa ushirika katika wilaya ya Kilolo umekuwa unalenga katika kumuwezesha mkulima kupata masoko ya mazao na mitaji kupitia Saccos na taasisi za kifedha. Amesema pia kupitia ushirika wilaya ya Kilolo imeweza kuwahakikishia wakulima upatikanaji wa pembejeo za kilimo na zana za kilimo kama pawatila, matrekta.

Amesema pamoja na juhudi za wilaya kuwawezesha wakulima kupata mikopo kupitia Saccos na taasisi za kifedha, ipo changamoto ambayo wanachama wengi sio waaminifu katika kurejesha marejesho ya mikopo yao. Aidha, amesema kuwa changamoto nyingine ambayo wilaya yake inaifanyia kazi ni uhamasishaji juu ya umuhimu wa kuweka akiba ili kuweza kukopa baadae. Afisa Ushirika huyo amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo ngazi ya wilaya, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 wilaya yake imetenga fedha za kutosha kutoa mafunzo ya kina kwa wakulima na wajasiliamali itakayoenda sambamba na elimu ya mikopo kwa wanachama wa Saccos.

Wilaya ya Kilolo ina aina nne ya vyama vya ushirika, vikiwepo vyama vya ushirika vya mazao (9), vyama vya akiba na mikopo (13), ushirika wa wapiga picha (1) na vyama vya wavuvi (2).
=30=

SERIKALI YABUNI MIKAKATI YA KUKUZA KILIMO



Serikali imeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbli ya kwa lengo la kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na chakula cha kutosha kwa wananchi wake na ziada kwa ajili ya watu wengine.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika kilele cha sikukuu ya wakulima na maonesho ya Nanenane mwaka 2012 yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Maonesho ya kilimo vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
 Mgeni rasmi katika kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dr. Christine Ishengoma alipotembelea banda ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa

Katika hotuba yake, Dkt. Christine amesema “katika jitihada za taifa letu za kujitosheleza kwa chakula, mikakati mbalimbali imeendelea kubuniwa na kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kanda ya Nyanda za Juu Kusini kupewa jukumu la kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi na kuwa ghala la chakula la Taifa kutokana na fursa nzuri za uzalishaji zilizopo hatika mikoa hii”.

Amesema ili jukumu hili la kitaifa lifanikiwe ni lazima wakulima wazalishaji wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutumia vizuri fursa zilizopo, kuzalisha kwa tija kwa kutumia kanuni bora za kilimo zitakazowawezesha kupata ziada ya chakula ya kuuza kwa mikoa mingine isiyokuwa na firsa nzuri za uzalishaji.

Akiongelea viwanzo tija vya uzalishaji wa mazao ya chakula, Dkt. Christine amesema “..viwango vya tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa eneo bado viko chini. Takwimu zinaonesha kuwa, katika Nyanda za Juu Kusini uzalishaji wa mahindi kwa mfano, ni kati ya tani 2-3 kwa hekta moja wakati ambapo utafiti unaonesha kwamba hekta moja inaweza kuzalisha hadi tani 7”.Aidha, ametoa wito kwa viongozi na wakulima kuyatumia maonesho hayo kama jukwaa la kuwajengea uwezo wazalishaji wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuongeza tija na kufikia uwezo wa juu katika uzalishaji kadri inavyowezekana.

Akiongelea ufugaji, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa kanda hiyo ina fursa ya ufugaji kutokana na uwepo wa ardhi, mvua za kutosha, miundombinu ya machinjio ya kisasa na rasilimali kubwa ya mifugo. Amesema mifugo imekuwa ikichangia katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa njia ya nguvu kazi na samadi. Amesema “katika kanda hii, asilimia 70 ya wakulima hutumia wanyamakazi katika shughuli za kilimo. Hii ni hatua kubwa inayostahili kupongezwa kwani matumizi ya nguvukazi ya wanyama ni moja kati ya teknolojia rahisi, sahihi na endelevu kwa wakulima wetu”.

Ikumbukwe kuwa sekta ya kilimo nchini inatoa ajira kwa karibia asilia 80. Vilevile, wakazi karibu asilimia 90 wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanategemea kilimo kama shughuli kuu ya kiuchumi kwa mazao ya chakula na biashara.

=30=

MPAKA AWATAKA MPANDA KUPANDA MITI




 Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka ameshauri upandaji wa miti kwa wingi sana ili kuepukana na tatizo la wilaya hiyo kugeuka jangwa kutokana na matumizi makubwa ya kuni katika kukausha zao la tumbaku linaloendelea kushamiri katika wilaya ya Mpanda mkoa mpya wa Katavi.

Ushauri huo ameutoa alipotembelea banda la wilaya ya Mpanda katika uwanja wa maonesho ya Nanenane wa John Mwakangale- Uyole Mbeya.

Gertrude amesema kuwa kutokana na matumizi makubwa ya kuni zinazotumika katika kukaushia zao la tumbaku, ni vizuri wilaya hiyo ikajipanga katika kupanda miti kwa wingi ili kuziba pengo la miti inayokatwa kwa ajili ya matumizi ya kuni katika kukaushia tumbaku. Amesema kuwa ni vema mkakati huo ukaanza mapema wakati njia mbadala ya nishati ya ukaushaji wa tumbaku ikiangaliwa ili kutokuteketeza misitu na mazao yake.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka alipotembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda 

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, amesema njia za kisayansi zinahitajika katika kukausha majani ya tumbaku pasipo kuharibu mazingira. Aidha, ametoa wito wananchi kufikiria njia ya kiteknolojia itakayotumika katika ukaushaji wa majani hayo. Amesema kwamujibu wa kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane mwaka 2012 isemayo “Kilimo kwanza, zalisha kisayansi na kiteknolojia kukidhi mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu” vivyo hivyo wilaya ya Mpanda ifikirie hamasa ya maendeleo ya kiteknolojia katika kulifanya zao la tumbaku kuwa na tija zaidi katika ustawi wa wananchi na mazingira kwa ujumla wake.

Gertrude amesema kuwa ili kwenda sambamba na kauli mbiu hiyo, ni vizuri wilaya hiyo ikatoa hamasa zaidi katika utengenezaji wa zana zitakazosaidia katika kukipeleka mbele kilimo. Amesema kuwa wapo vijana wengi wanaoibuka na ubunifu wao kwa kutumia teknolojia rahisi wanaohitaji kupewa msukumo na kuendelezwa ili kuweza kuleta mapinduzi katika kilimo na ufugaji.

Akiongelea changamoto inayowakabili wanawake wajasiriamali katika upatikanaji wa masoko, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ametoa wito kwa wanawake wajasiriamali kuungama pamoja na kuunganisha nguvu zao katika shughuli zao za ujasiliamali. Amesema masoko ni changamoto inayowakabili wakina mama wengi wajasiriamali, na kushauri pindi wanapokuwa katika vikundi ni rahisi kwao kuweza kupatiwa mafunzo ya mbinu za upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema umefika wakati kwa wanawake wa Nyanda za Juu kusini kuungana na kutumia fursa iliyopo sasa ya soko pana la Afrika ya Mashariki.
=30=

Sunday, August 5, 2012

WAKULIMA NA WASINDIKAJI WAWEZESHWE ASEMA RC IRINGA



Halmashauri za Wilaya na Manispaa zimeshauriwa kuwasaidia wakulima na wajasiliamali wasindikaji katika kuhakikisha bidhaa zao zinafikia viwango vya ubora vinavyotakiwa ili kujihakikishia soko la uhakika.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipotembelea mabanda ya wajasiliamali na wasindikaji katika maonesho ya Nanenane katika Uwanja wa John Mwakangale -Uyole Mbeya katika siku ya Iringa Day.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. christine Ishengoma (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Fama Food Processing, Genovefa barnabas katika Uwanja wa Maonesho ya NaneNane Mbeya

Dkt. Christine amesema kuwa wakulima wasindikaji wanafanya kazi kubwa sana katika kusindika bidhaa za kilimo kwa kutumia juhudi zao wenyewe, hivyo kujikuta wakikwama katika utaalam na kushauri wawe wanapatiwa mafunzo na ushauri wa kitaalam ili kuufanya usindikaji wao uwe wa kisasa zaidi.

Amesema ni vizuri Halmashauri za Manispaa na Wilaya ziangalie jinsi ya kuwasaidia kitaalam na kiufundi ili bidhaa za usindikaji ziweze kufikia viwango vinavyokubalika na kupata lebo ya shirika la ubora (TBS). “watu wengi sasa wanaangalia lebo ya TBS ili kijihakikishia ubora hivyo ni vizuri mkahakikisha bidhaa zenu zinafikia ubora unaopkubalika na kupata lebo ya ubora” amesisitiza Dkt. Christine.

Akiongelea changamoto zinazowakabili wajasiliamali wasindikaji, mjasiliamali na mmiliki wa Fama Food Processing, Genovefa Barnabas amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wajasiliamali hasa wa Mkoa wa Iringa ni maeneo mahususi ya kuwawezesha kuzalishia bidhaa zao ili ziweze kupata uthibitisho wa ubora unmaotakiwa.  Akifafanua zaidi amesema “ili mjasiliamali anu wajasiliamali tuweze kutimiza ndoto zetu za kufanya shughuli za ujasiliamali vizuri ni vizuri serikali ikatusaidia kutenga maeneo ambayo yatakuwa mahususi kwa shughuli za ujasiliamali ambapo kila kitu kitakuwa kinafanyika hapo”. Amesema “kuanzia mazao na bidhaa zinapoletwa kutoka maeneo mbalimbali zinapokelewa katika eneo hilo, zinaanza kutengenezwa katika eneo hilo, zinapakiwa katika kontena, kufungwa na kuwekwa lebo hapohapo, kwa lugha nyingine mchakato wote unafanyika katika eneo moja hadi kwenda kwa mlaji”.

Akitetea umuhimu wa eneo hilo kwa wajasiliamali, Barnabas amesema kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa kwa sababu kupatikana kwake kutawawezesha kupata cheti cha ubora wa bidhaa toka shirika la viwango (TBS). Amesema kitendo cha kupata lebo ya ubora toka TBS kutawafanya watu wengi zaidi kujiridhisha na ubora wa bidhaa hizo.  

Nunu Mtatifikolo ambaye ni Mwenyekiti kikundi cha Wanawake cha JAFAKU amesema changamoto ya watanzania kukubali bidhaa zinazozalishwa na wajasiliamali wazalendo wa ndani ni mwiba katika ukuaji wao. “amesema ipo kasumba inayoendelea kutudidimiza ya wananchi kupenda bidhaa za nje tofauti na zinazozalishwa na wajasiliamali wa ndani”.

Amesema ili kuondokana na kasumba hiyo elimu inahitajika kutolewa kwa wananchi ili waweze kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. “Elimu hiyo itasaidia sana kubadili kasumba hii na elimu hii inatakiwa kuambatana na matangazo ya bidhaa za wajasiliamali” amesisitiza Mtatifikolo.

Mwenyekiti wa kikundi cha Wanawake wa KKKT-Nduli, Laurencia Malila amesema katika banda la Manispaa ya Iringa amesema kuwa wanawake wajasiliamali Mkoani Iringa wanakabiliwa na changamoto ya masoko kwa maana ya wanunuzi wa bidhaa zao. Amesema “pamoja na kuwa na bidhaa nzuri bado wananchi wanamuitikio mdogo wa kuzinunua jambo linalowafanya washindwe kuzalisha bidhaa kwa wingi”.  

Malila ambaye pia kikundi chake kinajihusisha na kilimo cha kisasa na ufugaji wa nyuki kikiwa na mizinga 47 ya nyuki ya kisasa, ametoa wito kwa watu wanaopenda kujifunza kilimo cha kisasa cha mahindi na maharage pamoja na ufugaji wa nyuki kuwatenbelea ili kujifunza katika mashamba darasa yao yaliyopo katika kata ya Nduli.

=30=

DR. ISHENGOMA ASISITIZA KILIMO CHA KISAYANSI



Zana ya Kilimo Kwanza itafanikiwa kwa wakazi wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini kulima kilimo cha kisayansi na kiteknolojia zaidi na kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara.

Ushauri huo umetolewa katika majumuisho baada ya mgeni rasmi Dkt. Christine Ishengoma kutembelea mabanda ya maonesho ya Nanenane kanda ya nyanda za Juu Kusini katika siku ya mkoa wa Iringa (Iringa Day) iliyofanyika katika uwanja wa maonesho ya Nanenane wa John Mwakangale Uyole Mbeya.

Dkt. Chrisrine ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema “kimsingi kilimo kwanza ni Nyanda za Juu Kusini yaani Mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Rukwa na Katavi kwa kuwa mikoa hii ndio wazalishaji wakubwa nchini, hivyo huwezi kutenganisha Kilimo Kwanza na Nyanda za Juu Kusini”.  Amesema katika kuendeleza kilimo katika ukanda huo ni lazima kilimo kiwe cha kisayansi na kiteknolojia zaidi ili kuwawezesha wakulima kulima maeneo madogo lakini kwa kupata mazao mengi zaidi na yenye ubora unaotakiwa. Amesema kuwa wakulima wameendelea kupata hasara katika kilimo kwa kutokufuata kanuni za kilimo bora jambo linalowafanya waweke nguvu nyingi katika kilimo lakini matokeo wanayoyapata hayaendani na nguvi halisi waliyowekeza katika kilimo hicho. Aidha, ametoa wito kwa wataalam wa kilimo kuwa karibu zaidi na wakulima ili kuwafundisha waweze kuepukana na kilimo cha kizamani na kimazoea.
Hapa huitaji maelezo zaidi ya picha kujieleza yenyewe

Akiongelea kuhama kutoka katika kilimo kidogo kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula, amesema “umefika wakati sasa wa kuhama kutoka katika kilimo cha kawaida na kukifanya kilimo chetu kiwe cha kibiashara. “Na hili litawezekana pale tu tutakapokifanya kilimo chetu kuwa kilimo cha kisayansi zaidi” amesema Dkt. Christine.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Iringa amesema baada ya kutembelea mabanda ya maonesho mikoa yote inafanya vizuri. Amesisitiza kuwa ili maonesho hayo yawe mazuri zaidi ni vema maandalizi yake yakaanza mapema zaidi katika Halmashauri zote.

Akielezea nini amejifunza katika maonesho hayo, amesema kuwa amejifunza mambo mengi sana ambayo baadhi hakuwa akiyafahamu kabisa, baadhi amejikumbusha baada ya kupita muda mrefu tokea ayafahamu na kusema “maonesho yaha yamekuwa ni shamba darasa kwa watu wengi”. Baada ya kujionea ubunifu wa kiteknolojia kutoka kwa wananchi mbalimbali, ametoa wito kwa mikoa hiyo ya nyanda za juu kusini kuwaangalia wabunifu hao kwa jicho la pekee ili waweze kuwaendeleza zaidi na wao kunufaika na ubunifu wao. Amesema kuwa imani yake ni kwamba pale juhudi za pamoja zitakapowekwa hakika kilimo kitatoka katika hali yake ya sasa na kuwa bora zaidi.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameweka rekodi katika maonesho hayo ya Nanenane baada ya kutembelea mabanda 40 ya maonesho kwa siku na kupokea maelezo na kuuliza baadhi ya maswali kwa waoneshaji mbalimbali.

=30=

RC IRINGA ALIPOTEMBELEA MABANDA YA 8 8 KATIKA UWANJA WA JOHN MWAKANGALE



 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma (mwenye sutu ya zambarau) akikagua zana alipotembelea Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa


  Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma (mwenye sutu ya zambarau) akikagua Mambo ya Lishe alipotembelea Banda la Halmashauri ya manispaa ya Iringa


 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma (mwenye sutu ya zambarau) akipokea maelezo ya Malisho ya Mifugo


 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma (mwenye sutu ya zambarau) katika picha ya pamoja alipotembelea banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa. 


Mama Kiula ajumuika na wadau katika kutembelea Maonesho ya Nanenane Mbeya

 Banda la Manispaa ya Iringa 

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma akisaini Kitabu cha Wageni katika banda la Manispaa ya Iringa

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr Christine Ishengoma akibadilishana mawazo na Mjasiliamali jasiri, Genoveva Barnabas

Dr. Ishengoma katika banda la ASAS  

 RC Iringa akikagua banda la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kulia ni kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa


 Mkuu wa Mkoa wa Iringa  akikagua mabanda ya Maonesho kulia kwake ni Shenal Nyoni

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa akipokea maelekezo katika banda la Halmashauri ya Wilaya Wilaya ya Iringa

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dr. Christine Ishengoma akisaini Kitabu cha wageni katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa

Dr. Christine Ishengoma akioneshwa note feki na noti halisi za 10,000.

Monday, July 30, 2012

KKKT IRINGA WATAKIWA KUSHIRIKI KATIKA SENSA




Washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, usharika wa Iringa Mjini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya uundwaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kufanikisha uundwaji wa Katiba hiyo kwa kujumuisha mapendekezo ya watu wengi zaidi.

Wito huo umetolewa na mgeni rasmi Dkt. Christine Ishengoma katika harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa kanisa kuu la mtaa wa Wilolesi iliyofantik Katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzanaia, Usharika wa Iringa Mjini leo.

Dkt. Christine ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema “ndugu zangu Washarika natoa rai kwenu kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na kuwaeleza waumini wengine na wananchi kwa ujumla ili washiriki katika mchakato huu kwa kutoa elimu na hamasa”. Amesema “napenda kutoa wito kwenu wote kuwa huru kutoa maoni yenu Tume itakapopita katika maeneo na kukusanya maoni yenu”. 

Amesema kuwa baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa Katiba ya sasa inamapungufu kadhaa, hivyo huu ndio wakati wao wa kutoa maoni yao ili hayo mapungufu yaweze kufanyiwa kazi na kuingia katika Katiba mpya. Amesema hili litafanikiwa pale tu, washarika na wananchi watakapojitokeza kwa wingi kutoa maoni yao pindi tume ya kukusanya maoni itakapopita katika maeneo yao. Amewataka kuwa makini katika kusikiliza tarehe na sehemu ambazo mikutano hiyo itakuwa ikifanyika ili waweze kuwasilisha maoni yao kwa tume hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kuwa huru katika kutoa maoni yao na kuwahakikishia kuwa ukusanyaji wa maoni hayo hauhusiani na itikadi yoyote. Amesema ili Katiba hiyo mpya iwe ya mafanikio ni lazima maoni ya wananchi wengi yaweze kukusanywa na mafanikio hayo yanatokana tu, na wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa tume hiyo.  
=30=

TAASISI ZA DINI ZATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO ILI KUFANIKISHA SENSA




Serikali Mkoani Iringa imeomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa dini katika kuhakikisha kuwa elimu ya kutosha na hamasa vinatolewa ili uelewa huo uwafikie waumini na wananchi wengi kwa ujumla.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiendesha zoezi la harambee ya ujenzi wa kanisa kuu la mtaa wa Wilolesi mjini hapa katika ibada ya kwanza iliyofanyika katika kanisa kuu, usharika wa Iringa Mjini.

Dkt. Christine amesema kuwa Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi tarehe 26 Agosti, mwaka huu na kuendelea kwa takriban siku saba. Amesema “Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu za kidemografia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na Watu wote na Makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum”. Amesema kuwa Sensa hiyo ni zoezi lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsi, mahali wanapoishi, hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. 

Akiongelea malengo ya Sensa hiyo, Mkuu wa Mkoa amesema “Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inalenga kutathmini utekelezaji wa Mipango yetu mikubwa ya Maendeleo ambayo imekuwa ikitekelezwa katika kipindi kilichopita. Mipango hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania na Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar”.

Akiongelea nafasi ya kanisa katika kufanikisha Sensa hiyo, Dkt. Christine amesema “napenda kuongelea nafasi ya Kanisa katika kuhakikisha Sensa ya Watu na Makazi inafanikiwa. Ni kweli kuwa Kanisa linalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanikiwa kwa sababu takwimu hizo ndizo zitakazoiwezesha Serikali kutambua hali halisi na mahitaji halisi ya huduma zilipo katika maeneo yenu hivyo kuingizwa katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa”. Amesema “kwa msingi huo, ninawaomba sana kuwahamasisha waumini na wananchi kwa ujumla ili wahesabiwe na wahesabiwe mara moja tu, ili takwimu zitakazokusanywa ziwe sahihi”.

Ameyataja mambo muhimu ya kutiliwa mkazo wakati wa kuwahamasisha washarika na wananchi kwa jumla kuwa ni tarehe ya Sensa, umuhimu wa Sensa na yatakayojiri wakati wa zoezi la kuhesabu watu. Sensa hiyo ya Watu na makazi inaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa’.