Wednesday, October 5, 2011

WALIMU ONGELEENI HIV/UKIMWI

Waalimu Mkoani Iringa wameshauriwa kutenga dakika tano katika ratiba zao za vipindi ili kuzungumza suala mtambuka la ugonjwa wa UKIMWI ili kuinusuru jamii dhidi ya janga hilo.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali la SUMASESU lenye makao yake makuu Wilayani Makete pamoja na watumishi wa Serikali kuu, Halmashauri na taasisi za kidini.
  Bw. Egnatio Mtawa, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMASESU Makete akisoma taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (hayupo pichani)

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Ishengoma amesema kuwa “tuendelee kutoa elimu shuleni ili kukabiliana na ugonjwa wa UKIMWI”, aidha, ameshauri “walimu wa Sekondari kutenga angalau dakika 5 hadi 10 kuzungumzia masuala ya ugonjwa wa UKIMWI”.
Kuhusiana na uhusiano wa mila na desturi dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mila na desturi ni nzuri sana ila tatizo lipo katika zile zinazopotosha. Ameshauri kuwa mila na desturi zote zinazopotosha lazima ziwekwe kando ili jamii iwe salama.
Mkuu wa Mkoa amepongeza ushirikiano baina ya Serikali na SUMASESU katika sekta ya maendeleo ya jamii Wilayani Makete wenye lengo la kuijengea jamii uwezo na kuwa na maendeleo endelevu.
Katika taarifa fupi ya shirika la SUMASESU kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa iliyotolewa na Mkurugenzi wa SUMASESU, Bw. Egnatio Mtawa amesema shirika lake linatekeleza miradi mikubwa miwili ambayo ni Mradi wa Ujana unaofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia shirika la fhi 360 na mradi wa usalama wa chakula unaofadhiliwa na shirika la Mkate kwa Dunia la Ujerumani.
Amesema kuwa mradi wa ujana unashughulika na utoaji elimu kwa jamii ili kujikinga na maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI, elimu ya afya ya uzazi na unyanyasaji wa kijinsia.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Makete, Bibi. Zainabu Kwikwega amesema kuwa lengo la kutembelea shirika hilo la SUMASESU ni kumuelezea Mkuu wa Mkoa shughuli zinazofanywa na shirika hilo kwa wanamakete pamoja na kuwatia moyo ili waendelee na utoaji huo wa huduma kwa wakazi wa Makete.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (kulia) akisalimiana na viongozi wa Wilaya ya Makete alipofanya ziara ya kujitambulisha wilayani humo.
       

Tuesday, October 4, 2011

RC RUVUMA AONGEA NA WAANDISHI WA HABARI

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe Said Thabit Mwambungu amesema kuwa Serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na waandishi wa habari katika ujumbe wa serikali kwa wananchi ili kusukuma gurudumu la maendeleo. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Said Mwambungu akiongea na waandishi wa habari Ofisi kwake

Mhe. Mwambungu amesema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wa Manispaa ya Songea Ofisini kwake hivi karibuni 
Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amewataka waandishi hao wa habari kuendelea kuhabarisha Umma wakizingatia maadili ya habari kwani kwa kukiuka maadili wanaweza kuipotosha jamii na kusababisha hatari katika jamii.
Kwa upande wake Katibu wa Ruvuma Press Club Bw. Andrew Chatwanga  amempongeza  Mkuu wa Mkoa kwa uamuzi wake wa kuongea na wanahabari hao ikiwa ni siku chache tu baada ya kuripoti mkoani kuanza kazi ya kuongoza shughuli za Serikali mkoani hapo.
Bw. Chatwanga alitumia fursa hiyo kumwomba Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za kipekee ili kuifanya Manispaa ya Songea inaboreka kwa usafi wa mazingira kama alivyofanya kwa Manispaa ya Morogoro. Kwa sasa Manispaa ya Songea usafi wa mazingira hauridhishi.

Habari hii ni kwa hisani ya Revocatus A. Kasimba, Afisa Habari, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa

LUDEWA NI PEMBEZONI NA WAPI?? AHOJI RC

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma ametofautiana na uongozi wa Wilaya ya Ludewa katika dhana inayoendelea kuwa Wilaya ya Ludewa ipo pembezoni.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amehoji alipokuwa akizungunza na watumishi na wananchi wa Wilaya ya Ludewa alipofanya ziara ya kujitambusha na kuzifahamu changamoto zinazoikabili Wilaya ya Ludewa.
Dkt. Ishengoma amesema “kuanzia sasa Ludewa hatupo pembezoni”. Aidha, amehoji kuwa Ludewa ipo pombezoni na wapi? Ameendelea kuhoji kuwa “kama Ludewa ipo pembezoni je, mwanzoni ni wapi”.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.) akiongea na watumishi na wananchi wa Wilaya ya Ludewa
Amesema kuwa maendeleo ndiyo dira inayoipeleka Wilaya pembezoni au mwanzoni. Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Wilaya na hali halisi aliyokutana nayo njiani inaonesha kuwa Wilaya hiyo inayo maendeleo yanayoonekana na kupimika.
Amewataka viongozi na wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuachana na dhana hiyo kwani inawafanya kujiona kuwa ni wanyonge na hivyo kujiweka pembeni na dhana ya maendeleo na uwajibikaji kikamilifu.
Aidha, amewataka wanaludewa kuchangamkia fursa iliyopo ya ujenzi wa viwanda na machimbo Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma ili kujumuika katika mchakato wa kujiletea maendeleo.
Akiongelea kero inayowakabili wananchi wa Wilaya hiyo ambayo ni barabara, amesema kuwa barabara za Wilaya hiyo zitajengwa kwa sababu zimeainishwa katika ilani ya uchaguzi ya chama tawala.
Dkt. Ishengoma ametoa ombi kwa watumishi wote wa Umma kuendelea kuipenda serikali yao kwa sababu inawajali na kutekeleza mahitaji yao ikiwa ni pamoja na kuwaletea maendeleo. Vilevile, amewataka kuwajibika kwa serikali yao kwa kuchapa kazi kwa bidii.
Akiongelea miradi ya maendeleo, amewataka watumishi na viongozi wanaosimamia miradi ya maendeleo kwa kutekeleza wajibu huo kulingana na thamani halisi ya fedha za Umma zinazotolewa.
Awali akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Ludewa, Mkuu wa Wilaya hiyo Bibi. Georgina Bundala amesema kuwa Wilaya yake inajishughulisha na shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kilimo (90%), biashara (3%), uvuvi, sekta binafsi (4%) na ajira rasmi (3%).  Amesema kuwa Wilaya yake ina fursa nyingi zinazohitaji kuendelezwa ili ziweze kuchangia katika pato la Wilaya na uchumi wa mwananchi. Amezitaja fursa hizo kuwa ni utajiri mkubwa wa madini ya chuma, makaa ya mawe, dharabu, chokaa na vito mbalimbali vya thamani.
Bibi. Bundala amesema kuwa kwa takwimu za mwaka 2008 wastani wa pato la mwananchi Wilayani Ludewa lilikuwa ni shilingi 125,000 kwa mwaka. Amesisitiza kuwa pato hilo ni dogo sana kukidhi mahitaji muhumu ya kibinadamu. Amesema kuwa mkakati wa Wilaya yake ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kuongeza pato la mwananchi kuendana na viwango vya kimataifa.
Amesema kuwa Wilaya yake inaendelea kuhamasisha jamii kuweza kukuza kilimo cha kahawa, pareto, chai, korosho, alizeti, ufuta, karanga na kupanua kilimo cha umwagiliaji.
=30=

'LUDEWA ONGEZENI KASI KATIKA MAENDELEO ASEMA RC'

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameitaka Wilaya ya Ludewa kuongeza kasi katika kujiletea maendeleo kutokana na kuwa na rasilimali nyingi na ardhi nzuri inayofaa kwa shughuli za kilimo.
Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika sekondari ya Mavanga katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kuzitembelea Wilaya za Mkoa wa Iringa akianza na Wilaya ya Ludewa.
Dkt. Ishengoma amesema “Ludewa ni Wilaya nzuri kwa kilimo na imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi pamoja na madini mengi”. Amesema kuwa Wilaya hiyo inabahati ya kuwa na madini ya makaa ya mawe na  chuma pamoja na madini mengine.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.)(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa BIBI. Georgina Bundala (kulia) wakibadilishana mawazo walipotembelea eneo la Chuma cha Liganga wilayani Ludewa.
Vilevile, amewataka wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuchangamkia fursa zitokanazo na madini hayo hasa pale yatakapoanza kuchimbwa rasmi. Amesema kuwa viwanda vikianza kujengwa lazima viwanufaishe wananchi wa Ludewa kwa wao kuchangamkia fursa za ajira pasipo kubweteka ili maisha bora yawezekane kwao. Amesisitiza kuwa maisha bora hayatawezekana kwa wananchi kubweteka ila pale tu watakapojishughulisha kwa kufanya kazi kwa bidii.
Akiongelea elimu Dkt. Ishengoma amewataka wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa sababu sekta hiyo inamuwezesha mwananchi kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Amesema kuwa wananchi wanawajibika katika kuendeleza sekta ya elimu kwa kusaidiana na serikali yao ili kuinua kiwango cha elimu Wilayani hapo. Amesema “katika kumuwezesha mwananchi kukabiliana na changamoto za leo za kimaisha ni lazima kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuwa elimu inampelekea mwananchi katika kupata ufumbuzi wa changamoto za kimaisha”.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Bibi. Georgina Bundala amesema kuwa wananchi wa Wilaya ya Ludewa ni wasikivu na wachapa kazi sana hasa wanapopatiwa maelezo sahihi kutoka kwa viongozi wao wanaowasimamia na wataalamu. Amesema kuwa Wilaya yake imejikita katika shughuli kadhaa za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kilimo, uvuvi, ufugaji na ujasiliamali.
=30=

RC ASISITIZA MASOMO YA SAYANSI LUDEWA

Mkuu wa Mkoa wa Iringa awataka wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lugarawa kitilia mkazo masomo ya sayansi ili waweze kulitumikia taifa katika fani hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akifungua daharia ya wasichana katika shule ya sekondari ya Lugarawa iliyopo katika kata ya Lugarawa Wilayani Ludewa.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa wanafunzi wengi hasa wa kike wamekuwa wakiyakimbia masomo ya sayansi kwa kisingizio cha ugumu wa masomo hayo jambo alilolikanusha. Amesema “masomo ya sayansi si magumu kama yanavyodaiwa na wengi, masomo yote yanahitaji juhudi na kujituma ili kuweza kufaulu”.  Amesisitiza kuwa elimu ni msingi wa maisha na maendeleo katika kila jamii inayohitaji kustaarabika.
Amesema “wazazi wamekuwa wakijitahidi kujenga miundombinu ya kielimu kama shule, maabara na daharia kutokana na mapenzi yao kwenu (wanafunzi)”. Amesisitiza kuwa kwa msingi huo wanafunzi nao wanajukumu la kurudisha shukrani zao kwa wazazi kwa kufauli vizuri mitihani yao na hatimae kuwa raia wema watakaolijenga taifa lao.
Aidha, amewataka wazazi na jamii ya Ludewa kugeukia pia uwekezaji katika ujenzi wa daharia za wavulana kwa sababu nazo ni muhimu sana katika kudhibiti makuzi ya wanafunzi hao wavulana.
Kwa mujibu wa taarifa ya wananchi wa Kata ya Lugarawa iliyowasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ujenzi wa daharia hiyo ulianza mwaka 2008 hadi mwaka 2010 lengo likiwa ni kuwawezesha wanafunzi wa kike 48 katika shule hiyo kukaa shuleni na kufuatilia masomo yao na kuepukana na hadha za kukaa nje ya shule ikiwa ni pamoja na kupata mimba.
Daharia hiyo iligharimu shilingi milioni 30,785,500 na wananchi wamechangia kiasi cha shilingi milioni 28,085,500 zikiwa ni gharama za kufyatua tofari na fedha taslimu. Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ilichangia shilingi milioni 2,700,000 kwa upigaji bati na saruji.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, yupo katika ziara ya kujitambulisha na kuzifahamu changamoto zinazozikabili Wilaya za Mkoa wa Iringa na kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo.
=30=

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.)(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Bibi. Georgina Bundala (kushoto) wakibadilishana mawazo alipowasili Wilayani Ludewa.

Monday, October 3, 2011

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati) alipowasili Mavanga Wilayani Ludewa na kupokelewa na viongozi wa Wilaya 

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.) (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Georgina Bundala katika Kata ya Mavanga 

Wasomi wakisoma shairi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.) alipowasili Wilayani Ludewa katika ziara ya utambulisho

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII


TAARIFA KWA UMMA

ASALI YA TANZANIA NI NZURI NA INAYO
UBORA WA KIMATAIFA

Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kuwa asali ya Tanzania ni nzuri kwa matumizi ya binadamu na kuwa ina viwango vya ubora vya kimataifa. Ukweli huu umedhihirishwa na maabara mbalimbali duniani, hasa zile za Jumuiya ya Ulaya ambao ndio wanunuzi wakubwa wa asali ya Tanzania.
Ufafanuzi huu unatolewa kufuatia taarifa ya hivi karibuni kupitia baadhi ya vyombo vya habari iliyosema kuwa kuna asali kutoka Tanzania ambayo ilikataliwa nchini China baada ya kuonekana kuwa na kemikali ya Nicotin. Wizara haina taarifa na asali hiyo maana haijatoa kibali chochote cha kusafirisha asali kwenda nchini China kwa miaka ya karibuni. Kisheria asali hairuhusiwi kusafirishwa kwenda nchi za nje bila kupata kibali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kupitia Mpango wa udhibiti Kemikali Katika Asali (Chemical Residue Monitoring Plan) Wiraza ya Maliasili na Utalii inahakikisha kuwa asali ya Tanzania inakidhi viwango vya ubora wa kimataifa. Wizara hukusanya sampuli za asali kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuzifanyia uchambbuzi kwenye maabara teule (Accredited Laboratory) na matokeo yake yanapelekwa  kwa wanunuzi, hasa  Umoja wa nchi za Ulaya ambao ndio wanunuzi wakubwa wa asali ya Tanzania.
Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi 4 za Afrika zinazoruhusiwa kuuza asali yake katika nchi za Umoja wa Ulaya. Kwa mfano, taarifa zinaonyesha kuwa asali inayozalishwa mkoani Tabora haijawahi kupatikana na kemikali ya Nicotin, wala kemikali yoyote inayodhuru binadamu.
Ili kudumisha ubora wa asali ya Tanzania Wizara inazingatia yafuatayo kabla ya kutoa Kibali cha kusafirisha asali kwenda nchi za nje:
  • Asali inakaguliwa na wataalam wa nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii;
  • Asali inapimwa na kuchunguzwa kwenye maabara za hapa nchini na nchi za nje kabla ya kusafirishwa;
  • Kibali cha kusafirisha kinatolewa kufuatana na taarifa ya maabara.
Tarifa za maabara zinaonyesha kila mwaka kuwa asali ya Tanzania haina kemikali zozote zinazoweza kudhuru. Sababu mojawapo inayoifanya asali ya Tanzania iwe na ubora wa asili ni kwa kuwa inazalishwa mbali kutoka kwenye mashamba yanayotumia kemikali. Kwa mfano zaidi ya  aslimia 90 ya asali ya Tabora huzalishwa kwenye mapori ya akiba na misitu ya hifadhi  (Game , Forest Reserves).
Kwa mfano, katika Wilaya ya Sikonge asali huzalishwa katika Misitu ya Hifadhi ya  Nyahua, Ugunda, Uwala na Iswagala. Katika Wilaya ya Urambo asali huzalishwa katika pori la akiba la Ugala na Myovosi/Kigosi na Misitu ya Hifadhi ya Mpanda line, North Ugala, na Igombe. Aidha katika Wilaya ya Uyui asali huzalishwa kwenye Misitu ya Hifadhi ya Igombe, Ilomelo Urumwan na Goweko. Katika maeneo yote haya  wafugaji nyuki hutundika mizinga zaidi ya kilomita 60 kutoka makazi na mashamba ya tumbaku.
Aidha, ufugaji nyuki husimamiwa na Sheria ya Ufugaji Nyuki Namba 15 ya mwaka 2002 ambayo inakataza kufuga nyuki karibu na mashamba yanayotumia kemikali. Inasisitizwa kuwa ufugaji nyuki ufanyike umbali wa kipenyo cha kilomita 7 kutoka mashamba ya tumbaku au mengine yanayotumia viwatilifu.
Sheria hii inatuhakikishia ubora zaidi kuliko Sheria za kimataifa ambazo zinakataza kuzalisha asali katika kipenyo cha kilometa 3 tu. Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Halimashauri za Wilaya inawaelimisha wafugaji nyuki kupitia ughani (Extension Services) kuhusu umuhimu wa kufuga nyuki kwa kuzingatia Sheria ya Ufugaji Nyuki.
Wizara inawakumbusha wafanyabiashara taratibu za kufuata ili kuuza mazao ya nyuki nchi za nje:
  1. Awe na Kampuni ya biashara iliyosajiliwa;
  2. Awe amesajiliwa kama mfanyabiashara wa mazao ya nyuki;
  3. Awe na leseni halali ya Biashara;
  4. Awe na kitambulisho cha mfanyabiashara (TIN);
  5. Awe amepata umepata soko nchi za nje na kuonyesha bei yake;
  6. Ubora wa mazao yake yahakikiwe na Wizara ya Maliasili na Utalii na kupewa kibali cha kusafirisha nje ya nchi.
Ili kudumisha ubora wa mazao ya nyuki wafugaji na wafanyabiashara wanatakiwa kuzingatia utaalam wa ufugaji nyuki, usafirishaji na ufungashaji. Utaalam huo hutolewa bure na wataalam wa Ufugaji Nyuki.
Inasisitizwa kuwa wafanyabiashara wote wanatakiwa kupata kibali cha kusafirisha asali nje ya nchi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.


George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 21 Septemba 2011

Saturday, September 24, 2011

MKUU WA MKOA WA RUVUMA AKABIDHIWA RASMI OFISI

  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe Said Thabit Mwambungu akisalimiana na watumishi wa ofisi yake mara baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza kuanza kazi ya kuuongoza mkoa huo. Kulia kwake ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Dtk Anselm Tarimo


 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Said Thabit Mwambungu akisaini kitabu cha wageni katika ofisi yake mpya mara baada ya kuripoti kuanza kazi ya kuongoza shughuli za Serikali mkoani Ruvuma. Kushoto ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Dkt Christine Gabriel Ishengoma ambaye sasa ameahamia Mkoa wa Iringa

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Said Thabit  Mwambungu akipokea hati ya Makabidhiano ya ofisi kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dkt Christine Gabriel Ishengoma tukio hilo lilishuhudiwa na wakuu wa sehemu na vitengo wote.

Picha zote kwa hisani ya Revocatus A. Kasimba, Msemaji wa Mkoa wa Ruvuma

Thursday, September 22, 2011

OFISI YA MKUU WA MKOA WATAKIWA KUDUMISHA MAWASILIANO

Wafanyakazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kudumisha mawasiliano baina yao ili kuweza kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa nyufa za kimawasiliano.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa ofisi yake kwa lengo la kufahamiana na kuboresha utendaji wa kazi.

Dkt. Ishengoma amesema “mawasiliano baina yetu ni nyenzo muhimu sana na kama kutakuwa na ufa wa kimawasiliano hatuwezi kwenda mbali katika utendaji wetu”.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni mtaalamu wa tasnia ya mbinu za mawasiliano ameitaka timu ya wataalamu wa ofisi yake kuendeleza utamaduni uliojengeka wa kuandaa taarifa na kuziwasilisha taifani kwa wakati ili kuendelea kulijenga jina zuri la Mkoa wa Iringa.

Aidha, amesisitiza usimamizi madhubuti wa fedha za Serikali kuu na Halmashauri. Amesema katika kuzisimamia Halmashauri “si kwa kukaa ofisini tu bali kwa kuzitembelea Halmashauri na kuwafikia walio vijijini”.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wafanyazi katika ofiisi yake kushirikiana katika kazi na kutokupigana vikumbo ili kufanikisha utendaji kazi.   
  
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuongea na wafanyakazi, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka amesema kuwa una jukumu la kuziwezesha na kuzijengea uwezo Serikali za Mitaa, kufikisha huduma bora za kiuchumi na kijamii na kuhakikisha amani, usalama na mshikamano unakuwepo.

Wednesday, September 21, 2011

RS WATAKIWA KUZIPENDA KAZI ZAO

Wafanyakazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kuzipenda kazi zao na kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufikia mafanikio ya kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa ofisi yake kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamiana na wafanyakazi wake.

Dkt. Ishengoma amesema “napenda kila mmoja apende kazi yake na asitamani kazi ya mwenzake na mambo yatajipa yenyewe hasa akiifanya kwa bidii”.

Aidha, amewataka wafanyakazi hao kuitumia fursa iliyopo Mkoani hapa ya wingi wa vyuo na vyuo vikuu kujiendeleza kitaaluma. Amesema “elimu haina mwisho na wafanyakazi wasisite kujiendeleza kielimu kwa sababu hakuna atakayekusukuma kujiendeleza”. Amesisitiza kuwa kila jambo jema chini ya jua linatokana na malengo madhubuti na kuwataka wafanyakazi hao kutokuridhika na kile walichonacho na kutamani kuendelea zaidi.

Aidha, amewataka wafanyakazi hao kuwa na wivu wa maendeleo. Amesema kinachomsaidia mwanadamu ni nia ya dhati ya kufanikiwa katika njia zilizo za halali.

Awali Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka alitoa pongezi kwa uteuzi wa Dkt. Ishengoma kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Aidha, aliahidi kwa niaba ya wafanyakazi wote kutoa ushirikiano unaostahili kwa Mkuu huyo wa Mkoa ili kuufanya Mkoa wa Iringa uzidi kusonga mbele katika kuimarisha ustawi wa wananchi.

Ikumbukwe kuwa Dkt. Ishengoma aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa akitokea Mkoa wa Ruvuma alipokuwa pia Mkuu wa Mkoa.

Tuesday, September 20, 2011

RC IRINGA AHAIDI USHIRIKIANO KUKUZA PATO LA MWANANCHI


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma ameahidi kushirikiana na viongozi wa Mkoa huo ili kuinua pato la mwananchi wa chini kwa minajili ya kumuinua kiuchumi.

Kauli hiyo ameitoa ofisini kwake wakati akipokea taarifa ya makabidhiano ya Mkoa wa Iringa iliyowasilishwa kwake na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka.

Amesema “ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega ili kuhakikisha mwananchi wa chini anainua uchumi wake yeye mwenyewe hasa kwa kuongeza pato lake”.

Dkt. Ishengoma ameitaja changamoto nyingine inayoukabili Mkoa wa Iringa kuwa ni ile ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Amesema Mkoa unachangamoto mahususi ya kuhakikisha inateremsha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kutoka asilimia 15.7 ya sasa  hadi kufikia angalau asilimia tano. Amesema kuwa japokuwa dawa ya ugonjwa huo bado haijapatikana ila wananchi wenyewe wanayo dawa ikiwa ni pamoja na kubadili tabia.

Aidha, amewataka viongozi wa Mkoa kuangalia maeneo yanayohitaji kufikishiwa zaidi elimu ya maambukizi ya UKIMWI ili kuweza kuinusuru jamii na janga hilo. Amesema kuwa ugonjwa huo ni lazima jitihada za kuudhibiti zifanyike ili kupunguza idadi ya yatima na wajane wanaotokana na matokeo ya ugonjwa huo.

Awali akiwasilisha taarifa ya makabidhiano ya Mkoa wa Iringa, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka amesema kuwa katika mwaka 2005 pato la Mkoa wa Iringa lilikuwa ni shilingi 867,482,000,000 huku Mkoa ukishika nafasi ya tano kitaifa. Aidha, pato la mkazi lilikuwa ni shinlingi 558,444 na Mkoa ulishika nafasi ya pili kitaifa.

Amesema katika mwaka 2010/2011 pato la Mkoa lilifikia Shilingi  1, 469, 720, 000,000 na pato la mkazi lilikuwa limeongeka kufikia Tshs 859,875 ambalo ni ongezeko la Shilingi 301,431 (54%).

Mpaka amesisitiza kuwa pato la Mkoa linaonekana ni kubwa lakini kwa kiasi kikubwa huchangiwa na mashamba makubwa ya chai, viwanda vya chai, misitu na viwanda vya mbao.

Upande wa Maambukizi ya UKIMWI Katibu Tawala huyo amesema kuwa Mwaka  2003/2004 maambukizi yalikuwa 13.4% na Mwaka 2010/11 maambukizi yamefikia 15.7%. Aidha, hadi Desemba, 2010/11 wananchi 74,632 wenye Virusi vya UKIMWI walioandikishwa kwenye Mpango wa Dawa za kupunguza makali.

Mkoa umekamilisha Mpango wa miaka minne 4 wa kupambana na tatizo la UKIMWI. Mpango huu ni kuanzia Oktoba 1998 hadi Septemba 2012.

MKUU WA MKOA WA IRINGA AWASILI RASMI MKOANI IRINGA

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (mwenye suti nyekundu) akizungumza na watumishi waliojitokeza kumlaki

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (mwenye suti nyekundu) akizungumza na watumishi waliojitokeza kumlaki kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka


 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (mwenye suti nyekundu) akiwasalimia wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa nje ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 

Mhandisi David Mwakalalile ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

 Kenneth Komba, Afisa Michezo ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

 Bibi. Hawa Kalolo ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

 Avelina Ngonyani, Mwangalizi wa Ofisi ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

 Neema G. Mwaipopo, Afisa Tawala ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

 Dennis Gondwe, Afisa Habari ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

 Bibi. Laurencia Mwanga, Katibu Muhtasi ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake


 Joseph Mnyikambi Afisa Elimu Mkoa ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

 Bw. Adam Swai, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Uchumi na Sekta za Uzalishaji ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

  Bw. Theophil Likangaga, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Huduma za Jamii ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

  Bw. Vicent James, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Miundombinu  ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake


 Bw. Barnabas Ndunguru, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu ni miongoni mwa watumishi waliopata bahati ya kusalimiana ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma siku ya kwanza ya kuripoti kwake

HATIMAE DIMOSO AWAPELEKA MATOMBO

Menrad Dimosso akitoa shukrani zake kwa ujumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na zawadi waliyompatia katika sherehe ya harusi yake iliyofanyika katika ukumbi wa NESTO ZANGIRA- MATOMBO.

 Menrad Dimosso akitoa shukrani zake kwa Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Nuhu Mwasumilwe baada ya kukabidhi zawadi ya Mkoa katika sherehe ya harusi yake iliyofanyika katika ukumbi wa NESTO ZANGIRA- MATOMBO.

Bwana harusi Menrad Dimosso na mkewe wakila keki kwa staili walioichagua wao 

 Hiyo ilikuwa miondoko ya KWAITO likiwa ni ombi mahususi la Sam Nyagawa

Mwenyekiti wa Kamati ya Harusi ya Menrad Dimosso Bi. NINA

Baadhi ya watumishi wa RS Iringa waliopata fursa ya kuwa mashuhuda

 Baadhi ya watumishi wa RS Iringa waliopata fursa ya kuwa mashuhuda

Mke wa Menrad Dimosso akirekebisha koti la MZEE baada ya kumvika ndani ya ukumbu wa NESTO ZANGIRA 

 Mke wa Menrad Dimosso akiingia ukumbini

Menrad Dimosso akiingia ukumbini

Monday, September 19, 2011

 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mteule Mhe. Dkt. Christine Ishengoma anatarajiwa kuwasili kesho katika kituo chake kipya cha kazi (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa) .

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa watu wote na kubandikwa katika mbao za matangazo katika Ofisi hiyo kutoka Sehemu ya Utawala inasema kuwa mteule huyo atawasili majira ya saa tano asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki.

Aidha, watumishi wote katika Ofisi hiyo wametakiwa kujitokeza muda huo ili kumlaki.

Mtandao wa www.dennisgondwe.blogspot.com unamtakia kila la kheri katika kituo chake kipya ukiamini KAZI KWANZA KATIKA KUIJENGA IRINGA YENYE NEEMA TELE