Monday, December 19, 2011

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa yapata Wakili




Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, imepata Wakili, baada ya Mwanasheria katika Ofisi hiyo Paulos Lekamoi, kusajiliwa na kutambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.




Wakili Paulos Lekamoi akitambuliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Bara

Fuatilia habari zaidi juu ya Paulos Lekamoi ni nani hasa??

YALIYOJILI MIAKA 50 YA UHURU KWA MKOA WA IRINGA KITAIFA

































 Baadhi ya watendaji katika Banda la Mkoa wa Iringa


 Baadhi ya watendaji katika Banda la Mkoa wa Iringa



 Mandari ya Banda la Mkoa wa Iringa kwa nje



 Sidhani kama kuna kitu ambacho kingeweza kuwatoa viongozi hawa wa Mkoa wa Iringa katika banda hili la Mkoa wa Kagera kabla ya kutimiza hadhima yao mahususi. 


 Miaka 50 ya Uhuru na Tafakari ya hali ya juu


 ...Hii inakutosha Mhe. RC ni maneno ya mjasiriamali 'Khadija Design' akimwambia Mhe. Mkuu wa Mkoa hayupo pichani.


 Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Zainab Kwikwega akisaini kitabu cha wageni katika Banda la Mkoa wa Iringa katika viwanja vya Mwl. J.K. Nyerere katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara


 Tarehe 01. Disemba, 2011 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka (katikati) na Kiongozi mwandamizi wa Banda la Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni wakiweka mikakati ya mapokezi ya viongozi wa kitaifa watakaotembelea banda la Mkoa wa Iringa


 Tarehe 01. Disemba, 2011 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka (kulia) wakifurahia jambo katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara


 Tarehe 01 Disemba, 2011, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) akiwa ni
miongoni mwa mamia kwa maelfu ya watanzania waliojumuika katika maadhimisho ya
Miaka 50 ya Uhuru katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam

Tarehe 01 Disemba, 2011, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka akiwa ni
miongoni mwa ma mia kwa maelfu ya watanzania waliojumuika katika maadhimisho ya
Miaka 50 ya Uhuru katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam



TANROADS YAKUSANYA MIL 18


Ofisi ya Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa (TANROADS) imekusanya zaidi ya shilingi milioni 18 katika kipindi cha kuanzia Julai, 2011 hadi Septemba, 2011 zikiwa ni tozo kwa magari yaliyozidisha uzito.

Taarifa hiyo imetolewa na Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa iringa, Mhandisi. Paul Lyakurwa, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa mwaka 2010/ 2011 na mpango wa matengenezo na ukarabati kwa mwaka 2011/2012 na taarifa ya utekelezaji hadi Septemba, 2011 ya Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa katika Kikao cha Bodi ya Barabara ya mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa St. Dominic katika Manispaa ya Iringa,

Mhandisi. Lyakurwa amesema kuwa ofisi yake inajukumu la kudhibiti uzito wa magari barabarani kwa kutumia mizani isiyohamishika iliyopo Makambako.
Amesema katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Septemba, 2011 magari yaliyopimwa ni 1,005 kati ya hayo magari 103 yalizidisha uzito na kulipishwa tozo la uharibifu wa barabara kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Barabara Na. 30 ya mwaka 1973 na kanuni zake za mwaka 2001 ofisi yake imekusanya shilingi 18.175 milioni.

Akielezea utekelezaji wa ahadi za Mhe. Dk. Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 zilizo katika Ilani ya uchaguzi ya CCM kuhusu sekta ya barabara Mkoani Iringa, hasa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Njombe- Makete (Km. 109 kwa kiwango cha lami amesema kuwa ujenzi wa Km. 11.5 kwa kiwango cha lami kati ya Mang’oto na Tandala ndani ya Wilaya ya Makete umekamilika kwa gharama ya shilingi 4,612,654 milioni.

Amesema ujenzi wa Km. 1 umepangwa kutekelezwa mwaka wa fedha 2011/2012 maeneo ya Mang’oto kwa gharama ya shilingi 797,040 milioni pamoja na utekelezaji huo kiasi cha shilingi 1,480,644 milioni zinahitajika kulipia deni la kazi zilizofanyika kati ya mwaka 2008/ 2009 na mwaka 2010/ 2011.    

Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma ameagiza ushirikishwaji wa jamii katika utunzaji wa miundombinu ya Mkoa wa Iringa ili iweze kuwanufaisha wananchi walio wengi.

Akifungua kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa wa Iringa, amesema bado kuna mapungufu kadhaa katika ushirikishwaji wa jamii katika utunzaji wa miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Iringa hususani shughuli zinazofanyika ndani ya hifadhi ya barabara na kuagiza jamii ihusishwe kikamilifu katika utunzaji huo wa miundombinu ya barabara.
=30=


Saturday, December 17, 2011


Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka ameshauri kudumisha ushirikiano wa kimkakati baina ya watumishi wa serikali na sekta binafsi ili jitihada za kumletea maendeleo mwananchi ziendelee kuzaa matunda mara dufu.
Mpaka amesema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi alipokuwa akiwasili katika viwanja vya maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere jijini hapa.
Amesema, “mafanikio katika utumishi wa Umma yataletwa kwa kudumisha ushirikiano baina ya watumishi wa Umma na watumishi wa Umma, na watumishi wa Umma na taasisi nyingine zisizo za Umma”. Amesema, “ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kiserikali ndio msingi wa mafanikio na hasa umuhimu huo huonekana pale unapotumika katika kutatua changamoto inayoikabili taasisi na kutafutiwa ufumbuzi wake kwa kuusisha mtumishi zaidi ya mmoja kwa maana nyingine uhumihu huo kufanya kazi kwa umoja”.
Mpaka amesema kuwa Mkoa wa Iringa umefanikiwa katika miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kutokana na dhana ya ushirikiano na umoja katika utendaji kazi.  Amesema, sekta za afya, elimu, miundombinu, maji na utawala bora katika Mkoa wa Iringa zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano huo.
Akiongelea utawala bora, amesema Mkoa umeendelea kuweka masanduku ya maoni katika sehemu zote za kutolea huduma kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa kuwapa wananchi nafasi ya kutoa maoni, malalamiko na michango yao kwa lengo la kuusaidia Mkoa katika kuzitatua kero hizo. Ameongeza kuwa Ofisi yake inae Afisa anayeshughulikia pamoja na mambo mengine malalamiko ya wananchi na watumishi na utaratibu huo umeteremshwa hadi katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Tarafa.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, amesema utawala bora katika ngazi ya Mkoa umejikita pia katika uboreshaji wa ofisi za Tarafa ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Amezitaja ofisi 14 za Tarafa zilizojengwa katika uboreshaji na usogezaji wa huduma karibu na wananchi kuwa ni Pawaga, Liganga, mwambao, Masasi, kalenga, Mlolo, Ifwagi, kibengu, Makambako, Magoma, Ukwama, Ikuwo, Malangali na Mahenge. Amesema zaidi ya lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi pia Mkoa umelenga kuyaboresha mazingira ya kazi ya Maafisa Tarafa.
Amesema, Mkoa umeendelea kutumia mbinu ya fursa na vikwazo vya maendeleo (o & OD) na inayowahusisha wadau wengine wa maendeleo hutumika katika kupanga mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya kijiji.
Atuganile George ni miongoni mwa wananchi waliofika kutembelea mabanda ya maonesho katika viwanja vya mwalimu Julius Nyerere amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni sekta ya Utumishi wa Umma imeendelea kuboreka tofauti na kipindi cha nyuma. Amesema “unajua ndugu mwandishi kipindi hiki hata ukiingia katika baadhi ya ofisi za serikali unajisikia kuwa umeingia katika ofisi zinazotoa huduma kwa wananchi kiukweli hali imebadilika na kuwa bora”.
=30=

MIAKA 50 NI MAFANIKIO NA CHANGAMOTO


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka watanzania kuyatumia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kutafakari mafanikio na changamoto kama taifa kwa kufanya ulinganifu na uchambuzi kupitia taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali nchini.
Kauli hiyo ameitoa nje ya banda la Mkoa wa Iringa, alipofanya ziara ya kujifunza mafanikio na changamoto za miaka 50 ya Uhuru katika viwanja vya maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara vya Mwalimu Julius Nyerere.
Mkuu huyo  wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesema maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru ni maadhimisho maalumu, tofauti na sherehe za maadhimisho tulizozoea kufanya kutokana na uzito wa kimantiki kupitia madhumuni na kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo “tumethubutu, tumeweza na tunazidi kusonga mbele”.
Amesema kwa upande wake anakubaliana kimsingi na hatua ya serikali ya kuamua kuhadhimisha maadhimisho hayo kwa kuzihusisha taasisi mbalimbali nchini katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere ili kuwapatia wananchi fursa ya kujionea na kupata maelezo ya kina juu ya maendelea yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo. Amesema, “zaidi ya wananchi hata watendaji wa serikali lazima wayatumie maadhimisho hayo kubadilishana uzoefu na mbinu za kukabiliana na changamoto katika baadhi ya maeneo ambayo taasisi nyingine zimefanya vizuri zaidi, na hii ndiyo maana ya maadhimisho yenyewe ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara”.
Akiongelea mafanikio ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Mkoa wake wa Iringa, Dk. Christine amesema kuwa kama Mkoa pamoja na mambo mengine, anajivunia kuongezeka kwa pato la Mkoa. Amesema, “ukirejea kipindi cha Uhuru, pato la Mkoa wa Iringa lilikuwa ni shilingi 5,693,000, wakati wastani wa pato la mkazi likiwa ni shilingi 103.  Katika mwaka 2010 pato la Mkoa wa Iringa liliongezeka hadi kufikia shilingi 1,702,430,000, wakati pato la mkazi nalo liliongezeka hadi kufikia shilingi 979,882”.
Amesema changamoto anayoiona kwa sasa ni kulitafsiri pato hilo kwa maana ya mkazi mmoja mmoja na jinsi linavyochangia katika kubadilisha maisha yake ya kila siku badala ya kuonekana katika ujumla wake. Akifafanua zaidi amesema kuwa sehemu kubwa ya pato la Mkoa wake huchangiwa na mashamba makubwa ya chai  na viwanda vya chai, misitu na viwanda vya mbao na tumbaku.
Ukiwa umesheheni wataalamu wa fani kadhaa, Mkoa wa Iringa unaokadiriwa kuwa na wakazi 1,764,285 pamoja na Halmashauri zake ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki katika maadhimisho hayo, ukiwa unashiriki kikamilifu katika kuonesha, kuchangia uzoefu wa mafanikio, changamoto na wadau mbalimbali nchini.
=30=

IDODI FIKIRIENI KILIMO CHA MTAMA


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amewataka wananchi wa Tarafa ya Idodi kufikiria kilimo cha mazao yanayostahimili ukame ili kukabiliana na tatizo la njaa linalowakabili wananchi wa Tarafa hiyo mara kwa mara.
Dk. Ishengoma anayefanya ziara maalumu ya kuhamasisha shughuli za kilimo na elimu katika Mkoa wa Iringa, siku yake ya kwanza ya ziara aliyoifanya katika Kata ya Nzihi, Tungamalenga na Mahuninga amesisitiza kilimo cha zao la mtama pamoja na mazao mengine. Amesema “si lazima kulima mahindi na mpunga tu kama zao la chakula, bali tubadilishe kidogo fikra ili tuweze kulima mazao yanayostahimili ukame na tuanze na zao la mtama”.
Amesema pamoja na jitihada za Serikali ya Mkoa kuhimiza kilimo cha zao la mtama lakini mkulima mmoja mmoja ni vizuri akalima pia muhogo na viazi vitamu kwa kujihakikishia uhakika na hifadhi ya chakula.
Amesema kuwa matarajio ni kila kaya kulima angalau ekari mbili za mtama. Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, itazigawa hizo mbegu bure kwa wakulima na kuwakumbusha wakulima kuwa wamebakiwa na kazi moja tu ya kulima baada ya kuondolewa gharama za kununua mbegu ya mtama. Vilevile, amesisitiza kuwa serikali itakuwa makini katika kuzigawa mbegu hizo kwa kuangalia eneo lililolimwa ili kuepukana na baadhi ya wakulima kuzitumia kwa matumizi mengine tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na serikali.
Aidha, amewataka wananchi kujihusisha na ufugaji wa wanyama wadogo wadogo ili uweze kuwasidia katika kukidhi mahitaji ya kawaida ya nyumbani. Amesema “ufugaji wa wanyama wadogowadogo unasaidia sana hasa akina mama kuweza kukidhi mahitaji ya familia”.
Akiongelea ufugaji wa ng’ombe ameshauri kuwa yatumike madume bora ili kupata maziwa mengi. Vilevile ameshauri kutumia njia ya uhamilishaji ili kupunguza gharama za ufugaji wa madume mengi ya ng’ombe na uhifadhi wa mazingira.
Kuhusu elimu, Mkuu wa Mkoa ameagiza watoto wote watakaofaulu wapelekwe shule ili kukuza kuwango cha elimu katika Mkoa. Amesema “kila mmoja lazima aone fahari kumpeleka mwanae shule na hasa watoto wa kike ili kuachana na tamaduni za kale zilizokuwa zikimfanya mtoto wa kike kukosa elimu”.
=30=

RC AKEMEA UKATAJI MITI


Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameagiza kuacha tabia ya kukata miti ovyo ili kuunusuru Mkoa na kugeuka jangwa kama baadhi ya maeneo ambayo yanakubwa na ukame wa mara kwa mara na kusababisha upungufu wa chakula.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akiongea na wananchi wa Kata ya Idodi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa alipofanya ziara ya kuhamasisha shughuli za kilimo na elimu.
Dk. Ishengoma amesema kuwa katika kipindi cha kuandaa mashamba wananchi wamekuwa na tabia ya kukata miti katika mashamba yao. Amesema “msikate miti yote sababu miti hii ndiyo inayotengeneza mvua hivyo, tukiendelea kukata miti hiyo ukame hautaisha bali utazidi kuongezeka katika eneo kubwa zaidi”.
Kutokana na ukame wa mara kwa mara unaosababisha upungufu wa chakula, Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na upungufu wa chakula ikiwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha mtama amesema Dk. Ishengoma.
Amesema ni vizuri wananchi wakabadili mawazo ya kutegemea mazao ya mahindi na mpunga pekee na kufikiria kilimo cha zao la mtama.
Akiongelea vocha za pembejeo za kilimo, amesema kuwa wananchi waliopata vocha hizo wazitumie vizuri ili kuweza kunufaika nazo na kufikiwa kwa malengo ya serikali ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia kilimo. Amesema wananchi wanawajibu wa kufahamu kuwa seti moja ya vocha za pembejeo inahusisha mbolea ya kupandia, mbegu bora na mbolea ya kukuzia.
Aidha, alitahadharisha kwa mawakala wasiowaaminifu kuwa lazima wafuate utaratibu uliowekwa katika usambazaji na matumizi ya vocha hizo na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wakala yeyote atakayekiuka utaratibu uliowekwa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa anafanya ziara ya kuhamasisha kilimo na elimu baada ya msimu wa kilimo kuanza wakati baadhi ya sehemu katika Tarafa ya Idodi ni miongoni mwa maeneo yaliyokubwa na ukame na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula. 
=30=

MALENGAMAKALI WEKEZENI KATIKA ELIMU


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi wa kata ya Malengamakali kuwekeza katika elimu ya watoto wao ili iweze kuwasaidia kwa kujiletea maendeleo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akiongea na wananchi wa kata ya Malengamakali iliyopo katika Jimbo la Ismani katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Dk, Ishengoma amesema “kwa kuwa leo tumepata nafasi ya kukutana hapa napenda kuwaomba wazazi wote kuhakikisha watoto wote waliomaliza darasa la saba na kufaulu wanahimizwa kwenda sekondari”.  Amesema elimu ndiyo hazina pekee mzazi anayoweza kujivunia kwa mtoto wake hivyo ni lazima kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanapelekwa sekondari.
Kwa upande wa kilimo Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kutokana na sehemu kubwa ya Mkoa kukumbwa na upungufu wa chakula uliosababishwa na upungufu wa mvua ulioleteleza ukame, mkoa umeweka mkakati wa kilimo cha mazao yanayostahimili ukame. Amesama mkakati unaoendelea kwa sasa ni kilimo cha zao la mtama.
Amesema kwa sasa wananchi wa mkoa wa Iringa tunaimba wimbo mmoja nao ni kilimo cha mtama. “Tumekubaliana kilimo cha zao la mtama kwa sababu zao la mtama linavumilia ukame kutokana na upungufu wa mvua”.  Amesema “pamoja na shukrani tunazozitoa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutupatia chakula cha njaa, lakini hatuwezi kukubali kama wanairinga huo ukawa utaratibu wetu wa kusaidiwa chakula cha njaa, lazima sisi wenyewe kukabiliana kwa pamoja na upungufu wa chakula kwa kulima mazao yanayovumilia ukame”.
=30=

WALIMU WA KUJITOLEA WASAIDIWE


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amezishauri serikali za kata na vijiji kuangalia uwezekano wa kuwasaidia vijana wanaofanya kazi ya kufundisha kwa kujitolea baada ya kumaliza masomo yao.
Ushauri huo ameutoa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akiongea na wananchi wa kata ya Idunda iliyopo wilayani Mufindi.
Mkuu wa Mkoa alikuwa akijibu swali juu ya mpango wa serikali wa kuwaajiri vijana wanaojitolea kufundisha katika shule za msingi na sekondari  katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mufindi. Dk. Ishengoma amesema “ni kweli vijana hawa wanaokuwa wamemaliza kidato cha nne na sita na kujitolea kufundisha madarasa yaliyochini  yao wanamchango mkubwa katika kutoa mchango wao kwa kuwafundisha wananfunzi wa shule za msingi na sekondari”.
 Amesema kutokana na upungufu wa walimu uliopo katika baadhi ya maeneo ya Kata za Wilaya ya Mufindi, vijana hawa wanaojitolea wanasaidia kupunguza upungufu uliopo ila ni jukumu la serikali za vijiji na kata iangalie upungufu uliopo katika ikama za shule zao na kuweka mikakati ya kuwasaidia ili wanafunzi waweze hao wakati serikali inaendelea kuongeza idadi ya walimu katika shule zake.
Aidha, kuhusu kuwaajiri amesema kuwa serikali haina utaratibu wa kuwaajiri watumishi wasiopitia mafunzo na kupata utaalamu unaostahili katika fani husika. Mkuu wa Mkoa ameziagiza Hamlashauri pindi yanapotokea matangazo ya kozi mbalimbali yaweze kutawanywa katika Kata na vijiji ili vijana wengi waweze kuyasoma na kuomba kozi hizo.
Akiongelea changamoto inayoikabili shule ya sekondari ya Idunda sambamba na umbali wa wanafunzi kati ya nyumbani na shuleni, Dk. Ishengoma amewataka wananchi wa Kata hiyo kuanza ujenzi wa Daharia za wanafunzi kwa juhudi na kuahidi kuwachangia shilingi 1,000,000. 
=30=

MIAKA 50 YA UHURU = MWALIMU NYERERE


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru hayawezi kutenganishwa na juhuri zilizofanywa na Baba wa Taifa katika kupigania Uhuru wa Tanzania na hapo ndipo historia inapoanzia.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesema kuwa tupo hapa leo kwa ajili ya kuadhimisha maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika Tarafa ya Mdandu wilayani Njombe. Kwa ujumla Mwaka huu una umuhimu wa kipekee hasa kwa Historia ya nchi yetu. Hapa  tulipofika na hatua tuliyopiga sio ya kubezwa hata kidogo kama baadhi ya watu wanavyotaka tuamini kuwa hakuna chochote kilichofanyika katika kipindi hiki cha miaka 50 ya Uhuru.
Dk. Ishengoma amesema “Sio rahisi kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru bila kukumbuka juhudi zilizofanywa na Baba wa Taifa na Muasisi wa Chama cha TANU katika harakati za kupigania Uhuru”. Amesema “Nchi yetu ilikuwa duni sana wakati wa uhuru kutokana na ujenzi wa mfumo wa Ubepari, Ukabaila na Unyonyaji ilivyokuwa imejengwa wakati huo”.
Dk. Ishengoma amesema ili kuinusu nchi hii zilihitajika juhudi zenye dhamira ya kizalendo zilizofanyika kupitia Azimio la Arusha, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, Siasa ni Kilimo, ‘Operatio’ vijiji, kisomo chenye manufaa, kuunganishwa kwa TANU na ASP na kuzaliwa kwa CCM, kurejeshwa kwa serikali za mitaa na kung’atuka kwa viongozi kwa mujibu wa Katiba.
Amefafanua kuwa haya yote mafanikio makubwa nchi inayojivunia kwa miaka 50 ya Uhuru misingi yake imejengwa katika uzalendo huo.
Akiongelea mafanikio ya elimu, amesema “Tulipopata uhuru, kilikuwepo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tu kilichokuwa na wanafunzi 14 wa kitivo cha Sheria. Sasa Tanzania ina vyuo vikuu na vyuo vishiriki visivyopungua 30. Mkoa wa Iringa Peke yake tuna Vyuo Vikuu 5”. Haya ni mafanikio makubwa sana na si ya kubeza hata kidogo.
Mkoa wa Iringa ukiwa ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania Bara unaadhimisha miaka 50 ya Uhuru sambamba ya maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Mkoa huo chini ya kauli mbiu “tumethubutu, tumeweza na tunazidi kusonga mbele”. Aidha, mkoa huo umepangiwa kufanya maadhimisho hayo tarehe 7-9 Novemba mwaka huu.
=30=

IRINGA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO


Mkoa wa Iringa umeendelea kuimarisha sekta ya miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wake wananufaika zaidi na miundombinu hiyo kwa kujiletea maendelea endelevu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Mkoa wa Iringa yanayofanyika katika Tarafa ya Mdandu Wilayani Njombe.
Dk. Christine amesema “mwaka 1961 hali ya miundombinu ya mawasiliano katika Mkoa wa Iringa ilikuwa duni sana, barabara nyingi zilikuwa hazipitiki kwa urahisi kwa mfano kwenda Ludewa au Makete tulitumia siku 2 au 3”.
Amesema mwaka 1961 mkoa wa Iringa ulikuwa na mtandano wa barabara upatao Km. 1,209.5 kati ya hizo Km. 76 ni barabara za vumbi na Km. 1,133.5 ni changarawe. Mwaka 2010 mtandao huo umeongezeka hadi kufikia Km. 8,776.56 kati ya hizo Km. 530.1 ni lami, Km. 5,942.06 ni changarawe na Km. 2,304.40 ni barabara ya udongo.  
Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameeleza mafanikio makubwa katika mawasiliano ya simu za mkononi, redio, televisheni, mtandao wa interneti, magazeti na fax. Ameongeza kuwa Mkoa umefanikiwa kuwa na umeme katika makao makuu ya wilaya zote.
Aidha, amesema kuwa ili Mkoa wa Iringa uendelee kupata mafanikio makubwa katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ni lazima kudumisha amani iliyoachwa na waasisi wa taifa letu. Amesema kuwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano ni njia pekee ya kuwaenzi waasisi wa taifa letu.
Katika taarifa fupi ya Wilaya ya Njombe, iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Sara Dumba, amesema kuwa wilaya yake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu ndani ya miaka 50 ya Uhuru. Amesema katika elimu ya msingi wilaya imeweza kuongeza idadi ya shule toka shule za msingi 44 hadi kufikia shule 260. Amesema kuwa shule za sekondari pia zimeongezeka kutoka moja mwaka 1971 hadi kufikia shule 62 mwaka 2011. katika elimu ya ufundi, wilaya ilikuwa na shule na vituo vya ufundi stadi vinne wakati wa uhuru lakini kufikia mwaka 2011 vimeongezeka hadi kufikia 12.
Sara amesema kuwa sekta ya afya nayo haikubali nyuma, mwaka 1961 wilaya yake ilikuwa na hospitali moja na kufikia sasa wilaya ina hospitali tatu, vituo vya afya vipo 11, zahanati zipo 99. Amesema kuwa wilaya yake inajivunia sekta hiyo kuendelea kutoa huduma nzuri na chanjo kwa magonjwa mbalimbali kwa mama wajawazito na watoto.