Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wilaya
ya Kilolo imetakiwa kuongeza juhudi katika ujenzi wa madarasa na majengo ya
utawala ili wanafunzi waweze kusoma vizuri bila kubanana jambo linaloathiri ufanisi
katika masomo yao.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipofanya ziara ya
kukagua wanafunzi walioripoti shuleni na hali ya miundombinu ya elimu wilayani
Kilolo jana.
Masenza
alisema “kuna shule za msingi madawati
hayajakamilika na vyumba vya madarasa pungufu. Hii maana yake maafisa watendaji
wa kata na vijiji hawajatimiza wajibu wao”. Afisa utumishi lazima upitie
mipango kazi ya maafisa watendaji wa kata na vijiji ili kujiridhisha kama
wameweka katika mipango ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Aliongeza kuwa zipo baadhi ya shule za msingi zina upungufu wa miundombinu ya
vyoo. Aliutaka uongozi wa wilaya kusimamia ukamilishaji wa miundombinu yote ya
elimu ili iwe chachu kwa walimu kufundisha vizuri na watoto kusoma zaidi.
Mkuu
wa mkoa huyo aliwataka wana Kilolo kuwa wamoja na kufanya kazi kwa umoja ili
kuzitatua changamoto zinazoikabili wilaya hiyo. “Changamoto katika elimu ni nyingi wilayani hapa, umoja wenu ndiyo njia
pekee ya kutatua changamoto hizi” alisema Masenza.
Akiwasilisha
taarifa ya hali ya uandikishaji wanafunzi katika shule ya msingi Utengule,
mwalimu mkuu Grayson Kwayu alisema kuwa wanafunzi walioandikishwa darasa la
kwanza matarajio yalikuwa kuandikisha wanafunzi 76 hadi kufikia tarehe
24/1/2017 jumla la wanafunzi 86 walikuwa wameandikishwa shuleni hapo.
Akiongelea
hali ya uandikishaji darasa la awali, mwalimu Kwayu alisema kuwa matarajio yalikuwa
kuandikisha watoto 96 kwa darasa la awali, hadi kufikia tarehe 24/1/2017 ni
wanafunzi 66 pekee waliokuwa wameandikishwa.
Akiongelea
nyumba za walimu, mwalimu mkuu huyo alisema kuwa shule yake inaupungufu wa
nyumba za walimu tano. Alisema kuwa mahitaji ya nyumba za walimu ni 14 wakati
nyumba zilizopo ni tisa. ”Kamati ya shule
kwa kushirikiana na serikali ya kijiji imeandaa mpango kazi kwa ajili ya
kujenga maboma matano ya nyumba za walimu kwa kipindi cha mwaka 2017-2020”
alisema Kwayu.
Shule
ya msingi Utengule ina jumla ya walimu 14, walimu saba wakiwa wa kiume na
walimu saba wa kike.
=30=