Monday, October 24, 2011

IKAMA YA WATUMISHI 662 IRINGA


MKOA wa Iringa umeidhinishiwa IKAMA ya watumishi 662 katika mwaka wa fedha 2011/ 2012 katika kutekeleza majukumu yake.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Sehemu ya Utumishi na Utawala kwa mwezi Julai hadi Septemba 2011/ 2012 katika kikao cha kudhibiti Mapato na Matumizi ya serikali katika ofisi yake, kwa niaba ya Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Afisa Tawala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Neema Mwaipopo amesema kuwa “kwa kipindi cha Julai- Septemba 2011/ 2012 Sekretarieti ya Mkoa ilipokea IKAMA iliyoidhinishwa mikoa ya Iringa na Njombe”.

Amesema Mkoa wa umeidhinishiwa kuwa na watumishi 662. Amesema kuwa watumishi waliopo ni 578 na nafasi wazi kuwa 84 na kati ya hizo ajira mbadala ni 48 na ajira mpya ni 36.

 Neema Mwaipopo, Afisa Tawala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa

Amesema kuwa mkoa wa Njombe umeidhinishiwa kuwa na watumishi 423 kati ya 71 waliopo na nafasi wazi 352. Amesema kati ya hizo ajira mbadala ni 10 na ajira mpya ni 342. Aidha, amesema kuwa maombi ya kujaza nafasi wazi 378 katika Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa na Njombe na maombi ya kibali cha ajira mbadala 58 yamewasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Akiongelea mafunzo kwa watumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mwaipopo amesema katka kipindi hicho watumishi wanne wameanza kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu katika chuo kikuu cha Tumaini na chuo cha Uhasibu (TIA). Amesema kuwa madhumuni ya mafunzo hayo ni kuimarisha utendaji kazi na ufanisi katika kazi kwa mujibu wa mpango wa mafunzo wa mkoa.

Akifunga kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) amewataka wafanyakazi katika Ofisi yake kufanya kazi kwa umakini mkubwa na uwajibikaji ili kuleta tija katika mkoa na taifa kwa ujumla. Aidha, amewataka kila mtumishi kurejea kipengele kinachomhusu katika Ilani ya uchaguzi ya chama kinachotawala na kuweka utaratibu wa utekelezaji wake.

Kikao cha kudhibiti mapato na Matumizi hufanyika kila baada ya miezi mitatu na hujadili pamoja na mambo mengine mapato na matumizi ya fedha za serikali.

RC AAGIZA MATUMIZI MAZURI YA FEDHA ZA SERIKALI

MKUU wa Mkoa wa Iringa ameagiza matumizi mazuri ya fedha za serikali kadri zilivyopangwa ili ziweze kuwanufaisha wananchi walio wengi katika jitihada za kuondoa umasikini na kuinua maisha ya kila siku.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (Mb.) katika kikao cha robo ya kwanza cha kudhibiti Mapato na Matumizi ya serikali katika ofisi yake kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake. 

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. christine Ishengoma (Mb.)

Dk. Ishengoma aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho amesema “lazima fedha za serikali zitumike vizuri kadri zilivyopangwa hasa upande wa miradi ya maendeleo ili ziwanufaishe wananchi wengi”.
Amesisitiza kufuatwa kanuni na taratibu za kihasibu ikiwa ni pamoja na ulipwaji wa madai mbalimbali kwa muda ili kuongeza ufanisi wa kazi na hatimae mkoa kupata hati safi ya kiukaguzi.

Aidha, Mkuu wa Mkoa ameagiza kufanyiwa kazi mapungufu yote yaliyobainishwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mthibiti mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2009/ 2010 mapema na kuwasilisha taarifa hiyo sehemu husika na kuhakikisha mapungufu hayo hayajitokezi kwa mara nyingine. 

Akiwasilisha taarifa ya Mkaguzi wa Nje kuhusu mapungufu yaliyojitokeza katika ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010 kwa mkoa wa Iringa, Mkaguzi Mkazi, Ismail Mbiru amesema kuwa ripoti hiyo imebaini mapungufu kadhaa yaliyoainishwa kwa kila Halmashauri kwa ajili ya kuyatolea majibu sahihi ili kuleta ufanisi katika kusimamia mapato ya Halmashauri.
Mbiru ameyataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa zenye mapungufu makubwa, taarifa zenye nyaraka pungufu, taarifa za halmashauri ambazo fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo hazijatumika na kuwasilisha taarifa zenye hati zenye shaka.

Mapungufu mengine ameyataja kuwa ni kuwasilisha taarifa yenye wadaiwa wasiolipa na wasiolipwa, kuwasilisha taarifa zenye mishahara isiyolipwa na haikurejeshwa Hazina na kuwasilisha taarifa ya vitabu vya maduhuli ambayo hayajarejeshwa na mawakala wa kukusanya mapato.

Wednesday, October 19, 2011

WELLINGTON HARRISON TURNER GONDWE-Jr


Wellington Harrison Turner Gondwe, alizaliwa tarehe 11 Oktoba, 1987 mjini Morogoro.

Alibatizwa mwaka 1990 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Usharika wa Bugando na alipata Kipaimara mwaka 2001 katika Usharika huohuo.

Alijiunga na shule ya msingi Mlimani mwaka 1994 na kuhitimu darasa la Saba katika Shule ya Msingi ya Lake mwaka 2002.
Aidha, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Murutunguru iliyopo Wilayani Ukerewe mwaka 2003 hadi Juni, 2004.

Baada ya hapo alihamia katika Shule ya Sekondari ya Thaqaafa Julai, 2004- 2006. Kutokana na ugonjwa hakuweza kufanya mitihani yake ya kidato cha Nne iliyotarajiwa kuanza 22 Oktoba, 2006.

Wellington alianza kuugua Malaria kali tarehe 3 Oktoba, 2006. Aidha, alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando tarehe 10 Oktoba, 2006.

Pamoja na jitihada za Madaktari za kunusuru maisha yake kushindikana na roho kushindana na mauti, alifariki tarehe 20 Oktoba, 2006 saa 12 kamili jioni.

BWANA alitoa na BWANA ametwaa jina lake lihimidiwe.


WATUMISHI WA UMMA NA HUDUMA BORA


Watumishi wa Umma wamekumbushwa kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii na kuhakikisha jamii inaridhika na huduma hiyo pamoja na changamoto zilizopo.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. George Masaju (kulia) akiongea na wafanyakazi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa hawapo pichani na Kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bw. Aseri Msangi (kushoto)
Masaju amesema “tunatambua kuwa sisi ni watumishi wa Umma na tuna maadili yetu ya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 na mabadiliko yake Na. 17 ya mwaka 2007”. Amesema kwa msingi huo wa utumishi wetu wa Umma “sote kwa pamoja lazima huduma zetu tuzitoe kwa ubora na kwa viwango vya kuridhisha kwa Umma”.
Amesema “nawajibika kuwakumbusha wajibu wetu sote kwa Serikali na tukumbuke kuwa sisi ndio watendaji wa kuwasaidia viongozi wetu wa juu”.
Aidha, amewakumbusha kuwa wafanyakazi katika ngazi za mikoa na Halmashauri ndio walio karibu zaidi na wananchi hivyo wanawajibika kufanya kazi kwa uwezo wao na viwango kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema utoaji wa huduma bora kwa wananchi unasaidia katika kuondoa kero na kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya Serikali yao.
Akisisitiza dhana ya ubora wa huduma kwa wananchi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa ubora huo ujikite katika utoaji wa maamuzi sahihi na yanayotolewa katika muda muafaka.
Ametolea mfano wa huduma zikitolewa vizuri katika idara ya polisi na mahakama kutasaidia kupunguza uhalifu.
Vilevile, amesisitiza kuwa jukumu la kudhibiti uhalifu nchini si la idara ya polisi na mahakama pekee bali ni jukumu linalohitaji msukumo wa pamoja baina ya mamlaka zinazohusika na wananchi kwa umoja wao.

Sunday, October 9, 2011

KKKT DAYOSISI YA KUSINI KUJENGA CHUO KIKUU

Askofu mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kusini Njombe ameazimia kuanzisha ujenzi wa chuo kikuu cha dayosisi katika ukanda wa kusini ili kuendeleza na juhudi za kanisa katika kuiletea jamii ustawi.
Kauli hiyo imetolewa na Askofu mteule Isaya Japhet Mengele baada ya kusimikwa kazini na Mkuu wa KKKT nchini Askofu. Dk. Alex Malasusa katika kanisa kuu, Dayosisi ya Kusini-Njombe.
Akiongelea mipango yake ya baadae Askofu Mengele amesema ni ujenzi wa chuo kikuu cha dayosisi katika ukanda huo wa kusini ili kuwanufaisha wananchi wengi katika sekta ya elimu.
Aidha, akiongelea dhana ya kilimo kwanza, Askofu. Mengele ameipongeza serikali kwa hatua hiyo na kuishauri kuwa kilimo kwanza ili kitoe matokeo mazuri kifanyike kwa kanda kutokana na mazao yanayozalishwa katika kanda husika ili kuongeza chachu na kuinua kilimo ili kiwanufaishe wananchi wengi zaidi.
Akiongelea sekta ya elimu amesema ataendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha utoaji wa elimu nchini. Aidha, ameishauri Serikali huongeza kasi katika kuifanya hospitali teule ya Ilembula kuwa hospitali ya rufaa ikiwa ni pamoja na kuisaidia gari la kubebea wagonjwa ili kuwasaidia wananchi wengi.
Katika salamu za Mkoa wa Iringa, zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amempongeza Askofu mteule Mengele kwa uteuzi wake. Aidha, amewaomba viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wao kukaa chini na kutafakari juu ya nchi na kuiombea ili iendelee kuwa na amani, upendo na utulivu.
Vilevile, Dk. Ishengoma imelishukuru kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania kwa michango na ushiriki wake katika kuiletea maendeleo jamii. Ameitaja michango hiyo kuwa ni pamoja na kuijenga jamii katika maadili na kuwafanya wananchi wake kuwa raia wema, mingine ni elimu na afya. 
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika aliyemuwakilisha Waziri Mkuu aliyepo safarini nchini Brazili amewataka viongozi wa dini kukemea maovu, na kuwataka waumini kufuata mfundisho ya dini na kujitolea kulijenga kanisa lao na nchi yao.

RASILIMALI ZA NCHI ZIWANUFAISHE WANANCHI

Serikali imeshauriwa kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kwa maslahi ya nchi na kuwanufaisha wananchi wenyewe walio wengi.
Ushauri huo umetolewa na Askofu mteule wa Dayosisi ya Kusini- Njombe, Askofu. Isaya Japhet Mengele katika ibada ya kumsimika na kumuingiza kazini msaidizi wa Askofu, Mch. Dk. George Mark Fihavango iliyoongozwa na Mkuu wa KKKT nchini Askofu. Dk. Alex Malasusa iliyofanyika katika kanisa kuu, Dayosisi ya Kusini Njombe.
Askofu. Mengele amesema kuwa rasilimali za nchi zinapogawanywa kwa maslahi ya nchi na wanufaikaji wakawa ni wananchi, nchi hutawaliwa kwa amani na utulivu. Aidha, ameshauri pia migodi itakayoanzishwa katika ukanda wa kusini mwa nchi, uanzishwaji, uratibu na usimamizi wake lazima uwe mzuri ili kuepusha migogoro inayoshuhudiwa katika ukanda wa kaskazini mwa nchi.
Akiongelea uhifadhi wa mazingira, amesema kuwa ni muhimu kwa Serikali na wadau wengine wote wa maendeleo na wenye mapenzi mema na nchi hii kutilia mkazo dhana ya uhifadhi wa mazingira ili kuinusuru nchi na uharibifu unaotokana na uharibifu wa mazingira ili nchi iwe mahali salama kwa ustawi wa binadamu wake.
Askofu mteule Mengele ameipongeza Serikali katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na kusifu Serikali kutojiingiza katika masuala la kidini hali inayochangia ukuaji na ustawi wa uhuru wa kuabudu unaoendana na misingi ya kidemokrasia nchini.
Akimsimika rasmi, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Askofu. Dk. Alex Malasusa amewataka viongozi wa dini kutokutumia nafasi zao kwa maslahi ya kisiasa.
Katika salamu za Mkoa wa Iringa, zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amempongeza Askofu mteule Mengele kwa uteuzi wake. Aidha, amewaomba viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wao kukaa chini na kutafakari juu ya nchi na kuiombea ili iendelee kuwa na amani, upendo na utulivu.
Vilevile, Dk. Ishengoma imelishukuru kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania kwa michango na ushiriki wake katika kuiletea maendeleo jamii. Ameitaja michango hiyo kuwa ni pamoja na kuijenga jamii katika maadili na kuwafanya wananchi wake kuwa raia wema, mingine ni elimu na afya. 

Saturday, October 8, 2011

MKUU WA MKOA WA IRINGA AONGEA NA WAZEE NA VIONGOZI WA DINI IRINGA

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amewaomba wazee wa Mkoa wa Iringa kumpatia ushirikiano wa kutosha katika jukumu lake la kuuongoza Mkoa huo kwa pamoja waweze kuuletea maendeleo.
Dkt, Ishengoma ameyasema hayo alipoongea na wazee wa Iringa alipokutana nao katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (kulia) akiongea na wazee wa Mkoa wa Iringa, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Aseri Msangi
Dkt. Ishengoma amesema kuwa wazee ni hazina kubwa katika Mkoa hivyo ushirikiano wao ni muhumu sana katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo. Amesema “ninaamini kuwa wazee ni chachu ya kuleta maendeleo kwa sababu mumefanya kazi kwa muda mrefu na kukutana na changamoto na mambo mengi katika Mkoa wetu wa Iringa”.
Mkuu huyo wa Mkoa amewafahamisha wazee hao kuwa Ofisi yake ipo wazi muda wote kwa ajili ya kupokea ushauri, kushauri na kushauriana katika mambo ya kuuendeleza Mkoa wa Iringa.
Aidha, amechukua fursa hiyo kuwafahamisha wazee hao kuwa Mkoa unatarajia kuadhimisha maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru tarehe 7 hadi 9 Novemba, 2011 itakayoenda sambamba na kukimbiza Mwenge wa Uhuru Mkoani Iringa. Amesema mwaka huu tofayuti na miaka mingine Mwenge wa Uhuru hautakimbizwa Mkoa mzima bali utakimbizwa katika makao makuu ya Mkoa na Iringa utakesha katika uwanja wa Samora.
Wakati huohuo Mkuu huyo wa Mkoa wa Iringa amekutana na viongozi wa madhehebu ya dini ya Iringa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa majira ya mchana.
Dkt. Ishengoma amesema “viongozi wa dini ndio mliowashika watu hivyo tukishirikiana kwa pamoja mambo yanayohusu maendeleo yatafikiwa haraka”. Amesema kuwa ushirikiano huo baina ya Serikali na madhuhebu ya dini utasaidia hata malezi ya vijana kwa sababu vijana wengi wanaokengeuka wanatoka katika madhehebu ya dini yanayoongozwa na viongozi hao.
Wazee wa Mkoa wa Iringa wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Iringa (hayupo pichani) 
Askofu wa Kanisa la Aglikana Dayosisi ya Ruaha, Bw Joseph Mgomi amesema kuwa Dayosisi yake imekuwa ikifanya kazi nyingi za kijamii kwa kushirikiana na Serikali ili kumletea maendeleo mwananchi wa Iringa na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali. Amesema miongoni mwa shughuli hizo kuwa ni miradi ya maji na kilimo.  

MUFINDI WASHAURIWA KUANZISHA CHUO KIKUU

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewashauri wanamufindi kuangalia uwezekano wa kuwa na chuo kikuu ili kuwasogezea karibu huduma hiyo muhimu wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na watumishi wa Serikali kuu, Halmashauri na taasisi mbalimbali katika ukumbi mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Karibu Wilayani Mufindi, Mhe. Mkuu wa Mkoa
Dkt. Ishengoma amesema “pamoja na kuwa na mafanikio makubwa katika nyanja za uzalishaji na uchumi, Mufindi tufikirie kuwa na chuo kikuu”. Amesema kuwa chuo kikuu ni muhimu sana katika kuzalisha wanataaluma watakaosaidia kusukuma zaidi gurudumu la maendeleo Wilayani hapo. Amesema uanzishwaji wa chuo kikuu Wilayani Mufindi utawasaidia wananchi wengina wa maeneo ya jirani kuvutika katika kujiendeleza kielimu.
Akiongelea sekta ya maji, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa sekta hiyo bado inaasilima zilizo chini jambo linalowakoshesha wananchi wengi huduma hiyo. Amesema “kwa pamoja ni lazima tujitahidi ili kuongeza kasi ili tufikie malengo ya matakwa ya sera ya maji”.
Aidha, ameishauri Halmashauri hiyo kuangalia vyanzo vingine vinavyoweza kuiletea mapato ili kuiwezesha Halmashauri hiyo kujiendesha vizuri zaidi. Amesema kuwa Halmashauri inapojiimarisha kimapato inapanua wigo wake wa utoaji huduma kwa wananchi na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Mufindi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista Kalalu amesema kuwa ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400, wilaya yake imeongeza miradi ya maji na kuongeza idadi ya watu wenye uwezo wa kupata maji safi na salama kutoka asilimia 40 mwaka 2005/2006 kwa wakazi wa mjini, hadi asilimia 53 mwaka 2010/2011. Aidha, idadi imeongezeka kutoka asilimia 56 mwaka 2005/2006 kwa wakazi wa vijijini, hadi asilimia 61 mwaka 2010/2011.


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista kalalu akisisitiza jambo

Amesema kuwa miradi hiyo ni ya uchimbaji wa visima 35 ambavyo vimewapatia maji wananchi wapatao 8,750 pamoja na ujenzi wa mtego mmoja wa maji ambao unawanufaisha wananchi 2000.
Bibi. Kalalu amesema kuwa uhifadhi wa vyanzo vya maji na rasilimali za maji umeongezeka kutoka vyanzo 100 vilivyokuwa vimehifadhiwa mwaka 2005 hadi kufikia vyanzo 705 mwaka 2010.  Amesema vyanzo hivyo ni vile ambavyo hutiririsha maji yake katika mto wa Ruaha.

Friday, October 7, 2011

TUMIENI SKIMU YA MWAGILIAJI -RUAHA MBUYUNI



Wananchi wa Kata ya Ruaha Mbuyuni wametakiwa kuitumia skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni kwa shughuli za kilimo ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi.

Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za kilimo katika skimu hiyo ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni iliyopo katika kata ya Ruaha Mbuyuni.

Dkt. Ishengoma amesema “Ruaha Mbuyuni mnalo bonde zuri sana ila halitumiki ipasavyo kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji, lazima hali za wanaruaha mbuyuni zibadilike kutokana nakuinuka baada ya serikali yenu kuwatengenezea mrefeji na banio la maji”. Amesema baada ya kulitembelea bonde hilo na skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni ni dhahili kuwa shuguli za kilimo bado kipo chini sana na kushauri hamasa itolewe kwa wananchi kuitumia skimu hiyo kwa kilimo cha kisasa ili waweze kuvuna zaidi ya mara moja.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji wa kijiji cha Ruaha Mbuyuni Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Nassoro Almasi amesema kuwa mwezi Aprili mwaka 2008 mto Lukosi ulihama katika mkondo wake wa asili na kuacha miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo banio kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha ukanda wa juu wa Wilaya ya Kilolo. 

Amesema kuwa madhara ya mvua hizo yalisababisha ekari 500 za mazao ya chakula ambayo ni mahindi, mpunga, maharage, vitunguu, nyanya na mbogamboga kuathirika kwa ukame na kusimamisha shughuli za kilimo.

Skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni ilianza miaka ya sabini baada ya wakulima wenyewe kuchepusha maji kwa kutumia mawe, magogo, matete na majani ili kumwagilia mashamba yao. 


KILOLO DHIDI YA UKAME


Wilaya ya Kilolo imeshauriwa kulima mazao yanayovumilia ukame ili kukabiliana na ukame unaoendelea kuinyemelea wilaya hiyo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa Serikali kuu na Halmashauri Wilayani Kilolo alipofanya ziara ya kujitambulisha na kuzifahamu changamoto zinazoikabili Wilaya hiyo.

Dkt. Ishengoma amesema “lazima tutafute mazao yanayostahimili ukame, lazima twende katika kilimo cha mtama”.  Amesema “lazima tumfikirie mwananchi wa Kilolo atapataje chakula cha kutosha, bahati mbaya huwa sipendi sana tabia ya kuomba omba chakula cha msaada sababu si staha kwa mtu mzima”.

Aidha, ameishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kuangalia uwezekano wa kununua mbegu bora za mtama na kuweka utaratibu mzuri ambao watautumia kwa wakulima ili uweze kuwanufaisha. Amesema kwa mujibu wa vituo vya utafiti mbegu bora ya mtama si nyingi sana kwa sababu sehemu nyingi za nchi zimekumbwa na ukame na kusababisha maeneo mengi kulazimika kununua mbegu ya mtama.

Ameushauri uongozi wa Wilaya ya Kilolo kuwashawishi wananchi kununua mbegu bora za mtama na kuzipanda kwa vitendo. 

Mkuu huyo wa Mkoa amesema “tumepata njaa kwa sababu hatutumii kilimo cha umwagiliaji”. Amesisitiza matumizi mazuri ya skimu za umwagiliaji ili kujihakikishia chakula cha kutosha. Kilimo cha umwagiliaji kinamuwezesha mkulima kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka na kujihakikishia uhakika wa chakula.
Akiongelea usindikaji wa mazao amesema kuwa usindikaji huo unaongeza thamani ya mazao husika. 

Amewataka maafisa Mipango kushirikiana na kuandika maandiko ya miradi midogo midogo ili kuweza kuyaongezea mazao thamani. Amesema “ni lazima tuweke mikakati ya kuwainua wananchi, si lazima mpaka wananchi waibue wenyewe sisi wataalamu tunaweza kuwajibika kwa niaba ya wananchi”.    

Wednesday, October 5, 2011

WALIMU ONGELEENI HIV/UKIMWI

Waalimu Mkoani Iringa wameshauriwa kutenga dakika tano katika ratiba zao za vipindi ili kuzungumza suala mtambuka la ugonjwa wa UKIMWI ili kuinusuru jamii dhidi ya janga hilo.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali la SUMASESU lenye makao yake makuu Wilayani Makete pamoja na watumishi wa Serikali kuu, Halmashauri na taasisi za kidini.
  Bw. Egnatio Mtawa, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMASESU Makete akisoma taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (hayupo pichani)

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Ishengoma amesema kuwa “tuendelee kutoa elimu shuleni ili kukabiliana na ugonjwa wa UKIMWI”, aidha, ameshauri “walimu wa Sekondari kutenga angalau dakika 5 hadi 10 kuzungumzia masuala ya ugonjwa wa UKIMWI”.
Kuhusiana na uhusiano wa mila na desturi dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mila na desturi ni nzuri sana ila tatizo lipo katika zile zinazopotosha. Ameshauri kuwa mila na desturi zote zinazopotosha lazima ziwekwe kando ili jamii iwe salama.
Mkuu wa Mkoa amepongeza ushirikiano baina ya Serikali na SUMASESU katika sekta ya maendeleo ya jamii Wilayani Makete wenye lengo la kuijengea jamii uwezo na kuwa na maendeleo endelevu.
Katika taarifa fupi ya shirika la SUMASESU kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa iliyotolewa na Mkurugenzi wa SUMASESU, Bw. Egnatio Mtawa amesema shirika lake linatekeleza miradi mikubwa miwili ambayo ni Mradi wa Ujana unaofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia shirika la fhi 360 na mradi wa usalama wa chakula unaofadhiliwa na shirika la Mkate kwa Dunia la Ujerumani.
Amesema kuwa mradi wa ujana unashughulika na utoaji elimu kwa jamii ili kujikinga na maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI, elimu ya afya ya uzazi na unyanyasaji wa kijinsia.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Makete, Bibi. Zainabu Kwikwega amesema kuwa lengo la kutembelea shirika hilo la SUMASESU ni kumuelezea Mkuu wa Mkoa shughuli zinazofanywa na shirika hilo kwa wanamakete pamoja na kuwatia moyo ili waendelee na utoaji huo wa huduma kwa wakazi wa Makete.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (kulia) akisalimiana na viongozi wa Wilaya ya Makete alipofanya ziara ya kujitambulisha wilayani humo.
       

Tuesday, October 4, 2011

RC RUVUMA AONGEA NA WAANDISHI WA HABARI

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe Said Thabit Mwambungu amesema kuwa Serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na waandishi wa habari katika ujumbe wa serikali kwa wananchi ili kusukuma gurudumu la maendeleo. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Said Mwambungu akiongea na waandishi wa habari Ofisi kwake

Mhe. Mwambungu amesema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wa Manispaa ya Songea Ofisini kwake hivi karibuni 
Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amewataka waandishi hao wa habari kuendelea kuhabarisha Umma wakizingatia maadili ya habari kwani kwa kukiuka maadili wanaweza kuipotosha jamii na kusababisha hatari katika jamii.
Kwa upande wake Katibu wa Ruvuma Press Club Bw. Andrew Chatwanga  amempongeza  Mkuu wa Mkoa kwa uamuzi wake wa kuongea na wanahabari hao ikiwa ni siku chache tu baada ya kuripoti mkoani kuanza kazi ya kuongoza shughuli za Serikali mkoani hapo.
Bw. Chatwanga alitumia fursa hiyo kumwomba Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za kipekee ili kuifanya Manispaa ya Songea inaboreka kwa usafi wa mazingira kama alivyofanya kwa Manispaa ya Morogoro. Kwa sasa Manispaa ya Songea usafi wa mazingira hauridhishi.

Habari hii ni kwa hisani ya Revocatus A. Kasimba, Afisa Habari, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa

LUDEWA NI PEMBEZONI NA WAPI?? AHOJI RC

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma ametofautiana na uongozi wa Wilaya ya Ludewa katika dhana inayoendelea kuwa Wilaya ya Ludewa ipo pembezoni.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amehoji alipokuwa akizungunza na watumishi na wananchi wa Wilaya ya Ludewa alipofanya ziara ya kujitambusha na kuzifahamu changamoto zinazoikabili Wilaya ya Ludewa.
Dkt. Ishengoma amesema “kuanzia sasa Ludewa hatupo pembezoni”. Aidha, amehoji kuwa Ludewa ipo pombezoni na wapi? Ameendelea kuhoji kuwa “kama Ludewa ipo pembezoni je, mwanzoni ni wapi”.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.) akiongea na watumishi na wananchi wa Wilaya ya Ludewa
Amesema kuwa maendeleo ndiyo dira inayoipeleka Wilaya pembezoni au mwanzoni. Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Wilaya na hali halisi aliyokutana nayo njiani inaonesha kuwa Wilaya hiyo inayo maendeleo yanayoonekana na kupimika.
Amewataka viongozi na wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuachana na dhana hiyo kwani inawafanya kujiona kuwa ni wanyonge na hivyo kujiweka pembeni na dhana ya maendeleo na uwajibikaji kikamilifu.
Aidha, amewataka wanaludewa kuchangamkia fursa iliyopo ya ujenzi wa viwanda na machimbo Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma ili kujumuika katika mchakato wa kujiletea maendeleo.
Akiongelea kero inayowakabili wananchi wa Wilaya hiyo ambayo ni barabara, amesema kuwa barabara za Wilaya hiyo zitajengwa kwa sababu zimeainishwa katika ilani ya uchaguzi ya chama tawala.
Dkt. Ishengoma ametoa ombi kwa watumishi wote wa Umma kuendelea kuipenda serikali yao kwa sababu inawajali na kutekeleza mahitaji yao ikiwa ni pamoja na kuwaletea maendeleo. Vilevile, amewataka kuwajibika kwa serikali yao kwa kuchapa kazi kwa bidii.
Akiongelea miradi ya maendeleo, amewataka watumishi na viongozi wanaosimamia miradi ya maendeleo kwa kutekeleza wajibu huo kulingana na thamani halisi ya fedha za Umma zinazotolewa.
Awali akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Ludewa, Mkuu wa Wilaya hiyo Bibi. Georgina Bundala amesema kuwa Wilaya yake inajishughulisha na shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kilimo (90%), biashara (3%), uvuvi, sekta binafsi (4%) na ajira rasmi (3%).  Amesema kuwa Wilaya yake ina fursa nyingi zinazohitaji kuendelezwa ili ziweze kuchangia katika pato la Wilaya na uchumi wa mwananchi. Amezitaja fursa hizo kuwa ni utajiri mkubwa wa madini ya chuma, makaa ya mawe, dharabu, chokaa na vito mbalimbali vya thamani.
Bibi. Bundala amesema kuwa kwa takwimu za mwaka 2008 wastani wa pato la mwananchi Wilayani Ludewa lilikuwa ni shilingi 125,000 kwa mwaka. Amesisitiza kuwa pato hilo ni dogo sana kukidhi mahitaji muhumu ya kibinadamu. Amesema kuwa mkakati wa Wilaya yake ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kuongeza pato la mwananchi kuendana na viwango vya kimataifa.
Amesema kuwa Wilaya yake inaendelea kuhamasisha jamii kuweza kukuza kilimo cha kahawa, pareto, chai, korosho, alizeti, ufuta, karanga na kupanua kilimo cha umwagiliaji.
=30=

'LUDEWA ONGEZENI KASI KATIKA MAENDELEO ASEMA RC'

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameitaka Wilaya ya Ludewa kuongeza kasi katika kujiletea maendeleo kutokana na kuwa na rasilimali nyingi na ardhi nzuri inayofaa kwa shughuli za kilimo.
Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika sekondari ya Mavanga katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kuzitembelea Wilaya za Mkoa wa Iringa akianza na Wilaya ya Ludewa.
Dkt. Ishengoma amesema “Ludewa ni Wilaya nzuri kwa kilimo na imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi pamoja na madini mengi”. Amesema kuwa Wilaya hiyo inabahati ya kuwa na madini ya makaa ya mawe na  chuma pamoja na madini mengine.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.)(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa BIBI. Georgina Bundala (kulia) wakibadilishana mawazo walipotembelea eneo la Chuma cha Liganga wilayani Ludewa.
Vilevile, amewataka wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuchangamkia fursa zitokanazo na madini hayo hasa pale yatakapoanza kuchimbwa rasmi. Amesema kuwa viwanda vikianza kujengwa lazima viwanufaishe wananchi wa Ludewa kwa wao kuchangamkia fursa za ajira pasipo kubweteka ili maisha bora yawezekane kwao. Amesisitiza kuwa maisha bora hayatawezekana kwa wananchi kubweteka ila pale tu watakapojishughulisha kwa kufanya kazi kwa bidii.
Akiongelea elimu Dkt. Ishengoma amewataka wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa sababu sekta hiyo inamuwezesha mwananchi kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Amesema kuwa wananchi wanawajibika katika kuendeleza sekta ya elimu kwa kusaidiana na serikali yao ili kuinua kiwango cha elimu Wilayani hapo. Amesema “katika kumuwezesha mwananchi kukabiliana na changamoto za leo za kimaisha ni lazima kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuwa elimu inampelekea mwananchi katika kupata ufumbuzi wa changamoto za kimaisha”.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Bibi. Georgina Bundala amesema kuwa wananchi wa Wilaya ya Ludewa ni wasikivu na wachapa kazi sana hasa wanapopatiwa maelezo sahihi kutoka kwa viongozi wao wanaowasimamia na wataalamu. Amesema kuwa Wilaya yake imejikita katika shughuli kadhaa za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kilimo, uvuvi, ufugaji na ujasiliamali.
=30=

RC ASISITIZA MASOMO YA SAYANSI LUDEWA

Mkuu wa Mkoa wa Iringa awataka wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lugarawa kitilia mkazo masomo ya sayansi ili waweze kulitumikia taifa katika fani hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akifungua daharia ya wasichana katika shule ya sekondari ya Lugarawa iliyopo katika kata ya Lugarawa Wilayani Ludewa.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa wanafunzi wengi hasa wa kike wamekuwa wakiyakimbia masomo ya sayansi kwa kisingizio cha ugumu wa masomo hayo jambo alilolikanusha. Amesema “masomo ya sayansi si magumu kama yanavyodaiwa na wengi, masomo yote yanahitaji juhudi na kujituma ili kuweza kufaulu”.  Amesisitiza kuwa elimu ni msingi wa maisha na maendeleo katika kila jamii inayohitaji kustaarabika.
Amesema “wazazi wamekuwa wakijitahidi kujenga miundombinu ya kielimu kama shule, maabara na daharia kutokana na mapenzi yao kwenu (wanafunzi)”. Amesisitiza kuwa kwa msingi huo wanafunzi nao wanajukumu la kurudisha shukrani zao kwa wazazi kwa kufauli vizuri mitihani yao na hatimae kuwa raia wema watakaolijenga taifa lao.
Aidha, amewataka wazazi na jamii ya Ludewa kugeukia pia uwekezaji katika ujenzi wa daharia za wavulana kwa sababu nazo ni muhimu sana katika kudhibiti makuzi ya wanafunzi hao wavulana.
Kwa mujibu wa taarifa ya wananchi wa Kata ya Lugarawa iliyowasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ujenzi wa daharia hiyo ulianza mwaka 2008 hadi mwaka 2010 lengo likiwa ni kuwawezesha wanafunzi wa kike 48 katika shule hiyo kukaa shuleni na kufuatilia masomo yao na kuepukana na hadha za kukaa nje ya shule ikiwa ni pamoja na kupata mimba.
Daharia hiyo iligharimu shilingi milioni 30,785,500 na wananchi wamechangia kiasi cha shilingi milioni 28,085,500 zikiwa ni gharama za kufyatua tofari na fedha taslimu. Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ilichangia shilingi milioni 2,700,000 kwa upigaji bati na saruji.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, yupo katika ziara ya kujitambulisha na kuzifahamu changamoto zinazozikabili Wilaya za Mkoa wa Iringa na kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo.
=30=

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.)(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Bibi. Georgina Bundala (kushoto) wakibadilishana mawazo alipowasili Wilayani Ludewa.

Monday, October 3, 2011

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati) alipowasili Mavanga Wilayani Ludewa na kupokelewa na viongozi wa Wilaya 

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.) (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Georgina Bundala katika Kata ya Mavanga 

Wasomi wakisoma shairi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (Mb.) alipowasili Wilayani Ludewa katika ziara ya utambulisho

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII


TAARIFA KWA UMMA

ASALI YA TANZANIA NI NZURI NA INAYO
UBORA WA KIMATAIFA

Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kuwa asali ya Tanzania ni nzuri kwa matumizi ya binadamu na kuwa ina viwango vya ubora vya kimataifa. Ukweli huu umedhihirishwa na maabara mbalimbali duniani, hasa zile za Jumuiya ya Ulaya ambao ndio wanunuzi wakubwa wa asali ya Tanzania.
Ufafanuzi huu unatolewa kufuatia taarifa ya hivi karibuni kupitia baadhi ya vyombo vya habari iliyosema kuwa kuna asali kutoka Tanzania ambayo ilikataliwa nchini China baada ya kuonekana kuwa na kemikali ya Nicotin. Wizara haina taarifa na asali hiyo maana haijatoa kibali chochote cha kusafirisha asali kwenda nchini China kwa miaka ya karibuni. Kisheria asali hairuhusiwi kusafirishwa kwenda nchi za nje bila kupata kibali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kupitia Mpango wa udhibiti Kemikali Katika Asali (Chemical Residue Monitoring Plan) Wiraza ya Maliasili na Utalii inahakikisha kuwa asali ya Tanzania inakidhi viwango vya ubora wa kimataifa. Wizara hukusanya sampuli za asali kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuzifanyia uchambbuzi kwenye maabara teule (Accredited Laboratory) na matokeo yake yanapelekwa  kwa wanunuzi, hasa  Umoja wa nchi za Ulaya ambao ndio wanunuzi wakubwa wa asali ya Tanzania.
Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi 4 za Afrika zinazoruhusiwa kuuza asali yake katika nchi za Umoja wa Ulaya. Kwa mfano, taarifa zinaonyesha kuwa asali inayozalishwa mkoani Tabora haijawahi kupatikana na kemikali ya Nicotin, wala kemikali yoyote inayodhuru binadamu.
Ili kudumisha ubora wa asali ya Tanzania Wizara inazingatia yafuatayo kabla ya kutoa Kibali cha kusafirisha asali kwenda nchi za nje:
  • Asali inakaguliwa na wataalam wa nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii;
  • Asali inapimwa na kuchunguzwa kwenye maabara za hapa nchini na nchi za nje kabla ya kusafirishwa;
  • Kibali cha kusafirisha kinatolewa kufuatana na taarifa ya maabara.
Tarifa za maabara zinaonyesha kila mwaka kuwa asali ya Tanzania haina kemikali zozote zinazoweza kudhuru. Sababu mojawapo inayoifanya asali ya Tanzania iwe na ubora wa asili ni kwa kuwa inazalishwa mbali kutoka kwenye mashamba yanayotumia kemikali. Kwa mfano zaidi ya  aslimia 90 ya asali ya Tabora huzalishwa kwenye mapori ya akiba na misitu ya hifadhi  (Game , Forest Reserves).
Kwa mfano, katika Wilaya ya Sikonge asali huzalishwa katika Misitu ya Hifadhi ya  Nyahua, Ugunda, Uwala na Iswagala. Katika Wilaya ya Urambo asali huzalishwa katika pori la akiba la Ugala na Myovosi/Kigosi na Misitu ya Hifadhi ya Mpanda line, North Ugala, na Igombe. Aidha katika Wilaya ya Uyui asali huzalishwa kwenye Misitu ya Hifadhi ya Igombe, Ilomelo Urumwan na Goweko. Katika maeneo yote haya  wafugaji nyuki hutundika mizinga zaidi ya kilomita 60 kutoka makazi na mashamba ya tumbaku.
Aidha, ufugaji nyuki husimamiwa na Sheria ya Ufugaji Nyuki Namba 15 ya mwaka 2002 ambayo inakataza kufuga nyuki karibu na mashamba yanayotumia kemikali. Inasisitizwa kuwa ufugaji nyuki ufanyike umbali wa kipenyo cha kilomita 7 kutoka mashamba ya tumbaku au mengine yanayotumia viwatilifu.
Sheria hii inatuhakikishia ubora zaidi kuliko Sheria za kimataifa ambazo zinakataza kuzalisha asali katika kipenyo cha kilometa 3 tu. Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Halimashauri za Wilaya inawaelimisha wafugaji nyuki kupitia ughani (Extension Services) kuhusu umuhimu wa kufuga nyuki kwa kuzingatia Sheria ya Ufugaji Nyuki.
Wizara inawakumbusha wafanyabiashara taratibu za kufuata ili kuuza mazao ya nyuki nchi za nje:
  1. Awe na Kampuni ya biashara iliyosajiliwa;
  2. Awe amesajiliwa kama mfanyabiashara wa mazao ya nyuki;
  3. Awe na leseni halali ya Biashara;
  4. Awe na kitambulisho cha mfanyabiashara (TIN);
  5. Awe amepata umepata soko nchi za nje na kuonyesha bei yake;
  6. Ubora wa mazao yake yahakikiwe na Wizara ya Maliasili na Utalii na kupewa kibali cha kusafirisha nje ya nchi.
Ili kudumisha ubora wa mazao ya nyuki wafugaji na wafanyabiashara wanatakiwa kuzingatia utaalam wa ufugaji nyuki, usafirishaji na ufungashaji. Utaalam huo hutolewa bure na wataalam wa Ufugaji Nyuki.
Inasisitizwa kuwa wafanyabiashara wote wanatakiwa kupata kibali cha kusafirisha asali nje ya nchi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.


George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 21 Septemba 2011